Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maddison atemwa England, EURO 2024

James Maddison: Tottenham James Maddison

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo Mshambuliaji James Daniel Maddison wa Tottenham Hotspur ameondolewa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 26 cha Timu ya Taifa ya England ‘The Three Lions’ kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Ulaya ‘UEFA Euro 2024’.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 alitokea benchi kwenye mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Bosnia & Herzegovina wa ushindi wa mabao 3-0, na amekuwa mchezaji wa kwanza kati ya saba waliokatwa kwenye uteuzi wa awali wa wachezaji 33 wa Kocha Gareth Southgate.

Kwenye fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022, Maddison aliachwa dakika za mwisho na baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu atazikosa pia fainali hizo za Ulaya na atalazimika kusubiri fainali nyingine za Kombe la Dunia 2026.

Hata hivyo, Kocha Southgate ana muda hadi saa 11 jioni kesho Ijumaa kuwasilisha kikosi chake cha mwisho, kabla ya kutangazwa rasmi Jumamosi (Siku moja baada ya mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya Iceland kwenye Uwanja wa Wembley).

Maddison aliondoka Leicester City na kujiunga na Spurs kwa uhamisho wa Pauni 40 milioni Julai mwaka jana, lakini jeraha la kifundo cha mguu lilizuia kuonyesha makali yake akiwa na miamba hiyo ya Kaskazini mwa London.

Wakati huo huo, mapema leo Alhamisi ripoti zimeeleza Curtis Jones na Jarell Quansah pia wanatarajiwa kukosa kushiriki Fainali za Euro 2024.

Wawili hao wanaoitumikia Liverpool hawatasafiri kwenda Ujerumani, licha ya misimu ya kuvutia huko Anfield katika msimu wa mwisho wa Jurgen Klopp.

Jones alijiimarisha katika safu ya kiungo ya Liverpool, huku Quansah akiimarika vyema katika safu ya ulinzi baada ya kuichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Newcastle United Agosti mwaka jana.

Kuachwa kwa Jones na Quansah kunatoa matumaini mapya kwa Adam Wharton kuingia kwenye kikosi cha mwisho, baada ya kiungo huyo wa Crystal Palace kuichezea timu yake ya taifa ya England katika ushindi wa Jumatatu dhidi ya Bosnia.

England itaanza kampeni za Euro 2024 dhidi ya Serbia Juni 16, kabla ya mechi nyingine za hatua ya makundi dhidi ya Denmark na Slovenia mnamo Juni 20 na Juni 25 mtawalia.

Southgate atakuwa na kibarua cha kuiongoza Three Lions kutwaa ubingwa wa Euro 2024 kwa mara ya kwanza, baada ya kushindwa kwa mikwaju ya penalti na Italia katika Fainali ya Euro 2020.

Chanzo: Mwanaspoti