Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabadiliko yaiva Yanga

06c51ae5bba95642a4c414ed1d3a1f60 Mabadiliko yaiva Yanga

Wed, 2 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RIPOTI ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ya Yanga inatarajiwa kukabidhiwa leo kwa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.

Ofisa Habari ya klabu hiyo, Hassan Bumbuli aliliambia HabariLEO jana kuwa, ripoti hiyo iliyokuwa imefuatwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM Hersi Said nchini Hispania tayari imekabidhiwa kwenye Kamati ya Mabadiliko na leo itatua kwa Kamati ya Utendaji.

“Kesho (leo) Kamati ya Mabadiliko chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa itakabidhi ripoti kwa Kamati ya Utendaji ya Yanga kuelekea kwenye mchakato wa mabadiliko na mambo sasa yameiva tayari kwa kazi,” alisema.

Mchakato huo umekuwa ukidhaminiwa na mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo GSM ambao waliahidi kushirikiana na klabu hiyo kukamilisha mipango yote ya kuhakikisha Yanga inaendeshwa katika mfumo wa uwekezaji wa kisasa.

Katika hatua nyingine, kampuni nane zilizoomba zabuni ya ujenzi wa hosteli za kisasa na viwanja vya mazoezi Kigamboni kwa klabu ya Yanga zitafanya ziara kutazama eneo husika na kutumia fursa hiyo kuuliza maswali.

“Tutawapeleka katika eneo letu kule Kigamboni watauliza maswali na kujibiwa kisha tutasubiri kufunga Desemba 18, mwaka huu kisha tutatangaza tena,” alisema.

Bumbuli alisema bado milango iko wazi kwa wazabuni zaidi kuendelea kujitokeza kwa kuwa awamu ya pili itatangazwa kuanzia Desemba 18 hadi 30, mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz