Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabao 10 bora raundi ya 22 Ligi Kuu ya NBC

Stepahne Aziz KI Ahadi Stephane Aziz Ki.

Tue, 30 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni, kumekuwa na mchuano mkali kwa timu tatu za Yanga, Azam FC na Simba kusaka ubingwa na nafasi mbili za juu kwa ajili ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Mchuano mwingine ni timu zinazotaka nafasi ya tatu na ya nne, ili kujiweka kwenye mazingira ya kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika, huku zingine zikipigana kubaki Ligi Kuu.

Vita nyingine ipo kusaka Kiatu cha Dhahabu ambapo Stephane Aziz Ki mwenye mabao 15 na Feisal Salum aliyepachika mabao 14 mpaka sasa wanaonekana kutoshikika.

Mwisho wa msimu pia kuna tuzo ya bao bora la msimu, ambapo hukusanywa mabao yote yaliyoonekana kufungwa kwa ustadi na kupigiwa kura.

Hapa kuna mabao 10 'makali' yamefungwa raundi ya 22, ambayo yameingizwa kwenye kinyang'anyiro cha kusaka bao kali la msimu. Katika makala haya, tunakuletea mabao hayo, wachezaji waliyoyapachika wavuni na jinsi yalivyofungwa, twende sasa...

10# Bakari Selemani (Coastal vs Mashujaa)

Mpira ulikuwa kwenye wingi ya kushoto kwa Jackson Shiga ambaye alipiga krosi iliyonaswa na Crispin Ngushi, jaribio lake la kutaka kufunga kwa mguu wa kushoto lilishindikana shuti kwani alilopiga lilionekana kutoka nje.

Ghafla, Bakari Selemani alifika eneo sahihi na wakati sahihi na kuukwamisha mpira wavuni dakika ya 57, mchezo uliochezwa, Aprili 12, mwaka huu, katika Uwanja wa Lake Tanganyika. Hilo lilikuwa ni bao la pili na la ushindi kwa Coastal, ilishinda ugenini mabao 2-1.

9# Ibrahim Abraham (Prisons vs KMC)

Ilibaki dakika 10 tu mechi kumalizika, huku Prisons ikiwa nyuma kwa bao 1-0 nyumbani, Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya. Akitokea benchini, beki wa kushoto, Ibrahim Abraham, alipachika bao la kusawazisha na kuiokoa timu yake kupata kipigo nyumbani, mechi ikiisha kwa sare ya bao 1-1.

Ilikuwa ni Aprili 12, mwaka huu, na lilitokana na mpira mrefu wa kurushwa, uliomparaza mchezaji mmoja wa Prisons na kuwapoteza maboya mabeki wa KMC. Mpira ulidunda hatua tatu kutoka langoni, mbele yake kukiwa na mfungaji aliyefumua shuti kali la mguu wa kushoto, ukajaa wavuni.

8# Shadrack Malungwe (Mashujaa vs Coastal)

Ilikuwa ni Aprili 12, mwaka huu, mechi ambayo Mashujaa ilikuwa mwenyeji wa Coastal Union, Uwanja wa Lake Tanganyika, wageni wakishinda mabao 2-1. Shadrack Malungwe wa Coastal Union alifunga moja ya mabao makali katika raundi ya 22 ambalo lilikuwa la kwanza la mchezo huo dakika ya tisa.

Shiga alipiga krosi iliyomkuta mfungaji akiwa mbali kidogo na lango. wakati ikidhaniwa anaweza kuutuliza kwanza, alipiga kichwa na mpira kupinda kama pembeni mwa lango la Mashujaa kabla ya kujaa wavuni.

7# Joseph Guede (Yanga vs Singida)

Moja ya mabao maridadi kufungwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara lilikuwa la Joseph Guede wa Yanga katika mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate. Ilikuwa ni dakika ya 41, ambapo aliupata mpira uliopigwa na Joyce Lomalisa akiwa wingi ya kushoto, alimhadaa mchezaji mmoja wa Singida Fountain Gate na kupiga mpira wa kiufundi kwa kuukata.

