Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madhara ya kukimbia na raba za kubana

Raba Za Kubanann Madhara ya kukimbia na raba za kubana

Mon, 24 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni hatua nzuri kwa yule ambaye hivi sasa amekuwa na mwamko wa kufanya mazoezi ya kukimbia kidogo kidogo kwa kundi au binafsi katika maeneo ya wazi au yale ya pembezoni mwa barabara za huduma.

Kama ulikuwa hujui ni kuwa zoezi la kukimbia kidogo kidogo ndio zoezi rahisi kufanyika na mamilioni ya watu duniani ikiwamo wazee kwa vijana hatimaye kuwaweka katika afya bora na kuishi maisha marefu.

Afya ni mtaji na ni mali, ukifanikiwa kuwa na afya bora maana yake unaokoa fedha nyingi ambazo pengine ungeweza kuzitumia kukabiliana na mwili usio na afya njema unapopata magonjwa hasa yale yasiyoambukiza ambayo ni gharama kubwa kwako na kwa nchi.

Kukimbia ni zoezi jepesi na pia ni burudani, ndio maana wakimbiaji wa kisasa wamekuwa wakijipenda na kutinga katika mazoezi hayo wakiwa na mavazi nadhifu ya kimichezo ikiwamo raba kali za kukimbilia.

Katika kona hii ya mbio nyepesi au kwa Kiingereza Jogging, jicho la spoti dokta leo litalenga uvaaji wa raba zakubana kuliko kile kiwango kinachopendekezwa na Wataalam wa Afya za wanamichezo.

Moja ya nyenzo muhimu ya mkimbiaji wa mbio nyepesi za kujenga na kuboresha afya ya mwili ni raba anayoitumia katika mazoezi haya yanayokuepusha na magonjwa yasiyoambukiza kama Kisukari.

Ni kawaida mitindo ya uvaaji wa kisasa kuwa na nguvu mpaka kuushinda ushauri wa wataalamu wa afya na matokea yake kutofuatwa na wanamichezo wakimbiaji wa mbio nyepesi.

Wapo baadhi ya wanamichezo hasa vijana wanaopenda waonekane wana miguu midogo na hivyo kujikuta wakivaa viatu vinavyowabana pasipo kujua kuwa uvaaji huo una madhara kiafya katika miguu.

Kuvaa viatu vya michezo vya kubana kiujumla huwa na matokeo hasi kwa afya ya miguu ikiwamo maumivu baada ya kumaliza kucheza au wakati wa kucheza. Kutokana na maumbile ya kiasili ya miguu eneo la chini ya ungio la kifundo cha mguuu ndilo linaloathirika zaidi ikiwamo vidole vya miguuni hasa dole gumba.

Madhara mbalimbali ya kiafya huibuka kutokana na viatu hivyo kubana katika seheme za mguu ikiwamo kucha, vidole, misuli, ngozi, nyayo, maungio ya vidole, kisigino, mishipa ya damu na fahamu.

Kitendo cha kiatu kubana mishipa ya damu na ya fahamu katika eneo la mguu eneo la kifundo ina maana tishu za eneo hilo litakosa lishe yakutosha na huku pia mipitisho ya fahamu kuzuia au kubanwa.

Mara nyingi viatu vya kubana vinaweza kuwa vyembamba au vifupi sana kuliko ile saizi halisi ya mvaaji na pia eneo la mbele kuwa na upana mdogo au kuchongoka sana.

Mgandamizo wa viatu vya kubana huweza kusababisha kucha kukua vibaya na kuchimba katika kitako cha kucha na kusababisha jeraha.

Baadaye jeraha hilo huvamiwa kirahisi na bakteria na kutengeneza uambukizi mkali wa kidole ambao husababisha maumivu makali, homa, kuvimba na kuleta usaha.

Viatu hivyo vikivaliwa mara kwa mara hutengeneza magaga au mipasuko katika nyayo hasa katika eneo la kisigino, kitabibu tatizo hili huitwa Cons and Calluses.

Baadaye tatizo lingine huibuka ambalo ni vidole gumba kuwa na mtutumko na kuota vinundu katika vifupa vya vidole vya miguuni na kuharibu umbile asilia la vidole ikiwamo kupinda.

Hali hii huleta ulemavu wa kudumu katika ungio la kidole gumbakitabibu hujulikana kama Bunion na likitokeo katika ungio la kidole cha tano hujulikana kama Bunionettes.

Lipo tatizo linalojulikana kama Metatarsalgia ambalo haliwezi kuonekana kwa macho, husababisha maumivu miguuni hasa katika kisigino.

Tatizo lingine ni madhara ya mishipa ya fahamu kubanwa kitabibu huitwa Morton’s Neuroma ambalo huwa na dalili kama hisia za ganzi, vitu kuchomachoma na kuwaka moto miguuni.

Matatizo mengine ni kupata michubuko katika ngozi ya miguu, kuhisi uchovu katika misuli ya miguu na kuhisi uzito katika maungio ya kifundo na vidole.

Ukiacha matatizo ya kiafya, viatu vya kubana vinaweza kukusababishia kushindwa kufanya zoezi la ukimbiaji kwa usahihi na ufanisi hivyo kutotimiza lengo la zoezi.

Viatu vinapobana mguuni kunamfanya mkimbiaji kupata maumivu hivyo kuyafanya mazoezi hayo kuwa si burudani tena hatimaye kushusha hamasa yako ya mazoezi.

Ushauri, tumia viatu kuendana na saizi yako hali vyenye kupwaya kiasi na kuvutika visivyo vyembamba wala kuwa vifupi na vilivyotengenezwa kwa ngozi laini, raba au kitamba.

Chunguza kiatu kipya unachonunua kabla yakukitumia, hakikisha sehemu ya mbele ina upana wa kutosha ili usibane dole gumba la mguu na mazingira ya ndani yawe na kanyagio laini.

Kumbuka biashara ya raba za mazoezi imekua kubwa kimataifa katika makampuni makubwa hivyo unapaswa kujua namba sahihi ya kiatu unachovaa kwani kuna tofauti ya namba za raba toka China, Uk na USA.

Akiba haiozi, vizuri kuwa na machanguo kadhaa ya raba kama vile kuwa na jozi 3 ili kuwa wigo mpana wa uchaguzi wa raba ya kukimbilia.

Wengi wanaopata madhara ya viatu vya kubana ni wale ambao wanaagiza nje ya nchi hivyo kupishana na saizi ya raba hio na pia huwa na dhana kuwa ni bora zaidi pasipo kujua kuwa sasa bongo kila raba ya kampuni kubwa inapatikana katika maduka ya michezo.

Fika katika maduka hayo na chagua kitu sahihi kitakochofanya ukimbiaji kuwa na tija kwako hatimaye kufikia malengo ya ukimbiaji mwepesi.

Kumbuka kuwa ni bora zaidi kutumia viatu vikubwa kiasi visivyokupa majeraha kuliko kuvaa viatu vidogo sana vyakubana vitakavyokupa majeraha yatakayokuweka nje ya ukimbiaji ili kuuguza madhara hayo.

Chanzo: Mwanaspoti