Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MODRIC: Fundi mwenye mihela, anayezeeka na utamu

Modric Pic Luka Modric

Tue, 13 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Dunia ilipata mshtuko sana wiki iliyopita baada ya kushuhudia timu iliyopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Kombe la Dunia, Brazil ikiangukia pua mbele ya Croatia na kushindwa kusonga hatua ya nusu fainali baada ya kupoteza mechi kwa mikwaju ya penalti.

Pale Croatia kuna mmoja kati ya mastaa ambao ndio wanaonekana kuibeba sana timu ukiachana na damu changa zinazokimbiza kinoma, huyu anaitwa Luka Modric, mmoja kati ya mastaa waliofanya kazi kubwa kwe-nye michuano ya Kombe la Dunia kule Urusi na hata sasa huko Qatar.

Vijana wanasema anazeeka na utamu wake, lakini sio tu utamu wa kusakata kabumbu ambao anazeeka nao, staa huyu pia anazeeka na utajiri wake, kivipi? twende sawa.

ANAPIGAJE PESA

Chanzo chake cha pesa zaidi ni mpira wa miguu ambao anakunja pesa kupitia usajili wake sambamba na mshahara anaokunja kila wiki.

Tovuti mbalimbali zinaeleza kuwa Luka ndio mchezaji tajiri zaidi kwa sasa nchini Croatia akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 75 milioni na mshahara wake kwa wiki ni Euro 378,654 na kwa mwaka ni Euro 19.69 milioni.

Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi staa huyu anaripotiwa kuwa alipata zaidi ya Pauni 4 milioni kama pesa ya usajili kwa kuongeza mkataba.

Jamaa anapata mpunga wa kutosha pia kupitia madili mengine ya nje ya uwanja ambako ana mkataba wa ubalozi na kampuni ya Nike Sofa Score, Oly Bet, Russell Brown na MAX TV ambazo zote zinamuingizia kiasi kisichopungua Pauni 10 milioni kwa mwaka.

NDINGA

Anapenda sana kuendesha magari ya kifahari lakini ndinga nyingi alizonazo ni kutoka kampuni ya Audi Q7 na anamiliki matoleo yote mapya ya kila mwaka yanayotolewa na kampuni hiyo kuanzia mwaka 2016, 2017, 2019, 2020 na 2021. Vilevile ana Bentley Continental GT, thamani ya ndinga zote alizonazo inakadiriwa kufika Dola 800,000 ambazo ni zaidi ya Sh1.6 bilioni za Kitanzania.

MSAADA KWA JAMII

Kila mwaka anaripotiwa kutoa zaidi ya Pauni 500,000 kwa ajili ya kusaidia taasisi za Arthur Rank Hospice Charity sambamba na kampeni ya kupambana na kansa iitwayo Beat Up Cancer.

MJENGO

Mwaka 2019, alinunua nyumba ya kirahari huko jijini Madrid kwa Euro 12 milioni, ukubwa wa eneo ambalo nyumba hiyo ipo ni zaidi ya mita 10,000 na nyumba yenyewe ina ukubwa wa mita 2,700.

Ina nyumba tisa, ukumbi wa sinema wenye viti 18, pia kuna baa kwa ajili ya kujivinjari.

Kuna chumba maalumu kwa ajili ya watoto wake kucheza, bwawa la kuogelea na viwanja vya michezo mbali mbali.

MAISHA BINAFSI

Jamaa sio mtu wa kujirusha, inadaiwa kuwa anajali sana familia yake ndio maana hata akanunua nyumba ambayo ina kila kitu ndani kwa sababu hapendi sana kutembea na kuchangamana na watu.

Muda mwingi anapokuwa hayupo kwenye majukumu ya kimpira hupendelea sana kulala na kucheza soka kwenye viwanja vilivyo ndani ya nyumba yake.

Kwa sasa yupo kwenye ndoa na mrembo Vanja Bosnic ambaye amezaa naye watoto watatu.

Chanzo: Mwanaspoti