Safu za ulinzi za Simba na Ihefu zina kazi ngumu ya kuzibabe timu zao wakati zitakapokutana leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku kutokana na mwenendo usioridhisha wa kila upande katika kulinda nyavu zao.
Timu hizo kila moja inakaribia kuwa na wastani wa kuruhusu angalau bao moja kwa mchezo katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo katika mechi tano ilizocheza, Simba imeruhusu idadi ya mabao manne wakati Ihefu yenyewe katika michezo yake sita ya mwanzo, nyavu zake zimetikiswa mara tano.
Presha kubwa hapana shaka ipo kwa wageni Ihefu kwani wamekuwa na udhaifu mkubwa katika safu yao ya ushambuliaji ambayo imeonyesha ubutu ikifunga mabao matatu tu katika mechi sita, tofauti na Simba ambayo ni moto wa kuotea mbali katika kufumania nyavu ambapo hadi sasa imefunga mabao 14 huku ikiwa imecheza mechi pungufu.
Simba itaingia katika mchezo huo ikijivunia kuwa timu pekee kati ya 16 za Ligi Kuu ambayo haijapoteza mchezo wala kutoka sare hadi sasa ikiwa imeshinda zote tano ilizocheza, lakini Ihefu pia itaingia kwa kutamba kuwa timu pekee iliyoimfunga Bingwa Mtetezi wa ligi (Yanga),ikimchapa 2-1 katika mechi ya mzunguko wa tatu wa ligi.
Aidha mchezo huo utanogeshwa na rekodi za msimu huu, ambapo Simba katika mashindano matatu tofautiĀ iliyoshiriki, haijapoteza mechi hata moja huku ikiwa imekutana na vigogo kama Al Ahly ya Misri, Yanga na Power Dynamos ya Zambia.
Kwa upande wa Ihefu rekodi hizo haziibebi kwani msimu huu imecheza mechi sita ambazo zote ni za Ligi Kuu na kuambulia ushindi mara mbili tu, sare moja na kupokea kichapo mara tatu.
Hata hivyo Ihefu bado rekodi zake inapokutana na Simba sio nzuri kwani katika misimu miwili Walima Mpunga hao wa Mabarali walipokutana na Wekundu wa Msimbazi, Simba imeshinda mechi zote tano, ikifunga jumla ya mabao 14, huku Ihefu ikitoka kapa na mabao mawili tu ya kufunga.
Kocha mkuu wa Simba, Robertinho alisema kutakuwa na mabadiliko ya kimbinu na wachezaji kwenye mechi na Ihefu lakini lengo kuu ni kupata ushindi ili kusogea kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa huo.
"Tumecheza mechi mbili ngumu dhidi ya Al Alhly, ndani ya muda mchache, tulifanya vizuri lakini kwa bahati mbaya tukashindwa kusonga mbele kwa sababu ya kanuni, huko tumetoka na sasa tunajipanga na mechi zijazo.
Tutakuwa na mabadiliko ya mbinu na hata wachezaji lakini lengo letu kuu ni kuhakikisha tunashinda mechi hiyo ili kutengeneza mazingira bora ya kuwa bingwa," alisema Robertinho.
Kwa upande wa Basena wa Ihefu alisema; "Simba ni timu ngumu na imekuwa na muendelezo mzuri, tunaiheshimu kwa hilo lakini tumejiandaa kufanya vizuri pia.
Zitakuwa dakika 90 nzuri na ngumu, tunasubiri muda ufike tukapambane kupata kile tunachokitaka," alisema Basena.
Mastaa wa Simba ambao hawapati muda mwingi wa kucheza kikosini hapo wakiwemo, Moses Phiri na Luis Miquissone huenda wakaanza kwenye mechi ya leo huku kwa Ihefu mastaa wake wote wakiwemo Victor Akpan, Never Tigere na Juma Nyosso wakitarajiwa kuwepo.