Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maafande watasumbua sana

Maafande Watasumbua Maafande watasumbua sana

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kipindi fulani tukaanzisha mjadala wa kibaguzi kwamba timu zilizo chini ya taasisi za kijeshi zipunguzwe katika ligi zetu za madaraja tofauti kwa sababu mbalimbali.

Kuna waliotoa sababu kwamba timu hizo zikiwa nyingi, zitakuwa zinapanga matokeo hasa inapofika muda wa moja au mbili kuhitajika kupanda daraja au kupigania kubaki katika daraja husika.

Wengine wakatuambia kwamba hizo timu zipunguzwe kwa vile zimekuwa zikiongoza kwa kufanya vurugu kwa mashabiki, wachezaji na makocha wa timu pinzani, viongozi wa mamlaka za soka na hata marefa.

Kama kawaida yetu, tukaidandia haraka haraka dhambi hiyo ya kuzibagua timu za kijeshi na tukaanza kutengeneza mazingira ya kuzishusha daraja kilazima na nyingine kushawishi kambi ambazo zilikuwa zinazisimamia kuziuza kwenda kwa raia.

Lakini hoja zote zile mbili ambazo zilikuwa zinatumika kama sababu hazikuwa na mashiko wala ushahidi uliojitosheleza maana hata hizo timu za kiraia ambazo tulikuwa tunataka ziwe nyingi nazo zilikuwa na matatizo hayohayo ambayo tulikuwa tunayatumia kama sababu ya kuhalalisha dhambi yetu kwa timu za majeshi.

Zipo timu za kiraia ambazo zimekuwa vinara wa vurugu na matendo ya hujuma lakini pia zipo zinazopanga matokeo sasa hili liko wazi ni vile tu tuliamua kumpa mbwa jina baya.

Sasa ghafla timu za majeshi ziko kibao katika ligi ya Championship licha ya mapambano yale ya kuzishusha na sababu ya hili iko wazi kwamba taasisi hizi zinamudu kuwapa huduma muhimu na kwa wakati wachezaji, makocha na maofisa wengine wa timu za ligi ya hiyo ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kutokuwa na udhamini kwa muda mrefu.

Hizo timu za kiraia tunazozitaka nyingi hazina uhakika wa kuwapa huduma nzuri wachezaji na misuli imara ya kiuchumi na ndio maana zinasalimu amri mbele ya maafande.

Chanzo: Mwanaspoti