Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maagizo mapya manne Ligi Kuu

Mzize Red Eyes Maagizo mapya manne Ligi Kuu

Thu, 1 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uliona macho ya mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize wakati anaipiga Hat trick Hausung juzi? Basi ule ndio unaitwa ugonjwa wa macho mekundu ‘Red eyes’. Kabla Ligi Kuu haijarejea klabu zimepewa maagizo mapya manne ya kufuata. Na Mamlaka za soka zimeenda mbali zaidi na kusema timu ikijichanganya tu inaweza kupoteza mchezo husika nje ya uwanja.

Tangu maradhi hayo yaanze mchezaji wa kwanza kuonekana uwanjani akicheza akiwa na tatizo hilo ni Mzize kwenye mchezo huo wa Shirikisho ambao Yanga ilishinda mabao 5-1 huku akiweka wavuni mabao matatu.

Baada ya mchezo huo, picha za Mzize kusambaa zilianza kuzusha maswali juu ya imekuwaje mshambuliaji huyo ameruhusiwa kucheza wakati akiwa anaugua maradhi hayo lakini hata hivyo Chama cha Madaktari wa Tiba za Wanamichezo (TASMA) kimemtetea.

Wakati Ligi Kuu Bara ikiendelea Februari 2, Tasma kupitia Katibu Mkuu wake Dokta Juma Sufian akasema wametoa maagizo yafuatayo kwa madaktari wa klabu zote;

Kwanza, wasisitize muda wote wachezaji na watu walioko kambini kunawa mikono. Pili,hakuna kushikana mikono au kukumbatiana. Tatu, Hakuna kuweka mikono machoni hata kama ni wakati wa kushangilia. Lakini la Nne kutoka Bodi ya Ligi ni, kila timu lazima izingatie kanuni na kinyume na hapo wasipoleta kikosi uwanjani pointi zimeenda.

Sufian anasema mchezaji anaruhusiwa kucheza akiwa na maradhi hayo kutegemeana na yeye anavyojisikia kwa vile siyo hatarishi bali yanatesa.

“Ujue haya maradhi ya macho yanambukizwa kwa njia ya mtu kugusa macho yake, ukigusa macho aidha unafuta au kufanya lolote na baadaye ukaenda kumshika mkono mtu mwingine ambaye hana basi utakuwa umemuambukiza,” alisema Sufiani.

“Wakati mwingine sio lazima ukamguse ambaye hana lakini inatokea yule mwenye maradhi hayo akagusa hata kitasa cha mlango au chombo chochote ambacho kikishikwa na mtu mwingine asiyekuwa na maradhi haya bado ataambukizwa.

“Ingekuwa mbaya kama maradhi haya yangekuwa yanaambukizwa kwa njia ya hewa kama ilivyokuwa Uviko 19 hapo tungesema kuna hatua kubwa zaidi za kuchukua, huu ni ugonjwa ambao unasumbua tu, maumivu yake ni ya kawaida labda yakiwa makali utaugua kichwa kwa kiasi na hata macho kuuma na kuwasha.”

LIGI INACHEZEKA

Sufiani aliongeza licha ya mlipuko huo bado ligi inaweza kuendelea ingawa wameshawasiliana na madaktari wa klabu za ligi kuhakikisha wanazingatia kutoenea kwa maambukizi wakati wachezaji wakiwa kambini na viwanjani.

“Kuhusu ligi kusimama sioni hilo sana labda hali iwe mbaya kwa kiasi kikubwa sana, mpaka sasa tunavyozungumza kesi ambayo tunayo ni hii ambayo tumeiona ya huyu mchezaji wa Yanga (Mzize) hatujajua mpaka anacheza labda daktari wa timu yake aliona kama amepona au ana anafuu.

“Tumeshawasiliana na madaktari wa klabu zote ambao ni wanachama wetu wa TASMA kwanza tunawaamini kwa maradhi haya hatuna shaka wanajua hatua za kuchukua za kupunguza maambukizi, kubwa ni juu ya usafi kwenye mikono yao.”

“Tunashauri nyakati hizi sio salama tena kusalimiana kwa kupeana mikono, kufanya hivyo kama ukigusana mikono na mtu ambaye amegusa macho yake na anaugua maradhi haya basi atakupa na wewe.”

UNAKUMBUKA ISHU YA SIMBA?

Msimu mmoja uliopita kuna balaa moja liliikumba Simba ikiwa kwenye maandalizi ya kucheza na Kagera Sugar ugenini na kikosi cha wekundu hao kilisafiri mpaka mkoani humo tayari kwa mchezo huo.

