Rafiki yangu mmoja, kiongozi wa Simba ambaye ana dhamana kubwa ya kuiongoza timu hiyo, msimu uliopita aliendelea kunisisitizia kitu alichokuwa ananiambia mara nyingi. Kwamba Fiston Mayele alikuwa mshambuliaji wa kawaida tu, ila Yanga walikuwa wanafanya namna kupata mabao yake.
Nilibaki nacheka. Rafiki mwingine akanisisitizia Kocha wa Yanga, Nasriddine Nabi alikuwa hana ubora wowote kama kocha. Nilibaki nacheka. Kuna nyakati za kuongea kama masihara na kuna wakati wa kuongea kama utani.
Kuna rafiki yangu mwingine aliwahi kusema ‘wangemfukuza’ Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said katika mpira baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Yanga katika uchaguzi ambao ulimuingiza madarakani takribani miaka miwili iliyopita.
Majuzi Simba imefungwa mabao 5-1 na watani zao nimekumbuka mengi. Nadhani lilikuwa hitimisho tu la anguko lao dhidi ya watani. Kipimo cha maendeleo ya Simba sio Yanga, lakini unahitaji kuangalia kwa makini mwenendo wa mtani wako kwa ajili ya kujijenga na kesho iliyo salama zaidi.
Simba waliidharau Yanga wakati inajijenga. Simba walilewa na utawala wao wa miaka ya karibuni. Simba walimdharau Hersi wakaidharau na Yanga wakati ikiendelea kujitafuta.
Simba walibeza hata Yanga kufika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika. Ule wa madaraka ni mtamu. Simba walikuwa katika madaraka ya soka nchi hii kwa miaka minne mfululizo wakasahau na kuidharau Yanga.
Leo Simba amefungwa mabao matano na Yanga na anasakwa mchawi. Mtu wa kwanza kutolewa kafara ni kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Ameshaondoka. Amekwenda kwao.
Ikadaiwa kwamba kuna wachezaji wanashutumiwa kuhujumu mechi. Kama unaamini kuna wachezaji wamehujumu mechi kwa nini umfukuze kocha?
Hapo hapo Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu naye anashutumiwa kwa kuhusika na kipigo. Swali, kipigo kilitokana na Robertinho, wachezaji au Mangungu?
Nadhani huku ni kuweweseka. Ukweli ni kipigo kikubwa walichopewa Simba na Yanga kilikuwa njiani. Lilikuwa suala la muda tu kwa namna ambavyo ungetazama timu zote mbili zilivyokuwa zinachezwa. Simba wamefungwa na moja kati ya timu bora zaidi kwa sasa ukanda huu.
Pengo lilianza kuonekana katika miaka ya karibuni wakati Yanga wamechukua ubingwa mara mbili mfululizo. Pengo likaonekana zaidi pale Tanga wakati Simba walipojifariji kwa mikwaju ya penalti na kutwaa ngao ya jamii dhidi ya Yanga katika pambano ambalo Yanga alitawala kwa muda mrefu wa mchezo.
Kama vile haitoshi, Yanga alicheza mpira mkubwa dhidi ya Azam huku Simba akikaliwa kooni na Singida. Hapo hapo kumbuka Yanga walikuwa wameweka kambi Kigamboni huku Simba wakitokea Uturuki na Azam wakitokea Tunisia. Ilikuwa ni kiashiria tosha kuelekea msimu mpya.
Baada ya hapo Yanga wakawa wa moto wakishinda mabao mengi mwanzoni mwa ligi hadi walipojikwaa tena dhidi ya Ihefu.
Simba walikuwa wanashinda huku zikitoka kauli ambazo hatujazizoea kutoka kwa mashabiki na viongozi wa Simba. Kwamba wao kitu muhimu ni pointi tatu tu sio lazima soka safi.
Kilichotokea wikiendi iliyopita kilikuwa wazi. Ni vile tu tunajitoa fahamu lakini tofauti ya Simba imeanza kwa mambo mawili makubwa katika misimu ya karibuni. Kwanza kabisa Simba wameendelea kukosea kusajili. Kwa miaka ya karibuni wanaweka wachezaji ambao wanajaza tu nafasi sio kwenda kugombania nafasi na kushusha umuhimu wa kina Clatous Chama kikosini.
