Klabu ya Young Africans huenda ikacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC kwenye kilele Cha Wiki ya Wananchi.
Jana Jumanne (Julai 19) Young Africans kupitia Idara ya Habari na Mawasilino ilitangaza Agosti 06 kuwa siku ya kilele cha Wiki ya Wananchi, ambapo itafanya Tamasha maalum Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Taarifa zinaeleza kuwa Young Africans ambayo inaanza rasmi Kambi ya maandalizi ya msimu mpya jana Jumatano (Julai 20), huenda ikacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki siku hiyo (Agosti 06) dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC.
Hata hivyo bado Uongozi wa Young Africans haijathibitisha taarifa hizo, na umeendelea kuwahimiza Mashabiki na Wanachama wake kuendelea kusubiri taarifa rasmi kuhusu mchezo wa kirafiki utakaorindima Siku ya Wananchi.
Katika kilele cha Wananchi mwaka 2021, Young Africans iliialika Zanaco FC kutoka Zambia, na ilikubali kupoteza kwa 2-1.
Young Africans imedhamiria kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, huku ikiwa na kazi nzito ya kuwakilisha nchi kwenye Michuano ya Kimataifa (Ligi Mabingwa Barani Afrika).