Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabadiliko Yanga kuwabeba mashabiki

E0a751be69ef42a6af97abe180e3e94b Mabadiliko Yanga kuwabeba mashabiki

Fri, 4 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KLABU ya Yanga imekabidhiwa ripoti ya rasimu ya awali ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji huku baadhi ya mapendekezo yakiwatambua wapenzi, mashabiki na wanachama.

Ripoti hiyo ilitoka La Liga hadi kwa Kamati ya Mabadiliko chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa kwa udhamini wa GSM na kukabidhiwa kwa Kamati ya Utendaji ilipokelewa na Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla ambaye naye aliikabidhi kwa mshauri wa klabu hiyo Senzo Mazingisa ili aifanyia kazi.

Katika hafla ya makabidhiano ya ripoti hiyo iliyofanyika Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa GSM ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko, Hersi Said alisema mfumo huo utakwenda kuirudisha klabu kwenye mikono ya wanachama.

“Sisi kama GSM, Kamati ya Mabadiliko ya kimfumo tunaandika historia kwa kuleta mfumo ambao unatoka katika dunia ya kwanza ya soka, uko wazi, utaleta maslahi kwenye klabu yetu ya Yanga na niwahakikishie wanachama watakuwa wamiliki halali,” alisema Hersi.

Alisema katika mabadiliko hayo waliona pungufu moja kati ya wanachama, wapenzi na klabu yao na kuwahakikishia kupitia mabadiliko watajenga daraja ili wote wanufaike na kuwa sehemu ya familia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko, Wakili Mgongolwa alisema vipaumbele vyao viwili walivyowapa La Liga ilikuwa wawasaidie katika mchakato wa kufanya mabadiliko kwenye uendeshaji, uongozi na kimfumo na namna watakavyowahusisha mashabiki, wapenzi na wanachama.

“Tunashukuru wadhamini wetu GSM kwani taarifa itadumu vizazi hadi vizazi. Sisi tunaweza tusiwepo ila maandishi yatakuwepo. Rasimu ina kama kurusa 400 baadaye itapitiwa na kupunguza hadi kurasa 100,” alisema.

Dk Msolla alisema Senzo atashirikiana na sekretarieti na kamati mbalimbali kupata muundo mpya uliopendekezwa ili klabu ibakie mali ya wanachama na kuahidi kuunda kamati ya mabadiliko ya katiba kwa ajili ya kurekebisha katiba iendane na yale yaliyopendekezwa.

Pia alisema wako tayari kufuata ushauri watakaopewa kwa kuzingatia katiba ya nchi ili kukamilisha mchakato huo.

Alisema baadaye watafanya semina kwa viongozi wa matawi na Mkutano Mkuu na wanachama wote na kupitia.

Senzo alisema jukumu walilopewa ni rahisi na kuahidi kuwa wataipitia ripoti hiyo kuangalia mambo muhimu ya kufanyiwa kazi.

Chanzo: habarileo.co.tz