Uongozi wa JKT Tanzania umejitokeza hadharani na kuweka wazi hauna mpango wa kuachana na kocha wao mkuu, Malale Hamsini anayehusishwa kuondoka huku ikielezwa anawindwa vikali na Mtibwa Sugar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa timu hiyo, Godwin Ekingo alisema licha ya taarifa juu ya kuhusishwa kuondoka kwa Malale ila wao kama viongozi hawana mpango wa kuachana naye kwa sasa.
"Watu wanapaswa kuelewa Malale ana mkataba wa muda mrefu na sisi hivyo hatuwezi kuachana naye kwa sababu tuna tambua uwezo wake na tunahitaji kuendelea naye kwa msimu huu unaoanza," alisema.
Kuhusu suala la Malale la kutoenda na timu Shinyanga kwenye maandalizi ya msimu 'Pre Season', Ekingo alisema yeye alisafiri na meneja kabla ya kikosi kuondoka ili wakaweke mambo yote sawa.
"Kocha aliondoka kabla ya timu kuanza safari kwa sababu alihitaji kwenda kuona sehemu ambayo tutafikia ili ajiridhishe kama ni tulivu kwa maandalizi yetu hivyo hayo mengine yapuuzeni tu."
Malale aliyeipandisha klabu hiyo Ligi Kuu Bara msimu huu inaelezwa yuko kwenye mipango ya kuinoa Mtibwa Sugar ambayo ilitangaza rasmi kuachana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Salum Mayanga.