Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maabad: Washambuliaji tunapitia magumu, tusipofunga tunabezwa

Maabad Pic Data Straika wa Coastal Union, Maabad Maulid

Sat, 12 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Straika wa Coastal Union, Maabad Maulid amesema washambuliaji hupitia kipindi kigumu pale wanaposhindwa kufunga mabao na kuwafanya kubezwa bila kupewa moyo akielezea kuwa baada ya kufunga bao kwenye mechi iliyopita imepunguza presha kwake.

Nyota huyo alifunga bao lake la kwanza msimu huu tangu alipojiunga na Coastal Union akitokea KVZ ya Zanzibar alipoibuka mfungaji bora wa ligi kuu Zanzibar alipotupia mabao 15.

Akizungumza jijini hapa, Maulid amesema washambuliaji hupitia kipindi kigumu haswa wanaposhindwa kufunga mabao na kuwafanya wadau na mashabiki kubeza bila kuwapa moyo.

Amesema baada ya kupitia kipindi kigumu kwa kucheza mechi saba bila kufunga bao, juzi presha ilipungua baada ya kuondoa gundu huku akiahidi makubwa zaidi kwenye mwendelezo wa ligi.

"Tunapitia kipindi kigumu sana na cha kujutia sisi washambuliaji tunapokosa kufunga mabao, ni wachache sana wanaoweza kukupa moyo lakini wengi huwa wanabeza nashukuru kwa bao la juzi dhidi ya Prisons limenipa morari na kujiamini" amesema Maulid.

Amesema anaamini ataendelea kufanya vizuri kuisaidia timu na kwamba kutokana na mabadiliko yaliyopo kikosini wanaona mwanga wa timu kuendelea kuwa kwenye kiwango bora akiwaomba wenzake kikosini kupambana.

Amekiri ugumu wa ligi ya Tanzania kuilinganisha na Zanzibar akifafanua kuwa soka la hapa nchini ni nguvu zaidi na ushindani na kwamba kadri siku zinavyosogea anaendelea kulielewa na kwenda sambamba na wachezaji wenzake.

"Soka la Tanzania lina ushindani mkubwa na linahitaji kucheza kinguvu, lakini nashukuru kuna mabadiliko mazuri kadri tunavyoendelea kucheza naamini tutafanya vizuri" amesema nyota huyo.

Chanzo: Mwanaspoti