Kabla ya kuondoka tayari Simba ilikuwa na idadi ya wachezaji wachache waliokuwa wanaugua mafua makali na kikohozi na baada ya kufika Kagera siku moja kabla ya mchezo maambukizi hayo yaliongezeka kiasi cha kundi kubwa la wachezaji na hata maafisa wake kuugua.

Mchezo huo ulilazimika kusogezwa mbele baada ya Simba kuliripoti mapema hatua ambayo ilikaribia kuuweka mchezo huo kwenye mashaka ya kuchezeka ingawa baadaye mechi ikachezwa baada ya wachezaji afya zao kuwa sawa.

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Almasi Kasongo alisema wao hawataingilia miongozo inayotolewa na watu wa afya lakini akazikumbusha klabu kuzingatia kanuni za ligi wakati wa kupambana na maradhi hayo.

Na hawatarudia kilichotokea kwa Simba wakati ule.Kasongo alisema kanuni zao ziko wazi, kila klabu imepewa nafasi ya kusajili wachezaji 30 ambao wataweza kuhakikisha wapo ambao watakuwa tayari kucheza mechi na ikitokea timu imeshindwa kufika uwanjani kwa maradhi hayo itapokonywa alama tatu na mabao matatu zote zikitua kwa mpinzani.

“Naikumbuka hiyo ishu ya Simba na nafikiri mkiwa sawa na kanuni mtaona baada ya tukio lile tulibadilisha kanuni zetu, tukaenda kuchukua zile za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) ambazo walizitengeneza wakati wa mlipuko wa maradhi ya Uviko 19,” alisema Kasongo.

“Kanuni ile inasema wazi kama timu itashindwa kuleta timu uwanjani kutokana na ugonjwa wa mlipuko basi itapoteza mchezo husika, timu pinzani itapewa alama tatu na magoli matatu, kwa hiyo tunaomba klabu zihakikishe zinakuwa sawa huko ili mambo kama haya yasije yakatufikisha huko. Tunaamini wachezaji 30 hawawezi kuugua wote.”

Sura ya VI kuhusu Tiba na Bima ya Kanuni za ligi, kanuni ya 209(4) inasema “Ikitokea mchezo umeshindwa kuchezwa kutokana na sababu za kutotimiza idadi ya wachezaji wanaohitajika kikanuni kutokana na sababu za kiafya zilizosababishwa na magonjwa ya mlipuko, timu husika itakuwa imepoteza mchezo na timu shindani itapewa ushindi wa pointi tatu(3) na mabao matatu(3).”

HALI ILIVYO TANZANIA BARA

Ugonjwa wa macho, maarufu kwa jina la ‘red eyes’ umeathiri zaidi Watanzania 5,359 katika mikoa 17 ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 4,250 ndani ya siku zisizozidi 10. Watalaamu wanasema asilimia 80 mlipuko huo husababishwa na kirusi cha ‘Adenovirus’.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya afya zilizotolewa siku Januari 30, mwaka huu, kwa Dar es Salaam pekee, idadi imepanda kutoka 869 hadi 4,792 ndani ya wiki mbili.

Pamoja na Jiji la Dar es Salaam, mikoa mingine ni Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza.

Uchambuzi wa Mwanaspoti umebaini ugonjwa huo kusababisha hali ya taharuki kwenye makundi mbalimbali ikiwemo kwa wanamichezo ingawa tahadhari zinaendelea kutolewa. Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio alitoa tahadhari hivi karibuni kwa wanaotumia njia za asili ikiwamo kukamulia maziwa ya mama anayenyonyesha kwenye jicho lililoambukizwa, kuliosha kwa maji yenye chumvi au kwa chai ya rangi.

“Hairuhusiwi kutumia maji ya chumvi wala chai ya rangi, wengine wanatumia kunawa uso au macho na mama anayenyonyesha huwa anaweka maziwa yake, vyote hivyo haviruhusiwi na vinaweza kuleta madhara kwenye macho,” anasema.

Unapopatwa na maambukizi hayo kwa mujibu wa Dk Bernadetha, unapaswa kuendelea na utaratibu wa siku zote wa kujisafisha, kama kuoga na kuosha uso kawaida.

“Mtu akipata shida anaoga kama kawaida, anatumia taulo lake kujifuta uso kama kawaida lakini asichangie na mtu yeyote taulo hiyo.

“Kama kuna tongotongo au machozi yanayotoka machoni, unashauriwa kujifuta kwa tishu tena pembeni ya jicho na sio katikati,” anasema.

Kufuta katikati au kutumia nguo ngumu, anasema kunaweza kusababisha uvimbe zaidi au macho kuuma, kisha unapaswa kutupa hicho unachotumia kujifutia na unawe mikono.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, haishauriwi kutumia kitambaa kwa kuwa utakihifadhi na baadaye kukitumia tena, jambo linalosababisha kujiongezea ugonjwa.

