Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabosi Singida FG watajwa kung'atuka kwa Kocha Ernst Middendorp

Kocha Mpya Singida Mabosi Singida FG watajwa kung'atuka kwa Kocha Ernst Middendorp

Wed, 20 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Akiwa ameiongoza Singida Big Stars kwenye mchezo mmoja tu, kocha Ernst Middendorp jana amejiuzulu kuifundisha timu hiyo ya mkoani Singida akidai kutokuwa tayari kuingiliwa katika majukumu yake na uongozi.

Katika barua iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambayo inaripotiwa imeandikwa na kocha huyo raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 54, Middendorp amedai kuwa baada ya mchezo wa kwanza nyumbani wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Future FC ya Misri ambao Singida Big Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0, uongozi wa timu hiyo ulionekana kutofurahishwa na matokeo hayo huku ukimpa masharti ambayo yeye hajakubaliana nayo na kuamua kuachana nao.

"Mamlaka za Singida Fountain Gate zilipanga kikao cha haraka siku iliyofuata kikihusisha timu nzima ya ufundi pasipo kuelezea sababu za kikao. Tulitegemea kutakuwa na neno la pongezi lakini hiyo haikuwa jambo lenyewe. Lengo la kikao lilikuwa wazi kuwa kuelezea kutoridhishwa, maoni yangu hayakusikilizwa na majadiliano hayakuzaa matunda," alifafanua Middendorp katika barua yake hiyo.

Kocha huyo alieleza kuwa katika kikao hicho, uongozi wa Singida ulikuwa na hoja saba ambazo yeye alishanhazwa nazo na kuona vyema achukue uamuzi wa kung'atuka.

Hoja hizo ni kutoridhishwa na ushindi wa bao 1-0 ambapo uongozi ulitegemea ushindi mkubwa zaidi ya huo, timu kutoonyesha kiwango kizuri, kutokubaliana na uamuzi wa kutowapanga baahdi ya wachezaji, mkurugenzi wa ufundi na meneja wa timu kuamriwa waanze kumshauri kocha, kumlazimisha awapange baadhi ya wachezaji na kumuamrisha asiwapange baahdhi na mwisho ni kurudishwa kwa aliyekuwa kocha msaidizi (Mathias Lule) ili ashirikiane naye.

"Sikujaribu kubadili mawazo ya mamlaka na hivyo nikaamua kuondoka ili kuacha uhusiano wangu na Singida Fountain Gate. Safari ya kurudi nyumbani Johannesburg imechukua muda wa saa 20," alisisitiza Midderndop.

Dalili za Midderndop kuwa kikaangoni zilianza kujionyesha tangu Jumapili baada ya mchezo dhidi ya Future ambapo vigogo wengi wa timu hiyo walionekana kusimama vikundi vikundi huku wakionyesha kutoridhishwa na namna timu hiyo ilivyocheza licha ya kuibuka na ushindi huo.

Juzi jioni ikiwa ni siku moja tu tangu kumalizika kwa mchezo huo ambao kikosi cha Singida kilikuwa na mabadiliko makubwa, taarifa zilizagaa kuwa Middendorp ameshindwana na uongozi na kuondoka zake.

Jana gazeti la Mwananchi lilihudhuria mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi Azam dhidi ya Azam FC, kesho Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru na kushuhudia yakisimamiwa na Mkurugenzi wa ufundi, Ramadhan Nswazurwimo h pasipo uwepo wa Middendorp.

Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Olebile Sikwane alikiri kuondoka licha ya kwamba hawakufikia makubaliano ya mwisho.

"Kweli hayupo hapa kama nyie mnavyoona lakini tutaendelea kuzungumza nae kuona namna ambavyo atarejea kwenye kikosi chetu kuendelea na kazi yake, ana siku chache tu tangu ajiunge na sisi.

"Singida ni timu kubwa na hakuna ambaye yupo juu yake kwa hiyo tunamuheshimu kocha Ernst kwa sababu ana uzoefu mkubwa Ujerumani, Afrika Kusini hivyo siwezi kuzungumza lolote zaidi, kuna muda kuna kupishana kwenye bodi hata mimi inatokea hivyo ni vitu vya kawaida," alisema Sikwane.

Sikwane alifunguka zaidi na kusema kutokana na ratiba ngumu waliyonayo wameamua kumchukua aliyekuwa Mkurugenzi wa ufundi katika timu hiyo Ramadhan Nsanzurwimo kwa ajili ya kuitengeneza timu katika mechi zijazo.

"Nsanzurwimo atakuwa kocha mkuu kwa sasa akisaidiana na Lule (Mathias) kwa sababu tuna mechi kubwa dhidi ya Azam, Future na Simba, hawa tutaenda nao hadi tutakapopata kocha mkuu mpya kama tutashindwa na Ernst,"alisema Sikwane.

Singida BS inajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaochezwa Alhamis saa 1:00 usiku katika uwanja wa Azam Complex.

Middendorp alijiunga na Singida Big Stars, wiki mbili zilizopita akichukua nafasi ya Hans Pluijm ambaye alijiweka kando.

Chanzo: Mwanaspoti