Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu ya Mbappe, Messi, Ronaldo walivyofikisha umri wa miaka 24

Umri Pic.png Maajabu ya Mbappe, Messi, Ronaldo walivyofikisha umri wa miaka 24

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi Jumanne, Kylian Mbappe alitimiza umri wa miaka 24. Happy Birthday Kylian Mbappe. Yap, ndiyo kwanza ametimiza miaka 24, lakini kile anachokifanya uwanjani ni balaa kubwa. Masupastaa, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamekuwa na zama bora kabisa kwenye mchezo wa soka, wamevunja na kuandika rekodi moja baada ya nyingine.

Hata hivyo, hata siku moja usicheze kamari Mbappe atashindwa kufikia rekodi hizo moja baada ya nyingine na kuzivuka. Ubora wa Mfaransa huyo ni hatari. Kwa namna takwimu zake za mabao alizofunga na kuasisti akiwa hadi kufikia umri huo wa miaka 24, wamewafunika magwiji hao wawili, Messi na Ronaldo.

Mbappe aliibukia kwenye soka akiwa na umri wa miaka 17, akiwa kwenye kikosi cha Monaco msimu wa 2016-17. Aling’ara na kuifikisha nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya timu hiyo na waliibwaga PSG kwenye ubingwa wa Ligue 1. Majira ya kiangazi 2017 akiwa na miaka 18, alijiunga na PSG kwa ada ya Euro 180 milioni, uhamisho uliovunja rekodi ya dunia kwa mchezaji mwenye umri mdogo.

Na huu ni msimu wake wa sita Parc des Princes, anakaribia kabisa kuvunja rekodi ya mfungaji bora wa muda wote kwenye kikosi cha PSG, Edinson Cavani akiisaidia timu hiyo kubeba mataji manne ya Ligue 1 na mengine saba ya michuano ya ndani.

Mahali ambako Mbappe hajafikia kulinganisha na Messi na Ronaldo ni kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kutwaa tuzo ya Ballon d’Or.

Kwenye soka la kimataifa, Mbappe amekuwa kwenye ubora mkubwa kwelikweli. Alifunga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia wakati Ufaransa ilibeba taji miaka minne iliyopita huko Russia 2018. Alibeba pia Uefa Nations League mwaka 2021. Kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022, Ufaransa ilifika fainali na Mbappe alifunga hat-trick kwenye sare ya 3-3 bahati mbaya, Les Bleus ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 4-2 mbele ya Argentina ya mkali Messi.

“Kila mwaka nakuwa nawaza nani atashinda Ballon d’Or, Messi au Cristiano. Nani namfurahia? Hiyo ni kama uambiwe uchague mmoja kati ya baba au mama, huwezi,” alisema Mbappe.

Lakini, si muda mrefu, hadithi itabadilika na Ballon d’Or itakuwa inazungumzwa kwa lugha ya Mbappe. Messi na Ronaldo wamebeba tuzo hiyo mara 12 baina yao, tuzo saba na tano mtawalia. Kwa kile anachokifanya Mbappe na umri wake ndio kwanza miaka 24, kubeba Ballon d’Or ni suala la muda tu.

Messi alitimiza umri wa miaka 24 mwaka 2011. Katika kipindi hicho tayari alikuwa amebeba Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu na Ballon d’Or mara tatu.

Kwa Ronaldo, amini usiamini, alikuwa bado yupo Manchester United wakati anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ya kutimiza miaka 24. Kwa kipindi hicho alishinda kila kitu England na alibeba taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Alipotimiza miaka 24, Februari 2009, aliisaidia timu hiyo kubeba taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu England kabla ya kwenda Real Madrid alikosajiliwa kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia, Pauni 80 milioni. huko akatwaa mataji mengine manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na ndiye kinara wa mabao wa Los Blancos.

Cheki hapa, kilichotokea wakati Mbappe, Messi na Ronaldo walipotimiza miaka 24.

Kylian Mbappe

Amecheza: Mechi 363

Amefunga: Mabao 253

Ametoa: Asisti: 132

Amepiga: Hat-trick 14

Penalti: Amepata 24, amekosa 5

Mabao ya Ligi Kuu: 147

Mabao Mabingwa Ulaya: 40

Mabao kimataifa: 36

Mataji: Ligue 1 x 5, Coupe de France x 3, Coupe de la Ligue x 2, Trophee des Champions x 2, UEFA Euro Under-19 x 1, World Cup x 1, UEFA Nations League x 1

Tuzo binafsi: Mchezaji bora Ligue 1 x 3, Kiatu cha Dhahabu x 1, Kinara wa mabao Ligue 1 x 4

Lionel Messi

Amecheza: Mechi 326

Amefunga: Mabao 197

Ametoa: Asisti 84

Amepiga: Hat-trick 10

Penalti: Amepata 19, amekosa 24

Mabao ya Ligi Kuu: 119

Mabao Ligi ya Mabingwa Ulaya: 37

Mabao kimataifa: 17

Mataji: La Liga x 5, Champions League x 3, Copa del Rey x 1, Supercopa de Espana x 3, UEFA Super Cup x 1, FIFA Under-20 World Champions x 1, Olimpiki x 1

Tuzo binafsi: Ballon d’Or x 2, Kiatu cha Dhahabu Ulaya x 1, Mchezaji bora La Liga x 3, Pichichi (Mfungaji bora La Liga) x 1

Cristiano Ronaldo

Amecheza: Mechi 362

Amefunga: Mabao 132

Ametoa: Asisti 66

Amepiga: Hat-trick 1

Penalti: Amefunga 16, amekosa 4

Mabao Ligi Kuu: 78

Mabao Ligi ya Mabingwa Ulaya: 11

Mabao kimataifa: 21

Mataji: Super Cup Ureno x 1, Premier League x 2, FA Cup x 1, Kombe la Ligi x 1, Ligi ya Mabingwa Ulaya x 1, Toulon Tournament x 1

Tuzo binafsi: Ballon d’Or x 1, Kiatu cha Dhahabu x 1, Mchezaji Bora Ligi Kuu England x 2, Mchezaji bora wa mwaka PFA x 2, Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu England x 1.

Chanzo: Mwanaspoti