Mabosi wa Al Hilal ya Sudan iliyoweka maskani ya muda nchini, wanadaiwa kuvutiwa na kiwango bora kilichoonyeshwa na nahodha wa KMC, Awesu Awesu wakati timu hizo zilipokutana katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Shule ya Baobab na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Katika mchezo huo uliopigwa Alhamisi iliyopita, Awesu ndiye aliyefunga bao la KMC na kuwateka mabosi hao wa Sudan, huku Mwanaspoti likipenyezewa taarifa kwamba huenda biashara baina ya klabu hizo ikafanyika endapo tu zitakubaliana.
“Ni kweli viongozi wa Al Hilal walitufuata baada ya mchezo ule kumalizika na kumuulizia mchezaji wetu, lakini hatujafikia makubaliano yoyote ingawa wameonyesha nia ya kumhitaji, hivyo kuhusu dili hilo bado, tusubiri,” kilisema chanzo chetu kutoka KMC.
Kocha wa KMC, Abdihamid Moallin alipotafutwa nasi kuhusu suala hilo alisema anachojua ni kwamba viongozi wa Al Hilal walisifu tu uwezo ulioonyeshwa na nyota huyo ingawa mambo mengine yaliyoendelea baada ya hapo hayatambui.
“Sio yeye peke yake aliyeonyesha kiwango kizuri kwa sababu wapo wengi tu ambao nao walisifiwa. Siri kubwa ni kutokana na kundi kubwa la wachezaji waliopo (KMC)ni vijana wanaojituma, hivyo hicho ndicho ninachokijua na wala si vinginevyo,” alisema.
Moallin aliongeza kuwa mchezo huo na Al Hilal ulikuwa kipimo kizuri kwao kwa ajili ya maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, Novemba 22, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kuanzia saa 1:00 usiku.