Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabao bora 10 ya msimu 2020/21 VPL

Mabao Pic Data Mabao bora 10 ya msimu 2020/21 VPL

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MSIMU wa Ligi Kuu Bara umemalizika leo na tayari tumeshamshuhudia bingwa akiwa Simba ambaye ameendelea kuchukua taji la nne mfululizo.

Simba wamekuwa na ubora wa juu uwanjani na walistahili ubingwa huo kutokana na aina ya soka wanalopiga na pia ubora wa kikosi chao.

Hebu tuyaangazie mabao 10 yaliyotikisa msimu huu yakipigiwa chapuo kuwa kati ya mabao bora ya msimu huu.

1. Bernard Morrison (Namungo vs Simba 1-3)

Hili linaweza kuwa bao bora la msimu. Ilikuwa ni dakika ya 88 na Simba ilikuwa ikiongoza 2-1 ugenini dhidi ya Namungo wakati Morrison alipopokea pasi ya Hassan Dilunga akiwa mbele kidogo ya duara la katikati ya Uwanja wa Majaliwa.

Morrison alichofanya ni kumchungulia kipa Jonathan Nahimana aliyekuwa amevutika mbele kidogo, akapiga shuti la juu la kiufundi sana lililokwenda moja kwa moja wavuni mpira ukipitia pale anapotagia ndege. Nahimana aliruka na kujinyoosha kwa uwezo wake wote, lakini vipimo vilimzidi.

2. Prince Dube (Azam vs KMC 3-2)

Ilikuwa dakika ya 65 wakati mshambuliaji wa Azam, Prince Dube alipopokea pasi ndefu ya kiungo Mudathir Yahaya, akakimbia kushoto mwa uwanja na kumzidi ujanja Andrew Vincent aliyeachwa akilamba sakafu.

Dube akageukia ndani na kulielekea lango vyema, akapiga shuti la ndizi matata kabisa mpira ukaenda kutinga kwenye nyavu ndogo kushoto kwa kipa mkongwe Juma Kaseja.

3. Mohamed Hussein (Gwambina vs Simba 0-1)

Hili lilikuwa bao pekee la ushindi kwa Simba ambapo beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliifungia timu yake baada ya kuuwahi mpira wa makosa kutoka kwa kiungo wa Gwambina, bila ya kuremba aliachia kali kutokea nje ya boksi na mpira kujaa moja kwa moja wavuni akimuacha kipa wa Gwambina, Mohamed Makaka akiruka bila mafanikio.

4. Lambert Subiyanka (Prisons vs Mwadui 2-0)

Hili nalo ni moja ya mabao ya kikatili sana likifungwa na mshambuliaji Lambert Subiyanka. Alipokea pasi ya mshambuliaji mwenzake Jeremia Juma katika dakika ya 22, akaumiliki mpira mbele ya beki Joram Mgeveke na baada ya kugeuka tu akiwa nje sana ya eneo la hatari akaachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni kwa juu.

5.Aniceth Revocatus (Yanga vs Mwadui 3-2)

Mshambuliaji wa Mwadui Aniceth Revocatus aliwafunga Yanga mabao mawili katika mchezo huu lakini bao la pili ndio lilikuwa la hatari zaidi.

Yanga walikuwa wanamiliki mpira kisha wakaupoteza na Mwadui kuanza haraka mashambulizi. Alichofanya Revocatus aliwakimbiza viungo wa Yanga kisha kufanikiwa kumweka chini beki Paul Godfrey na baaadaye kiungo Feisal Salum kushindwa kumsumbua akavuta kidogo akiwa mbali na eneo la hatari akaachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni pembeni kidogo juu na kumuacha kipa Farouk Shikhalo akiwalaumu mabeki.

6. Luis Miquissone (JKT Tanzania vs Simba 0-4)

Hili ni kati ya mabao matamu sana lililofungwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma wakati Simba wakishinda kibabe kwa mabao 4-0.

Bao hilo lilifungwa na winga wa Simba, Luis Miquissone katika dakika ya 54 ambapo wakati Simba wakilishambulia lango la JKT shuti la mshambuliaji Meddie Kagere linamgonga beki wa wanajeshi hao kisha Miquissone kuunasa mpira akautuliza kidogo na kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja pembeni juu kulia kwa kipa Patrick Muntari.

7. Rashid Juma (Namungo vs Polisi 0-1)

Kiungo wa zamani wa Polisi ambaye anaichezea timu hiyo kwa mkopo anastahili kuwa katika orodha ya mabao bora kupitia bao lake dhidi ya Namungo pale Uwanja wa Majaliwa.

Ilikuwa dakika ya 76 wakati Juma alipopokea pasi safi ya Jimmy Shoji na kabla ya kufunga akavuta kwa hatua moja mbali kabisa na eneo la hatari na kuachia shuti kali la mguu wake wa kulia, kipa Nurdin Balora alichoweza kuona ni nyavu zake zikitingishika huku Polisi wakishangilia.

8. Adam Adam (Namungo vs JKT 2-2)

Mshambuliaji wa zamani JKT Tanzania Adam Adam naye hakosekani katika orodha hii na kwenye mchezo huu alifunga bao lake moja kali dakika ya 5 tu ya mchezo akipokea pasi ya beki wake Michael Aidan.

Alichofanya Adam baada ya kuupokea mpira aliumiliki vizuri akitumia mguu wake wa kushoto na wakati mabeki wa Namungo wakitulia kuangalia atafanya kipi jamaa akaachia shuti kali la mguu huohuo wa kushoto ulionyooka na kufunga bao kali nje kabisa ya eneo la hatari na kumuacha kipa Jonathan Nahimana asijue kilichotokea.

9. Adam Adam (Mwadui vs JKT 1-6)

Wakati JKT Tanzania wanaichapa vibaya Mwadui waliokuwa nyumbani kuna bao kali lilifungwa na Adam Adam tena ilikuwa ni dakika ya 47 ya kipindi cha pili. Alipokea pasi ya kiungo Hafidh Mussa, akamhadaa beki wa Mwadui na akaachia shuti kali la mguu wa kushoto lililoanza kugonga mwamba kisha kujaa wavuni.

10. Clatous Chama (Simba vs Polisi 2-0)

Kwenye mchezo huu kiungo Chama alifunga mabao mawili lakini bao lake bora ni lile la pili akilifunga dakika ya 90. Alipokea pasi safi kutoka katikati ya uwanja, akatulia na kusogea mbele kidogo nje ya eneo la hatari kisha anaukata mpira kiufundi unaokwenda moja kwa moja wavuni juu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz