Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabosi Ligi Kuu England wanawaza kombe liende wapi

EPL Trophy Zz Mabosi Ligi Kuu England wanawaza kombe liende wapi

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mabosi wa Ligi Kuu England wanakuna vichwa kwa sasa juu ya kuweka mipango sawa itakavyokuwa siku ya mwisho ya msimu wa ligi hiyo na vita iliyopo kwenye mbio za ubingwa.

Kinachowaumiza vichwa ni kuhusu kombe lipelekwe wapi endapo kama timu tatu, Arsenal, Liverpool na Manchester City zitakwenda jino kwa jino kwenye mbio za ubingwa hadi siku ya mwisho ya msimu.

Mara tisa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England tangu ilipoanza mwaka 1992, timu mbili ndio zimekuwa zikichuana hadi siku ya mwisho ya msimu, huku Liverpool na Man City zilifanya hivyo miaka miwili iliyopita.

Na kinachoonekana msimu huu kinakwenda kutokea tena na Jumapili, Mei, 19 siku ya mwisho ya msimu, Man City, Arsenal au Liverpool zote zina nafasi ya kunyakua ubingwa. Kinachovutia zaidi, timu hizo zote zitakuwa nyumbani na Arsenal itakipiga na Everton uwanjani Emirates, Liverpool na Wolves kwenye Uwanja wa Anfield na huko Etihad, Man City itakaribisha West Ham United. Kwa sasa kuna makombe mawili yanayofanana. Taji Namba Moja lipo kwa bingwa mtetezi hadi wiki tatu za mwisho kabla ya msimu kumalizika. Taji la pili la Ligi Kuu England ni lile ambalo limekuwa likitembezwa sehemu mbalimbali za dunia kwenye matukio ya udhamini.

Makombe yapo mawili na sehemu zinazotakiwa kuwaniwa ni tatu. Lakini, sasa kuna kombe moja, ambalo lipo kwenye studio za uzalishaji za Ligi Kuu England, zilizopo huko Stockley Park, Uxbridge — ambako ndiko kwenye chumba cha mitambo ya VAR, linaloweza kutumika kuwekwa sehemu moja kati ya hizo tatu kama ushindani wa kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England utafika mwisho wa msimu.

Timu yoyote itakayonyakua ubingwa siku hiyo, itakapokabidhiwa kombe, italazimika kulirudisha baada ya wiki mbili ili likafanyiwe usafi na wataalamu maalumu. Inakuwa hivyo, kwa sababu kwenye siku ile ya sherehe ya kushangilia ubingwa, linakuwa limeshikwashikwa sana, hivyo linahitajika kusafishwa liendelee kubaki kwenye ubora na mvuto wake.

Chanzo: Mwanaspoti