Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu ya Euro 2024, kila mtu ana bei yake

Mastaa Wa Euroooo Maajabu ya Euro 2024, kila mtu ana bei yake

Tue, 18 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Euro 2024 imesheheni mastaa wa soka wenye majina makubwa duniani. Kutokana na hilo, ndiyo maana si kitu kinachoshangaza kuona hata thamani za bei zao sokoni zikiwa kubwa pia.

Kwa mujibu wa Transfermarkt, Euro 2024 imekusanya wachezaji wenye thamani kubwa sana sokoni, ambapo baadhi yao watatumia fainali hizo kama jukwaa la kujiweka sokoni na kunaswa na timu nyingine hasa ukizingatia hiki ni kipindi cha usajili wa dirisha la majira ya kiangazi likiwa linaendelea huko Ulaya.

Kwenye orodha ya vikosi 24 zinavyochuana kusaka ubingwa huo wa Ulaya, kwenye kila timu moja kuna mchezaji mmoja mwenye thamani kubwa sokoni kuzidi wengine. Kwa mastaa wote 624 waliopo kwenye fainali hizo, kiungo wa England, Jude Bellingham anashika namba mbili kwa kuwa na thamani kubwa zaidi sokoni, nyuma ya straika wa Ufaransa, Kylian Mbappe - huku wawili hao kuanzia msimu ujao wa 2024-25 watakipiga kwenye kikosi kimoja cha Real Madrid huko Santiago Bernabeu.

England thamani ya kikosi kizima ni Pauni 1.2 bilioni, huku supastaa wao, Bellingham akiongoza kwa kuwa na thamani kubwa, akithaminishwa na Transfermarkt kuwa na thamani inayofikia Pauni 165 milioni.

Mbappe kwenye kikosi chake cha Ufaransa anathaminishwa kuwa na thamani inayofikia Pauni 170 milioni, huku timu yake ya Les Bleus ikiwa na thamani ya Pauni 1.1 bilioni. Kwenye fainali hizo za Euro 2024, Three Lions na Les Bleus ndiyo timu zenye vikosi vilivyozidi Pauni 1 bilioni na ndiyo maana vinapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mikikimikiki hiyo inayofanyika Ujerumani.

Kwa kuzingatia mchezaji mmoja mwenye thamani kubwa kwenye kila kikosi cha timu hizo zilizopo kwenye fainali hizo za Euro 2024, kwenye kikosi cha Ureno yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 898 milioni, mbabe wao mwenye thamani kubwa kuzidi wengine ni Rafael Leao, thamani yake ni Pauni 76 milioni, wakati miamba mingine ya soka la Ulaya, Hispania yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 784 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa ni kiungo Rodri, mwenye thamani ya Pauni 98 milioni huko sokoni kwa mujibu wa Transfermarkt.

Uholanzi yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 686 milioni, supastaa wao Xavi Simons, ndiye anayeongoza akiwa na thamani ya Pauni 68 milioni, huku Ujerumani yenye timu yenye thamani ya Pauni 679 milioni, mkali wao mwenye thamani kubwa ni Jamal Musiala, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 100 milioni.

Italia na timu yao yenye thamani ya Pauni 591 milioni, staa wao mwenye thamani kubwa ni Nicolo Barella, anayethaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 64 milioni, wakati kwenye kikosi cha Ubelgiji chenye thamani ya Pauni 510 milioni, mchezaji anayeongoza kwa thamani kubwa ni Jeremy Doku, akithaminishwa kwa Pauni 59 milioni huko sokoni, huku Denmark yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 358 milioni, staa wao mwenye thamani kubwa sokoni ni Rasmus Hojlund, mwenye thamani ya Pauni 54 milioni.

Uturuki yenye kikosi cha Pauni 321 milioni, yenyewe mchezaji wao mwenye thamani kubwa sokoni ni Hakan Calhanoglu mwenye thamani ya Pauni 35 milioni, huku Ukraine yenye kikosi cha Pauni 307 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa kikosini ni Oleksandr Zinchenko, Pauni 37 milioni, wakati Croatia yenye timu yenye thamani ya Pauni 286 milioni, mkali wao mwenye thamani kubwa sokoni ni Josko Gvardiol, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 64 milioni.

Serbia yenye timu yenye thamani ya Pauni 263 milioni, straika wao Dusan Vlahovic, ndiye mwenye thamani kubwa sokoni, Pauni 54 milioni, wakati Uswisi na timu yao ya Pauni 225 milioni, staa wao mwenye bei kubwa sokoni ni Manuel Akanji, Pauni 36 milioni, huku Austria yenye timu yenye thamani ya Pauni 192 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa ni Konrad Laimer, anayethaminishwa na Transfermarkt kuwa na thamani ya Pauni 23 milioni na Scotland yenye timu yenye thamani ya Pauni 174 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa ni Andrew Robertson, Pauni 30 milioni.

Poland ya Robert Lewandowski, yenye kikosi chenye thamani ya Pauni 167 milioni, staa wao mwenye bei kubwa sokoni ni Piotr Zielinski, Pauni 21 milioni, huku Jamhuri ya Czech yenye timu yenye thamani ya Pauni 148 milioni, staa wao Tomas Soucek ndiye mwenye thamani kubwa zaidi, Pauni 30 milioni huku Hungary yenyewe na timu yao ya Pauni 141 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa zaidi sokoni ni Dominik Szoboszlai, Pauni 66 milioni.

Slovakia na kikosi chao cha Pauni 141 milioni, staa wao mwenye thamani kubwa ni beki Milan Skriniar, Pauni 34 milioni, huku Georgia na timu ya Pauni 135 milioni, mchezaji mwenye thamani kubwa ni Khvicha Kvaratskhelia, Pauni 74 milioni, wakati Slovenia yenyewe timu yake ina thamani ya Pauni 114 milioni na staa wao Benjamin Sesko ndiye mwenye thamani kubwa, Pauni 33 milioni, huku Albania yenye kikosi cha Pauni 92 milioni, mchezaji wao mwenye thamani kubwa ni Armando Broja, Pauni 22 milioni na timu yenye thamani ndogo zaidi kwenye fainali hizo ni Romania, Pauni 74 milioni na mchezaji wao mwenye thamani kubwa kwa mujibu wa Transfermarkt ni Radu Dragusin, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 21.

Chanzo: Mwanaspoti