Awali, ilionekana kama krosi hivi, lakini mpira ulikatika kwenye engo ya pili ya nguzo na kujaa wavuni, akiipa Yanga bao la kwanza, mechi iliyoisha kwa ushindi wa mabao 3-0.

6# Abdulkarim Mahmoud (KMC vs Prisons)

Mabeki wa Prisons na kipa wao walijichanganya na kumrudishia mpira kipa Yona Amosi, ambaye alikuwa kwenye presha ya wachezaji wa KMC, hivyo aliupiga mpira ambao haukwenda mbali sana. Ukamkuta mfungaji umbali wa mita 30, hakufanya ajizi kwani kipa alikuwa ametoka, akaupiga moja kwa moja, kwa shabaha ya hali ya juu, mpira ukatinga wavuni, dakika ya tisa ya mchezo, akiipatia KMC bao ambalo lilikuja kurudishwa mwishoni, ngoma ikaisha 1-1. Mchezo ulichezwa, Aprili 12, mwka huu Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

5# Jimson Mwanuke (Mtibwa vs Geita Gold)

Mpira uliopigwa na kipa Justin Ndikumana, uliguswa na mchezaji mmoja tu wa Mtibwa Sugar, kabla ya kumkuta, Jimson Mwanuke, anayeichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba.

Aliunchukua mpira huo akiwa pembeni winga ya kushoto, akaingia nao ndani kidogo, nje ya eneo la hatari akaachia kombora kali lililokwenda moja kwa moja wavuni, dakika ya 15 ya mchezo.

Mechi hiyo ilichezwa Aprili 13, mwaka huu katika Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, Mtibwa ilicheza dhidi ya Geita Gold, mechi iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.

4# Omari Omari (Mashujaa vs Coastal)

Omari Omari, aliisawazishia Mashujaa bao dakika ya 45, kwa shuti kali la mbali, kiasi cha mita 35, akitumia mguu wake wa kushoto, katia Uwanja wa Lake Tanganyika Aprili 12, mwaka huu ikicheza dhidi ya Coastal Union, ambapo iliisha kwa wageni kupata ushindi wa mabao 2-1.

3# Duke Abuya (Ihefu vs Simba)

Ilikuwa ni dakika ya 41, ambapo Duke Abuya aliifungia Ihefu bao, akiitendea haki krosi ya Mkenya mwenzake, Elvis Rupia, aliifungia Ihefu bao nyumbani, Uwanja wa Liti mjini Singida, mechi iliyochezwa, Aprili 13, mwaka huu.

Lilikuwa ni kosa la kipa wa Simba, Ally Salim, kuufuata mpira huo wa krosi, lakini akaukosa, ukamkuta Duke ambaye alimuacha akiwa ameanguka chini, akamlamba chenga Fondoh Che Malone, kabla ya kuujaza wavuni kirahisi. Mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1.

2# Kipre Junior (Azam vs Namungo

Kipre Junior aliupata mpira pembeni, akaingia nao ndani, akampa Paschal Msindo, ambaye alimrudishia tena, akiwa ametengeneza nafasi nyingine mbele, akaachia shuti la mguu wa kushoto kabla ya kuachia shuti lililojaa wavuni, Azam ilipocheza dhidi ya Namungo, Aprili 14, mwaka huu, Uwanja wa Azam Complex, ikitoka na ushindi wa mabao 2-0, yote akiyafunga yeye.

1# Stephane Aziz Ki (Yanga vs Singida)

Aziz Ki alifunga bao dakika ya 65 kwa shuti kali la kuhstukiza mbali kiasi cha mita 30 kwa mguu wa kushoto ambalo lilimkuta kipa Benedict Haule akiwa hajajiandaa na kujikuta mpira ukwama wavuni.

Kazi kubwa ilianza kufanywa na mfungaji mwenyewe alipata mpira kutoka nyuma kwa Khalid Aucho, akakimbia nao umbali mrefu, kabla ya kumpa Mzize ambaye alimuacha mfungaji kakaa kwenye eneo zuri na kumrudishia tena mpira. Mechi ilichezwa Aprili 14, mwaka huu katika Uwanja wa Liti mjini Singida, Yanga ikipata ushindi wa mabao 3-0.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live