Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maafande wa JKT vs Magereza hakuna mbabe

Maafande JKT Maafande wa JKT vs Magereza hakuna mbabe

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Pamoja na kutangulia kupata bao dakika ya 43, JKT Tanzania imeendeleza rekodi ya kutopata pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine jijini hapa baada ya leo kuambulia sare ya 1-1.

Matokeo hayo yanazifanya timu hizo kubaki nafasi zao, ikiwa Prisons nafasi ya 13 kwa pointi tano, huku JKT Tanzania wakiwa ya saba kwa alama nane baada ya kucheza mechi sita kila upande.

Huu ilikuwa mchezo wa tano kukutana timu hizo ambapo Prisons imeshinda mitatu, sare moja na kupoteza mmoja ugenini, huku ikitakata nyumbani dhidi ya wapinzani hao.

Katika mchezo wa leo, timu zote zilionesha soka safi, ambapo dakika 45 za kwanza JKT Tanzania walionesha kutawala mechi hiyo na kupata bao baada ya beki na Nahodha wa Prisons Salum Kimenya kujifunga akiokoa pasi ya David Bryson na kudumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili wenyeji walionekana kutulia huku kocha mkuu, Fred Felix 'Minziro' akifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mess Roland na Joshua Nyatin na kuingia Mambote Assis na Zabona Khamis ambao waliweza kuamsha morali ya timu na kuituliza.

Mabadiliko hayo yaliipa matunda timu hiyo na kuweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Jeremia Juma dakika ya 69 na kuihakikisha alama moja.

Kocha mkuu wa Prisons, Minziro amesema pamoja na kuruhusu bao la mapema ikiwa ni muendelezo kwao lakini leo vijana wake wamepambana na wametekeleza alichowaelekeza.

"Tulifanya makosa kidogo kipindi cha kwanza mabeki wakakosa umakini tukafungwa bao, lakini tulirejea vyema na kuweza kurekebisha na kusawazisha, kiujumla wachezaji wangu wamefanya vizuri na wanabadilika kila mara" amesema Minziro.

Kocha msaidizi wa JKT Tanzania, George Mketo amesema pamoja na hesabu zao zilivyokuwa kuondoka na ushindi lakini wapinzani wameweza kutibua mipango baada ya kushtukia mbinu zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live