Alichokisema Robertinho wakati anaondoka ndicho ambacho nilikizungumzia hivi karibuni. Hadi sasa wachezaji wawili waliojipatia nafasi katika kikosi cha kwanza ni Fabrice Ngoma na Fondoh Che Malone. Pambano dhidi ya Yanga alilalamika alipotoka uwanjani, Kibu Denis mambo yalianza kwenda kombo.
Wakati Robertinho akimlalamikia mchezaji ambaye alikuwepo tangu msimu uliopita kumbuka kwamba Yanga imeachana na Mayele, Yannick Bangala, Fei Toto na Djuma Shaban lakini wameendelea kuwa moto.
Kwa nini? Kwa sababu hawakosei sana katika usajili. Injinia anakosea kidogo halafu anapatia sana. Katika miaka ya karibuni Simba wanapatia kidogo halafu wanakosea sana.
Inachosha kurudia lakini Yanga ina wachezaji wengi wanaocheza kikosi cha kwanza kuliko Simba. Ina wachezaji wengi wazuri wanaoanza na wale wanaokaa katika benchi. Simba ina wachezaji wazuri wanaoanza tu wakati benchi halina kitu.
Miaka ya karibuni Simba imesajili wachezaji wengi ambao hawana viwango vya kuchezea Simba au ni majeruhi. Viongozi hawafanyi kazi zao sawa sawa linapokuja suala la usajili wa wachezaji na kijana mdogo waliyemdharau, Injinia Hersi amekuwa akiifanya kazi yake kwa uhakika.
Usajili tu kwa Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na Nickson Kibabage umewatia nguvu kwa kiasi kikubwa. Hapo hapo wachezaji wengine wamekuwa wakiimarika kila kukicha. Kina Clement Mzize.
Ndani ya uwanja kichapo cha Simba kilikuwa kinakuja kwa sababu mbalimbali, lakini zaidi kimchezo Yanga wanacheza mpira wa kisasa.
Kitu cha kwanza ni kwamba timu nyingi bora kwa sasa ni zile ambazo zinakuwa nzuri wakati hazina mpira.
Yanga wanakaba wote kwa ustadi na wanautaka mpira wao wakiupoteza au wakati hawana.
Hii inatokana na ukweli kwamba wana pumzi ya kutosha. Timu kadhaa zilishafungwa mabao matano na Yanga na ukiangalia ni kwamba zinachoka zaidi katika kipindi cha pili.
Mabao mengi ambayo Yanga wanafunga pindi wanaposhinda mabao mengi huwa wanayafunga katika kipindi cha pili.
Unapokosa nidhamu wanakuadhibu. Kwa sababu za kisoka, Simba waliishiwa pumzi katika kipindi cha pili wakaanza kukaba kwa macho zaidi.
Walijaribu kupishana na Yanga huku pumzi zao zikiwa chini. Yanga walikuwa bora wakati hawana mpira na pindi ambapo wangeupata walikuwa na kasi ya kuelekea katika lango la Simba.
Haya ni ya ndani ya uwanja lakini kote kote, ndani na nje ya uwanja, rafiki zangu wa Simba wamekuwa wakiwadharau Yanga na kuhisi kama vile wanafanya ujanja ujanja katika mafanikio yao.
Kama watakuwa wameshtuka itakuwa vizuri lakini wakiendelea kulala usingizi wa pono basi pengo baina yao na Yanga litaendelea kuwa kubwa.
Unapoona Mayele anakuwa mfungaji bora wa Shirikisho na bado unaamini kwamba mabao yake ni ya kununua unahitaji kupisha mawazo mapya ya uongozi.
Leo hayupo lakini Yanga wanafunga zaidi lazima ufahamu kwamba kuna nyakati zinakuacha. Umechoka kufikiri.
Madikteta wengi duniani huwa wanaanguka kwa sababu ya kuendelea kuamini wana nguvu kubwa.
Hawataki kuona kuimarika kwa fikra kwa watu wengine. Hadi siku unayopoteza nguvu kabisa unashtuka na kujikuta umechelewa.
Maadui wa Simba ni marafiki zangu wa karibu ambao nakunywa nao chai mjini na nikisoma mawazo yao tu dhidi ya watani zao nagundua wataendelea kuachwa mbali kama hawataamini kuwa wanafanya makosa huku wakiamini Yanga inasonga mbele kijanjajanja tu.