Hatma ya beki wa Cameroon, Che Malone Fondoh Junior ipo mikononi mwa Rais wa Heshima wa wa Simba, Mohamed 'MO' Dewji.
Simba inamtaka beki huyo, ambaye anacheza timu ya Taifa Cameroon na klabu ya Cotonsport kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chao hasa katika mashindano ya kimataifa.
Habari kutoka nchini Cameroon zinadai kuwa Malone anatarajia kukutana na tajiri Mo kwa lengo la kufanya mazungumzo kuona ni namna gani anaweza kumchomoa kwenye kikosi cha Cotonsports.
Awali, Coton ilickataa ofa ya Simba ya Dola 40,000 (Sh96.9 milioni) kwa ajili ya kumnunua mchezaji huyo, huku ikidai thamani ya mchezaji huyo ni Dola 100,000, ambazo ni sawa na Sh242.2 milioni.
Meneja wa mchezaji huyo anayetambulika kwa jina la Tamanji Lawrence anatarajia kukutana na Mo iwe hapa Tanzania au Dubai, ambako bosi huyo anaishi kwa lengo la kuzungumza dili hilo.
"Kikao hicho ndiyo kitaamua hatma ya mchezaji kama atakuja Simba au la," ilieleza taarifa hiyo kutoka Cameroon.
Wakati huo huo, Malone anatajwa kuwindwa na klabu mbili za Ulaya ikiwemo FC Zurich ya Uswisi na Paris FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Ufaransa.
Malone alijiunga na Cotonsport misimu miwili iliyopita na kucheza michezo 68, akiwa na timu hiyo akishinda mataji mawili ya Ligi Kuu na Kombe moja la FA.
Simba bado ina nafasi ya kumsajili beki huyo kitasa kama tu tajiri Mo atamua kuvunja benki ili kumshusha mitaa ya Msimbazi.
Hadi sasa, eneo la beki wa kati kwenye kikosi cha Simba yupo Henock Inonga, Joash Onyango na Kennedy Juma, huku ikiachana na Erasto Nyoni, ambaye alikuwa akitumika popote anapohitajika.
Simba inaripotiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka katika Ligi Kuu ya Rwanda, ā€ˇWilly Onana, ambaye pia ameibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa msimu.
Onana ameibuka na tuzo hiyo baada ya kufanya vizuri msimu uliopita akiwa na Rayon Sport kwa kufunga mabao 16, wakati timu hiyo ikitwaa ubingwa wa ligi nchini humo msimu uliomalizika.