Imefahamika kuwa Yanga imetumia kitita cha milioni Sh 350 kumrejesha winga wake Mkongomani, Tuisila Kisinda kutokea RS Berkane ya Morocco ambapo alikuwa akicheza.
Yanga imempa mkataba wa miaka miwili winga huyo raia wa DR Congo kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo katika msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo tumezipata, kutoka kwa mmoja wa mabosi wa timu hiyo kiungo huyo amekubali kurejea kukipiga Yanga mara baada ya kumuwekea dau hilo la fedha lililomshawishi kusaini mkataba.
Bosi huyo alisema kuwa tofauti na dau hilo, kingine kilichomrudisha ni mapenzi aliyonayo kabla ya kuuzwa Berkane akiwa na timu hiyo.
Aliongeza kuwa Rais wa timu hiyo, Injinia Hersi Said naye amehusika kumshawishi winga huyo kurejea Yanga kutokana na ukaribu uliopo baina yao.
“Kisinda alikuwa na ofa nyingi mara baada ya baadhi ya klabu kubwa kumfuata kwa ajili ya kuzungumza naye na kumsajili.
“Kisinda alikataa ofa zote na kuchukua maamuzi ya kuja kuichezea Yanga kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja.
“Hersi alihusika kwa kiasi kikubwa kufanikisha usajili wake ambaye akiwa Berkane alikuwa akiwasiliana naye na kushauriana mambo mengi,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa Hersi kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Usajili ni siri kati ya mchezaji na uongozi, hivyo ngumu kuweka wazi maslahi ya mchezaji na timu.”