Hata hivyo, anasema matumizi ya kitambaa yanaweza kusababisha maambukizo ya bakteria jichoni au jeraha la kemikali na hivyo kupoteza uwezo wa kuona kabisa.

Kulingana na mtaalamu huyo, inashauriwa mgonjwa asikimbilie hospitali haraka, labda pale anapokabiliwa kiasi cha kushindwa kuvumilia.

Msingi wa ushauri huo ni kile kilichoelezwa na Dk Bernadetha kuwa, kuna hatari ya kusambaza zaidi ugonjwa huo kwa kuwa hospitali unakutana na watu wengi, pia mwanga.

“Mtu akipata hiyo shida, atulie, augulie mwenyewe, azingatie kunawa mikono kwa vitakasa mikono au sabuni na inapotokea unapiga chafya funika pua pamoja na mkono ili usisambaze. “Kwa sababu kuna uhusiano mikubwa kati ya ugonjwa wa macho na pua na mdomo kwa kuwa ugonjwa unaweza kuenea kwa njia mbalimbali,” anasema.

VIPI MATIBABU? Kuhusu tiba, Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo anasema bado hakuna tiba maalum ya maambukizi hayo, badala yake dalili zake zinakadiriwa kuisha kwa muda wa wiki mbili hadi sita kwa baadhi ya watu.

“Wagonjwa wanashauriwa kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa dawa ya kupunguza madhara kulingana na ishara zinazoonwa na daktari,” anasema.

Profesa Rugajjo anasema kuna namna lukuki zitakazowezesha kuzuia ugonjwa huo, ikiwemo kuepuka kugusa macho na iwapo utafanya hivyo unapaswa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Anasema vile vinavyogusa macho yako unapaswa ama kuvitupa au kuvisafisha kwa maji ya moto na sabuni, lakini haupaswi kuchangia vipodozi, taulo za karatasi, nguo na dawa za macho.

“Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pia tumia taulo tofauti na leso kwa kila mwanafamilia,” anasema. Mtu anaambukizwa ugonjwa huo, kwa kugusa machozi au tongotongo kutoka kwenye macho yenye ugonjwa huo. Anasema kugusana mikono na mtu mwenye maambukizo hayo ni sababu nyingine ya kuambukizwa ugonjwa huo na dalili zake huanza kujitokeza kuanzia siku tano hadi 14 baada ya kupata vimelea.

Hata hivyo, anasema wanafunzi wanaougua wanashauriwa kukaa nyumbani hadi dalili zinapoisha kwa kuwa ni ngumu kuzuia maambukizo yasisambae kwenye mazingira ya shule. Profesa Rugajjo anasema unapoona jicho linakuwa jekundu, linawasha na kuchomachoma, macho yanavimba, yanaogopa mwanga, yanatoa matongotongo meupe na ya njano ujue una dalili za ugonjwa huo.

“Uwezo wa kuona unakuwa kama kuna ukungu na unasikia maumivu ya macho hizi zote ni dalili za Red Eyes,” anasema. Kwa ujumla wake, anasema ugonjwa huo unasababishwa na kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho na husambaa kwa kasi kubwa.

4,500 WAUGUA ZANZIBAR Zaidi ya watu 4,579 wameugua ugonjwa wa macho mekundu (red eyes) kisiwani Zanzibar. Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, alitoa kauli hiyo ofisini kwake jana ambapo alisema wagonjwa hao wameripotiwa katika hospitali na vituo vya afya vya Serikali na binafsi.

Hata hivyo, Mratibu wa huduma za Afya Msingi ya Matibabu ya Macho, Rajab Mohammed Hilali alisema athari za ugongwa huo ni kupunguza uoni wa macho kwani virusi hivyo vinaathiri milango ya macho.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Hafidh alisema Serikali inachukua juhudi kuhakikisha kasi ya maambukizi ya maradhi yasiyopewa kipaombele hayawezi kuwa janga la jamii.

“Kusambaa kwa maradhi hayo inategemeana na tabia za wanajamii husika,hivyo ni wajibu wetu kila mmoja kuhakikisha anaepukana na tabia hatarishi zinazopelekea kupata na kusambaza maradhi,” alisema Hafidh.

Akizungumzia hali ya maradhi ya hayo, Mratibu wa maradhi yasiopewa kipaumbele Zanzibar, Dk Shaali Ame alisema maradhi hayo ambayo yanayosumbua zaidi kisiwani hapa ni kichocho, ugonjwa wa matende na tatizo minyoo.

Maradhi haya yanazikumba zaidi nchi za kimasikini kutokana na ukosefu wa mahitaji maalumu ikiwemo maji safi na salama.

Chanzo: Mwanaspoti