BAADA ya Simba kutwaa kibabe ubingwa wao wa nne mfululizo wakiifunga Coastal Union 2-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam juzi, Ligi Kuu Bara imebakiza raundi mbili ili ifikie tamati.
Ni raundi mbili za moto kwani ndizo zitakazotoa hatima ya timu kushuka daraja, kunusurika na ushindani wa kuwania tuzo binafsi kama vile mchezaji bora wa msimu, mfungaji bora, kipa bora, kinda bora na kadhalika.
Mechi za mwisho mara nyingi huambatana na mambo mengi yasiyotarajiwa na matokeo ya kushangaza ambayo yanaweza kuacha kilio au furaha kwa timu au wachezaji husika.
Makala hii inakuletea orodha ya mambo sita yasiyotegemewa ambayo yanaweza kutokea katika raundi hizo mbili za mwisho tofauti na matarajio ya wengi.
COASTAL, GWAMBINA NA IHEFU KUNUSURIKA
Coastal Union inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 34, huku Gwambina ikiwa nafasi ya 16 na pointi zake 34 na Ihefu iliyo na pointi 35 inashika nafasi ya 15.
Kwa mujibu wa kanuni za ligi, timu zilizopo katika nafasi ya 15 hadi ya 18 kwenye msimamo wa ligi, zitashuka daraja moja kwa moja na tayari Mwadui inayoshika mkia imeshadondokea Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Hata hivyo Coastal, Ihefu na Gwambina zinaweza kunusurika kushuka moja kwa moja kwa kupata nafasi ya kucheza mchujo au kubaki jumla ikiwa kila moja itashinda mechi zake mbili zilizobakia na pia timu za JKT Tanzania, Mbeya City, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting zikapoteza mechi zao zote zilizobakia.
NAMUNGO KUIPIKU BIASHARA UNITED
Biashara United inahitaji pointi moja tu ili ifikishe jumla ya pointi 50 ambazo zitaipa tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Hata hivyo, kama itapoteza mechi zake mbili ilizobakiza dhidi ya Prisons na Mbeya City inaweza kupoteza fursa hiyo mbele ya Namungo FC yenye pointi 43 ambayo imebakiza mechi dhidi ya Simba na Ruvu Shooting
MUGALU KUWA MFUNGAJI BORA
John Bocco ndio kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu akiwa amepachika mabao 15 nyuma yao akiwepo Prince Dube mwenye 14 na Chris Mugalu mwenye mabao 13.
Hata hivyo, kama Bocco na Dube wasipozitumia vyema mechi mbili zilizobakia kwenye timu zao, wanaweza kujikuta wakifikiwa au kuachwa kwenye mataa na Mugalu.
MWADUI KUFA NA MTU
Mwadui FC imeshuka daraja na sasa inacheza kukamilisha tu ratiba ya ligi hiyo na kuanza kujipanga kwa ajili ya Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao
Kiwango bora ilichoonyesha dhidi ya Yanga katika mchezo ambao ilifungwa mabao 3-2 kinatoa ishara kwa timu ambazo itacheza nazo katika mechi zao mbili za mwisho, Polisi Tanzania na Coastal Union kutoibeza na kudhani zitapata ushindi kirahisi dhidi yao
Coastal Union ndio inapaswa kuwa makini zaidi kwani inahitajika kushinda mechi dhidi ya Mwadui ili kujaribu kujinusuru na janga la kushuka daraja vinginevyo inaweza kwenda na maji.
NAMUNGO KUCHEZA MCHUJO
Licha ya kuwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 43, Namungo FC inaweza kujikuta katika kundi la timu mbili za kucheza mechi za mchujo (play off) ikiwa itafungwa mechi zake mbili dhidi ya Ruvu Shooting na Simba kisha timu zilizo chini yake zikapata ushindi kwenye mechi zao.
AZAM KUIPIKU YANGA
Kwa sasa Yanga iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 70 na Azam FC iko nafasi ya tatu na pointi zake 64.
Ikiwa Azam FC itapata ushindi katika mechi zake mbili dhidi ya Simba na Ruvu Shooting na Yanga ikapoteza dhidi ya Ihefu na Dodoma Jiji, Azam FC inaweza kumaliza katika nafasi ya pili na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwani itafikisha pointi sawa na Yanga na inaweza kunufaika na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa sasa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa wa Yanga ni mabao 29 wakati ule wa Azam FC ni mabao 27.
Tanzania Bara mara hii itawakilishwa na timu nne Afrika.