Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Machungu ya kupigwa mnayo nyie, hawa jamaa hayawahusu

R1227357 1296x729 16 9 Machungu ya kupigwa mnayo nyie, hawa jamaa hayawahusu

Tue, 3 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Arsenal ya msimu wa 2003-04 na Juventus ya 2011-12, ndizo klabu pekee kwenye Ligi Kuu kubwa za Ulaya, ambazo ziliandika historia ya kucheza msimu mzima bila kupoteza.

Kibabe sana. Na katika miaka ya karibuni, zimeshuhudiwa klabu kama Barcelona, Real Madrid, Manchester City, Liverpool na Bayern Munich zikiweka rekodi ya kuvuna pointi nyingi ndani ya msimu mmoja, lakini kucheza bila ya kupoteza mechi hata moja, hiyo si rekodi inayoweza kufikiwa kirahisi.

Siku chache zilizopita kulishuhudiwa timu za Liverpool, Man City na Inter Milan zikichapwa na kuondoka kwenye kundi la timu ambazo zingeweza kuweka rekodi ya kutopoteza mechi yoyote msimu huu.

Na hilo limeibua swali, je, kutakuwa na timu yoyote kwenye Ligi Kuu kubwa za Ulaya itacheza msimu wote wa 2023-24 bila kupoteza? Hadi sasa kuna timu nane tu, ambazo bado hazijaonja machungu ya kupoteza mechi tangu msimu huu ulipoanza.

Arsenal

Chama la Kocha Mikel Arteta, Arsenal limejipanga vyema kabisa kuhakikisha linafanya kitu kwenye Ligi Kuu England msimu huu baada ya kushindwa kidogo tu kunyakua ubingwa msimu uliopita. Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, tayari imeshacheza mechi saba, ikishinda tano na kutoka sare mbili, dhidi ya Fulham na Tottenham. Kocha Arteta amekuwa na mipango matata, lakini kikosi chake kinakabiliwa na mtihani mzito wikiendi ijayo ili kutambua kama kitabaki na rekodi yake ya kutopoteza au la, wakati itakapokabiliana na Man City.

Tottenham

Tottenham Hotspur imekuwa timu inayovutia sana kuitazama kwa sasa. Kwenye Ligi Kuu England msimu huu katika mechi saba ilizocheza, imevuna pointi 17 katika pointi 21. Spurs haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi hadi sasa, huku ikiwa imeshacheza na Manchester United, Arsenal na Liverpool. Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kwa sasa inashika nafasi ya pili na bila shaka inaweza kukaa kileleni endapo kama itashinda mchezo wake ujao kisha Man City na Arsenal zikatoka sare kwenye mechi yao ijayo watakapomenyana.

Barcelona

Mabingwa watetezi wa La Liga nusura wapoteze rekodi yao ya kutopoteza mechi kwenye ligi msimu huu baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili hadi kufikia dakika ya 80 kwenye mechi dhidi ya Celta Vigo inayonolewa na Kocha Rafael Benitez. Lakini, Joao Cancelo na Joao Felix wakawasha moto kwa kutengenezea straika Robert Lewandowski mabao mawili ya haraka, kabla ya Cancelo kufunga bao la ushindi na kuifanya Barca kushinda mchezo huo kwa mabao 3-2. Wenzao Real Madrid walipoteza rekodi yao kwa kuchapwa 3-1 na Atletico.

Bayern Munich

Bayern Munich haijapoteza mchezo wowote wa Bundesliga kwa msimu huu. Na straika wake mpya, Harry Kane ameanza kibabe kabisa maisha yake huko Ujerumani, akiwa amechangia mabao matano, akifunga mara tatu na kuasisti mara mbili katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Bochum. Wikiendi iliyopita, Bayern ilijiweka kwenye hatari ya kutibuliwa rekodi yao baada ya kuchapwa 2-0 na RB Leipzig hadi mapumziko. Lakini, mkwaju wa penalti wa Kane na bao la Leroy Sane liliiokoa na kupata sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo na kunusurika kichapo.

Bayer Leverkusen

Borussia Dortmund ilishindwa kidogo sana kuibwaga Bayern Munich kwenye mbio za ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita. Msimu huu, Bayern Munich inaweza kupata upinzani mkali kutoka kwa Bayer Leverkusen ya Kocha Xabi Alonso, ambaye anaonekana kuwa siriazi kwenye mikikimikiki hiyo, ambapo timu yake haijapoteza mchezo wowote hadi sasa. Alonso anatengeneza jina lake na kuwa mmoja wa makocha mahiri Ulaya, huku timu yake ikiwa na straika matata, Mnigeria Victor Boniface – ambaye anatisha kama Victor Osimhen.

Borussia Dortmund

Kwenye Bundesliga, miamba mingine ambayo haijapoteza mechi yoyote hadi sasa ni Borussia Dortmund. Haikucheza vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuchapwa na Paris Saint-Germain – lakini kwenye Bundesliga iliangusha pointi pia dhidi ya timu ndogo kama Bochum na Heidenheim. Pamoja na mwendo wao wa kusuasua, baso timu hiyo haijapoteza mchezo wowote kwenye Bundesliga na ilishinda dhidi ya timu ngumu Freiburg, Wolfsburg na Hoffenheim. Kwa sasa inaringana pointi na Bayern Munich, licha ya kumpoteza Jude Bellingham.

Nice

Miamba AS Monaco na mabingwa Paris Saint-Germain wote wanasubiri mbele ya Nice kwenye Ligue 1 msimu huu. Klabu hiyo inayomilikiwa na bilionea Sir Jim Ratcliffe ilipoteza mastaa wake kadhaa akiwamo Kasper Schmeichel, Aaron Ramsey, Ross Barkley na Nicolas Pepe kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Nice ipo kwenye nafasi ya nne kwenye Ligue 1 baada ya kushinda mechi tatu na kutoka sare mara nne, huku kocha wao ni kijana kabisa, Francesco Farioli ana umri wa miaka 34 tu. Anavutia kumtazama.

Rennes

Rennes wanaitwa ni wataalamu wa sare kwenye Ligue 1. Miamba hiyo inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi hiyo, katika mechi saba walizocheza, wameshinda mbili na kutoka sare mara tano. Walianza msimu kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Metz, lakini baada ya hapo wamejikuta wakibanwa na kutoka sare mfululizo dhidi ya Lens, Le Havre, Brest, Lille na Montpellier. Waliachana na gundu la sare kwa staili ya kibabe, wakishinda 3-1 dhidi ya Nantes na hivyo kuwamo kwenye orodha ya timu ambazo hazijapoteza msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti