Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabao matamu ya msimu huu

Pape Ousmane Sakho Shoot Mabao matamu ya msimu huu

Sat, 10 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Straika wa Yanga, Fiston Mayele ametoa somo kwa wazawa msimu wa pili mfululizo Ligi Kuu Bara juu ya namna ya kufunga na sasa anatazamwa kuwa miongoni mwa washambuliaji bora wa kigeni kuwahi kutokea kwenye soka la Tanzania.

Msimu uliopita Mayele (16) alizidiwa kete padogo na George Mpole (17) ambaye aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, lakini ni kama aliendelea pale ambapo aliishia kitu ambacho wachezaji wengi wazawa wamekuwa wakichemka.

Ikiwa imesalia michezo michache kabla ya msimu kumalizika Mayele tayari alikuwa amefikia idadi ya mabao 16 ambayo alipachika msimu uliopita, ni kati ya washambuliaji wachache mno wenye mabao mengi ndani ya kipindi kifupi.

Tuhame huko msimu huu wa 2022/23 tumeshuhudia mabao mengi yakifungwa kwenye viwanja mbalimbali lakini haya (10) yalikuwa kiboko.

10. PETERSON CRUZ VS PRISONS

Agosti 16, 2022 kwenye uwanja wa Liti Singida ambapo Singida Big Star ikiwa mwenyeji lilifungwa bao la kideo na Mbrazil Peterson Cruz kwenye mchezo wa kwanza wa msimu kwa vijana hao wa Hans van der Pluijm ambao ulikuwa dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons.

Bao hilo liliifanya Singida BS kuanza vizuri msimu, ilikuwa ni baada ya kazi nzuri ya Shafik Batambuze ambaye alikuwa winga ya kulia, alimdanganya mchezaji wa Tanzania Prisons na kupiga krosi ambayo ilimkuta Amissi Tambwe ambaye naye alitoa pasi kwa Cruz aliyemalizia kwa kujibetua 'tikitaka'.

9. BRUNO GOMES VS KAGERA SUGAR

Hakuna ubishi kuwa ni fundi wa kupiga mipira ya adhabu lakini hili lilikuwa ni bao la kawaida na lilikuwa la pili kwake kwenye mchezo huo, uliukokota mpira kwa umbali mrefu kabla ya kupiga shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Kagera Sugar, Said Kipao ilikuwa Oktoba 21 mwaka jana ambapo Singida BS ambayo ilikuwa ugenini iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

8. HAMAD MAJIMENGI VS AZAM FC

Lilikuwa bao la pili la kusawazisha kwa Coastal Union ya Tanga, Novemba 27, 2022 kwenye uwanja wa Azam Complex dhidi ya wenyeji wao, Azam FC, Hamad Majimengi alitandikwa mkwaju wa mbali ambao ulimshinda Ali Ahamada. Hata hivyo mchezo huo ulimalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

7. SHAABAN DJUMA VS MTIBWA SUGAR

Kipa aliyekuwa akiidakia Mtibwa Sugar, Faruk Shikhalo aliteseka Septemba 13, 2022 kwani baada ya kupanga vizuri ukuta wake, alishangaa upande ule ule beki wa Yanga, Shaaban Djuma akipitisha mpira ambao ulimshinda, ilikuwa moja ya faulo kali kupigwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara kwa kuzingatia umbali.

6. AZIZI KI VS SIMBA

Oktoba 23, 2022 kwenye mchezo wa watani wa Jadi ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, alishuhudiwa Stephane Azizi Ki akiisawazishia Yanga kwa mpira wa adhabu. Umbali, ustadi wa mpigaji na kasi ya mpira ni vitu ambavyo viligogesha bao hilo ambalo aliruhusu Aishi Manula licha ya kupanga vizuri ukuta wake.

5. MOSES PHIRI VS KMC

Pamoja na kwamba hakuwa na wakati mzuri kwenye michezo ya mwishoni mwa msimu, mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri ni kati ya washambuliaji hatari ni vile tu majeraha yalimrudisha hatua kadhaa nyuma na wakati anarejea alimkuta Jean Baleke gari likiwa limewaka hivyo ilikuwa ngumu kwake kumzidi kete.

Phiri aliwafanya kitu kibaya mabeki wa KMC, Desemba 7 mwaka jana kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa kabla ya kuifungia Simba bao la kwanza kwenye mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2. Ilikuwa ni dakika ya pili tu mchezo akiwa na mabeki watatu aliwapunguza na kuachia mkwaju ambao ulitinga moja kwa moja kwenye nyavu za wakusanya mapato hao lilikuwa bao lake la tatu la msimu.

4. FISTON MAYELE VS MTIBWA SUGAR

Miongoni mwa mabao ya fedheha ambayo Mtibwa Sugar iliruhusu msimu uliopita ni pamoja na hili, ambalo lilifungwa Septemba 13, 2022 kwenye uwanja wa Mkapa na Mayele ambaye aliukokota mpira kutoka karibu na katikati mwa uwanja baada ya kupokea pasi ya Farid Mussa, akawazidi uanja mabeki watatu na kufunga bao la pili kwa Yanga kwenye mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

3. GEORGE MAKANG'A VS SIMBA

Almanusra alizamishe jahazi la Simba, Desemba 7 mwaka jana baada ya kuifungia KMC bao la pili ambalo lilizua gumzo kwenye mchezo huo kwani hakuna ambaye alidhani anaweza kuuzungusha mpira ule kutokana na eneo ambao alikuwa pamoja na msitu wa mabeki ambao ulikuwa mbele yake.

Makang'a alipiga mzungusho na kumfanya kipa wa Simba, Aishi Manula kushindwa kuucheza mpira ule ambao moja kwa moja ulitinga kwenye nyavu. Lakini pia nyota huyo wa KMC aliifunga pia Azam FC, Oktoba 21 mwaka jana bao la kideo.

2. AZIZI KI VS KAGERA SUGAR

Licha ya kwamba amekuwa na panda shuka nyingi za kiwango chake msimu huu, moja ya mchezo ambao alikuwa kwenye ubora wake ni pamoja na ule dhidi ya Kagera Sugar, Aprili 11 mwaka huu kwenye uwanja wa Azam Complex ambapo aliweka kambani mabao matatu, ilikuwa hat-trick yake ya kwanza akiwa na jezi ya Wananchi.

Achana na bao la kwanza la mchezo huo ambalo alifunga kwa mkwaju wa penalti, nyota huyo wa zamani wa ASEC Mimosas, bao lake la pili ndilo lililozua gumzo, kwani sekunde chache baada ya kupokea mpira ambao ulikuwa ukidunda alimchungulia kipa wa Kagera, Said Kipao na kugundua alisogea kidogo, ndipo alipoachia mkwaju ambao ulitinga moja kwa moja kwenye nyavu.

Lakini pia kwenye mchezo huo lilishuhudia bao lingine kali kutoka kwa Bernard Morrison ambaye aliuzungusha mpira akitokea winga ya kushoto na kuifanya Yanga kupata bao la nne kwenye mchezo huo ambao Wananchi waliibuka na ushindi wa mabao 5-0, huo ulikuwa miongoni mwa ushindi mkubwa kwao kwenye ligi.

1. PAPE SAKHO VS MBEYA CITY

Kama mabao ya kideo basi, Pape Sakho ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo wa kuyafunga,ikumbukwe kuwa aliwahi kuchukua tuzo mwaka jana, 2022 kwenye michuano ya kimataifa kwa kupachika bao bora la msimu, hii nayo ilikuwa kiboko dhidi ya Mbeya City kwenye mchezo ambao Mnyama aliibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Wakati Simba ikisaka bao la tatu dakika ya 55, mabeki wa Mbeya City waliuna mpira na kujaribu kuondoka hatari hiyo lakini Richardson Ng'ondya ambaye alishuka kusaidia alifanya makosa na mpira kunaswa na Sakho ambaye aliachia mkwaju mkali ambao ulimshinda, Lameck Kanyonga ambaye alikuwa golini.

Lakini pia kwenye mchezo huo, ambao ulichezwa Februari 18 mwaka huu alishuhidiwa Saidi Ntibazonkiza naye akifunga bao la kideo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: