Kocha Mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps amekosoa mpango wa Shirikisho la Soka duniani (FIFA) wa Kombe la Dunia mwaka 2030 na kuhoji sababu za kimichezo na kimaadili za mashindano hayo.
Juma lililopita FIFA ilitangaza kwamba Fainali za Soka za Kombe la Dunia kwa upande wa wanaume za mwaka 2030 zitaandaliwa na nchi sita kwenye mabara matatu kama sehemu ya mpango wake wa kuadhimisha miaka 100 ya michuano hiyo.
“Nyuma ya mpango wa kuandaa michuano hiyo katika nchi nyingi tofauti, lakini pia kuna suala la mechi tatu kufanyika Bara la Amerika Kusini,” amesema Deschamps kwenye mkutano aliofanya na waandishi wa habari.
“Sijui nchi gani zitahusishwa, lakini ina maana kwamba nchi kutoka Amerika Kusini zitakuwa na faida na nchi nyingine shiriki zitatakiwa kwenda huko kucheza tena na tena.”
Kocha huyo amesema: “Sijui nani alifanya maamuzi, lakini siwezi kuficha ukweli kwamba napenda mshikamano kwenye jambo la kimichezo na kimaadili. Sidharni kama kutakuwa na umoja kule.”
Jumatano iliyopita FIFA ilikubali maombi ya nchi tatu za Morocco, Ureno na Hispania kuandaa kwa pamoja fainali za Kombe la Dunia, huku pia ikikubali kufanyika kwa mechi tatu kwenye nchi za Argentina, Paraguay na Uruguay, ambao awali waliunga mkono mpango wa nchi hizo kuandaa kwa pamoja michuano hiyo.
Mechi ya ufunguzi itafanyika katika jiji la Montevideo, ambapo kulifanyika kwa mara ya kwanza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1930. Nchi zote sita zitafuzu moja kwa moja kushiriki fainali hizo.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza Kombe la Dunia kufanyika kwenye bara zaidi ya moja.