Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu mbele wembe, nyuma uchochoro kuendelea?

KMKM X JKU Maajabu mbele wembe, nyuma uchochoro kuendelea?

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) iliyosimama kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea Ivory Coast inayotarajiwa kurejea kesho, lakini kabla ya kusimama Novemba, mwaka jana ilijaa maajabu ambayo hapana shaka mashabiki wa soka watakuwa wanajiuliza iwapo yataendelea.

Kabla ya kusimama kwa ligi hiyo, iliyoanza kuwa na mvuto wa kipekee katika misimu ya hivi karibuni kutokana na udhamini kumiminika visiwani humo, ilikuwa na mambo ya kushangaza kutoka kwa timu shiriki.

Ligi hiyo iliacha rekodi flani za kusisimua na pengine kushangaza kutokana na namna ambavyo kilipigwa.

Mathalan, ligi hiyo ambayo inahusisha timu 16 ikiwa katika raundi ya 15, imeshuhudia jumla ya mabao yote ya kufunga na kufungwa kwa timu hizo yakilingana ambapo zimefunga mabao 237 na kufungwa 237.

Hii ina maana kwamba ukichukua idadi ya jumla ya mabao hayo (237) yaliyoingia katika nyavu za timu zote 16 ni sawa na kusema washambuliaji kwa ujumla walikuwa hatari kufumania nyavu, huku mabeki wakiwa uchochoro kwa kuruhusu mabao mengi.

Si hivyo tu, lakini tofasiri nyingine ya mabao hayo inaweza kuwa na maana kwamba ligi kwa ujumla imeshuhudia utamu wa mabao.

Katika msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na JKU yenye alama 36, timu tano za juu zote ama zina mabao 20 au zaidi ya kufunga.

Msimamo unaonyesha kwamba JKU iliyopo kileleni imefunga mabao 21 ikifuatiwa na Zimamoto yenye alama 30 iliyofunga mabao 23, ya tatu ni KMKM ina pointi 29 imefunga 22 huku nafasi ya nne ikikimatwa na KVZ yenye mabao 20 ilhali ikiwa na alama 27 na inayofunga tano bora ni Kipanga yenye pointi 24 na mabao ya kufunga 20.

Kutokana na idadi hiyo ya mabao ina maana kwamba timu tano za juu kwa ujumla wake zimefunga mabao 106, huku timu zingine (kufuatana na nafasi zinayoshika kwenye msimamo na mabao ziliyofunga katika mabano) ni Uhamiaji (11 ), Mlandege (9 ), Chipukizi (10 ), Mafunzo (12 ), Hard Rock (10 ), Kundemba (17), New City (16 ), Malindi (13 ), Jamhuri (10 ), Ngome (12) na Maendeleo inayoburuza mkia ikiwa na mabao 11.

Kwa kuzingatia idadi ya mabao ya kufunga timu zilizopo katika nafasi tano za chini zimefumania nyavu na kuvuna mabao mengi zaidi kuliko zile zinazokamata nafasi za katikati ya msimamo kwa ujumla wake, kwani zimekusanya mabao 62, huku tano zinazofuata juu yake zikifunga 58.

Upande wa mabao ya kufungwa, timu tano za juu na tano zinazozifuatia zinatofautiana jumla ya mabao mawili tu kwani zile tano za juu zimefungwa 55 huku zinazozifuatia (namba 6-10) zikifungwa 57.

Utamu za ZPL haujaishia hapo kwani katika kufungwa zile tano za mkiani zimeruhusu jumla ya mabao 106 sawa na jumla ya mabao ziliyofunga timu tano zilizopo juu ya msimamo wa michuano hiyo ambazo zimefunga 106.

Katika upande wa pointi, jumla ya alama zilizovuna timu tatu za juu (Top 3) ambazo ni 95 ni zaidi ya jumla ya alama zote ambazo zimekusanywa na timu sita za mkiani zilizokusanya alama 85. Kwa ujumla timu zote zimevuna alama 323.

Akizungumzia ligi hiyo, mdau wa soka Zanzibar, Abdul Hajj Karim amesema ZPL imeendelea kuwa bora kutokana na udhamini ulioanza kujitokeza miaka ya karibuni, lakini kuna maajabu mengi ya ndani na nje ya viwanja.

"Kuna fedha nyingi zinaingia ambazo zinarahisisha mambo flani kufanyika kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wakati mwingine timu zilishindwa hata kusafiri," amesema.

Naye Mwambani Mohamed Miraj amesema pamoja na msukumo huo, pia ligi hiyo imekusanya vipaji vingi vya soka hivyo haoni ajabu mabao ya kufunga na kufungwa yakilingana.

"Kuna vijana wamoto sana kwa sasa katika Ligi Kuu Zanzibar ambao wanacheza boli kwelikweli. Ni vyema tu ukajua kwamba vipaji hivi vikitoka kwenda nje ya Zanzibar vitatisha sana," amesema.

Chanzo: Mwanaspoti