Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu ya Biashara United Ligi Kuu Bara

99040 Pic+biashara Maajabu ya Biashara United Ligi Kuu Bara

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Dar es Salaam. Wakati jahazi la Singida United likizidi kuzama katika Ligi Kuu Bara, Biashara United ya Musoma mkoani Mara haishikiki kwenye ligi hiyo.

Licha ya kuwa ni timu ndogo, lakini imekuwa na kiwango bora kiasi cha kuwashtua baadhi ya wadau soka nchini huku ikibebwa na wachezaji wake kama Innocent Edwin (mwenye mabao matano), Ramadhan Chombo ‘Redondo’, James Mwasote, Bright Obina, Atupele Green na Nahodha Abdulmajid Mangalo.

Biashara United imeanza kujiondoa kwenye presha ya kushuka daraja kwani kwa sasa iko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imecheza michezo 28, imeshinda 10, imetoka sare tisa na kupoteza tisa ikiwa na pointi 39.

Timu hiyo inayonolewa na kocha Mkenya, Francis Baraza, katika michezo 12 ya hivi karibuni imeshinda sita, sare nne na kupoteza miwili dhidi ya Simba na Lipuli FC.

Kocha huyo alitua nchini Novemba, mwaka jana na kuanza kibarua katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliofanyika Novemba 23 ambao ulimalizika kwa suluhu.

Baraza ameisadia Biashara United kuwa katika kiwango bora kwani tangu aanze kuinoa ameiongoza kwenye michezo 18, imeshinda minane, imetoka sare saba na kupoteza mitatu dhidi ya Yanga, Simba na Lipuli.

Pia Soma

Advertisement
Kocha huyo anasema kiwango bora cha timu kwa sasa kinatokana na mambo matatu makubwa.

Kikosi/nidhamu ya wachezaji

Baraza anasema alipotua jambo la kwanza lilikuwa kuwasoma wachezaji kuanzia uchezaji hadi tabia na baadaye kukaa na kuzungumza nao kama mzazi.

“Niliongea nao kwa kirefu na kuwaambia kuwa wao ndio wataamua waibakishe timu au waishushe (daraja) na pia mimi kama kocha nawaamini, kwa nini wao pia wasijiamini uwanjani,” anasema. “Pia kuna kitu nilikibadilisha kwao kwani wakati nafika mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini cha kushangaza wakati tukijiandaa karibu wachezaji saba hawakuwepo, nilipouliza niliambiwa wana ruhusa.

“Nikaona hilo ni tatizo na hakuna umakini kuanzia kwa viongozi hadi wachezaji kwani haiwezekana ukawaruhusu wachezaji kila mara wakati ligi inaendelea lazima wakirejea hawatakuwa fiti. Sasa hivi kila kitu kimebadilika na nimesimamia jambo hilo, na huoni tena wachezaji wakiomba ruhusa bila sababu ya msingi.”

Udhamini

Baraza anasema wadhamini wao, Barrick, wameongeza morali ndani ya timu na hivyo kuwafanya wachezaji kujituma zaidi uwanjani. “Kwa kweli nawashukuru kwani hakuna kazi kubwa kama kuendesha timu, wachezaji wakilia njaa maana yake hawatacheza vizuri, lakini wadhamini wanatusaidia sana.”

Benchi la ufundi/mashabiki

Baraza anasema siyo hayo tu, lakini pia wanapata sapoti nyingine, “nashukuru tangu nimefika nimekuwa na maelewano mazuri na benchi langu la ufundi na wanaelewa kitu gani nataka.

“Pia mashabiki nao wamekuwa chachu kubwa ya timu kufanya vizuri kutokana na jinsi wanavyokuja kwa wingi uwanjani na kutupa sapoti.”

Nahodha wa Biashara United, Abdulmajid Mangalo anasema kitendo cha wachezaji kupeana moyo kabla ya mechi kimechangia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri katika michezo ya hivi karibuni.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay anasema Baraza ametengeneza mfumo unaoendana na aina ya wachezaji alionao. “Aliangalia wachezaji wake na kutengeneza mfumo unaoendana nao, ndio maana timu inafanya vizuri. Pia safu ya ulinzi inasaidia kupandisha mashambulizi mbele,” alisema Mayay.

Chanzo: mwananchi.co.tz