Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MKWAMBI: KWA SIMBA HII, YANGA ITASUBIRI SANA

Mkwambi Pic Data MKWAMBI: KWA SIMBA HII, YANGA ITASUBIRI SANA

Sun, 11 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KATIKA utawala wa bodi ya Simba hakuna bosi aliyewahi kuitingisha klabu hiyo kama Swedy Mkwabi ambaye alisababisha mvutano mkubwa kisha akaamua kujiweka kando kwa kujiuzulu.

Baada ya kujiuzulu alikaa kimya na hakuwahi kufunguka lolote juu ya uamizi wa kuondoka na Mwanaspoti lilimfungia safari hadi jijini Tanga na kufanya naye mahojiano, ambapo alifunguka mengi. Fuatana nasi.

ALIPOANZIA KATIKA SOKA

Mkwabi anaeleza kuwa anatokea katika familia ya soka ambapo baba alikuwa mchezaji wa Simba (enzi hizo Sunderland) na Taifa Stars, na aliwahi kuwa kiongozi wa klabu hiyo, hivyo alijikuta anafuata mkondo.

“Nimerithi kuipenda Simba kutoka kwa baba kwa sababu nakua namuona yupo kwenye mpira. Huo ndio mwanzo kuwa kwenye soka,” anasema.

Related Faida za Chama, Miquissone kutamba Afrika SHAURI LA MWAKALEBELA PICHA PANA Yanayotokea Simba, Namungo sababu ni hii tuUONGOZI

Mkwabi anasema alianza uongozi Simba akiwa na kati ya miaka 29 na 30 kama mjumbe wa kamati utendaji aliyoitumikia kwa miaka minne na walifanya mengi chini ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage.

“Nakumbuka chini ya Rage tuliweza kununua uwanja ambao Simba inafanyia mazoezi sasa, tulianzisha Simba Tv kwa kushirikiana na katibu kipindi hicho alikuwa Evodius Mtawala na mwandishi Shafii Dauda ambacho kwa sasa Azam inailipa Simba pesa nyingi tu, lakini pia tulikuwa tunafanya mikutano yote minne ya matumizi na mapato, nje na hapo tuliweka dira nzuri ya mabadiliko haya ya sasa.”

KUJIUZULU KWAKE

Baadaye anasema Mkwabi aligombea umakamu wa rais kati ya mwaka 2014 na 2018 kura hazikutosha, hivyo akaendelea kubaki kama mwanachama na kiongozi mstaafu. Uchaguzi uliofuata aligombea uenyekiti akashinda. Hata hivyo akajiweka pembeni kwa manufaa ya Simba.

“Niliamua kuondoka kwa ajili ya manufaa ya Simba, katika uongozi ukiona vitu haviendi sawa ni vyema ukajiweka kando, mimi Mkwabi ni mtu mdogo ndani ya timu, sikuona sawa wakati naipigania klabu wengine wakiona naleta ugomvi, nikaamua niondoke kwa manufaa ya klabu ili nipishe mambo mengine yaendelee, kwani kulikuwa na taratibu za Simba ambazo zilikuwa hazijaenda sawa,” anasema.

“Binafsi sina tatizo na Mo Dewji, naamini hata yeye hana tatizo na mimi ni mwanachama mwenzake, lakini pia ni kiongozi wangu. Baada ya kujiengua bado nitabakia kuwa mwanachama wa kawaida na kama uongozi ukiona kuna jambo naweza kusaidia nitasaidia, ila kurudi kwenye uongozi sijafikiria kabisa.”

Anasema alijiuzulu Simba tangu Juni, lakini viongozi wa Simba walitangaza Septemba baada ya kuwatumia ujumbe wa kuwakumbusha kuliweka wazi jambo hilo.

“Mlijua mwezi wa tisa, ila nilijiuzulu mwezi wa sita baada ya kuwatumia uongozi ujumbe kwamba mmekaa muda mrefu bila kutangaza, ndipo wakatangaza, lakini nilikuwa nimeishawaambia baadhi ya viongozi wa matawi kwamba naondoka kwa manufaa ya Simba,”anasema.

SIMBA CAF

Mkwabi anasema Simba imeimarika kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na anaamini ikiendelea kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo ndani ya miaka mitano inaweza ikachukua ubingwa wa Afrika.

“Kikosi chetu cha Simba kimeimarika sana, kina wachezaji wenye ubora, ukiangalia wale wanaoanza na wanaokuwa benchi wana tofauti ndogo sana kiasi kwamba akiingia unaona anaweza akafanya mabadiliko ya mchezo, timu inafunga na kucheza mpira mzuri, binafsi nilitabiri kwamba Simba ya msimu huu inaingia robo fainali ya michuano hiyo,” anasema.

Mbali na michuano ya CAF anazungumzia Ligi Kuu Bara akisema imekua kutokana na Azam TV kuionyesha, lakini pia kila timu inayoshiriki inapambana na kwamba Afrika Mashariki, Tanzania inaonekana ndio ina ligi bora zaidi. “Simba na Yanga hazipati matokeo kirahisi zinapokutana na timu za mikoani, huo ndio ubora wenyewe wa ligi hata anapotoka mwakilishi wa CAF anafanya vizuri na ndio maana Namungo imefanya vizuri kwa mara ya kwanza kucheza michuano hiyo.”

TOFAUTI SIMBA NA YANGA

Kuhusu timu za Simba na Yanga, Mkwabi anasema: “Siwezi kuiongelea sana Yanga kwa sababu sio timu yangu, lakini msimu huu ukiacha kukamiana baina ya timu hizi kongwe zinapokutana katika mchezo wa watani wa jadi, Simba ina kikosi kipana, ina uwekezaji mzuri wa wachezaji wa viwango na kama Yanga ikiendelea kuwa na kikosi kama hiki hata msimu unaokuja bado haitachukua ubingwa hadi watakaposajili wachezaji wenye uwezo wa kuendana nao,” anasema.

ISHU YANGA UONGOZI

Mkwabi anatoa mtazamo wake changamoto anayoiona Yanga kwamba viongozi wengi ni wachanga, huku akimtolea mfano makamu mwenyekiti ambaye amefungiwa na TFF, Fredrick Mwakalebela.

“Nipo tayari kukoselewa, lakini naona viongozi wa Yanga kuna uchanga, mfano Mwakalebela aliongoza TFF lakini ni tofauti na kuongoza Simba na Yanga. Ameonyesha upungufu mwingi akiwa Yanga. Kuna vitu vinafanyika lakini sioni vikitoa matunda uwanjani. Misingi ya Yanga sijaona ikitendeka kama ilivyozoeleka, pia wanaowasajilia wachezaji nawatilia shaka.

“Yanga ikiwa bora na Simba bora tunakuwa tunapata timu ya taifa iliyo bora. Ni kitu ambacho kitafaa zaidi lakini ukiangalia kikosi cha Yanga kina tofauti kubwa kuweza kushindana na Simba hii. Kifupi Yanga wana changamoto nyingi ambazo lazima watulie kuweza kurudia ubora wao ili hizi timu kubwa ziwe chachu ya kukua kwa timu ndogo.”

UENYEKITI SIMBA

Kuhusu uenyekiti ndani ya Simba, Mkwabi anasema: “Simba nafasi ya uenyekiti haina nguvu, mwenye nguvu ni bodi, hivyo mwenyekiti aliyeingia sioni kama atakuwa na kitu cha kubadilisha sana badala ya kuwa msikilizaji na kuchangia mawazo yake. Anatakiwa kushirikiana na wenzake. Nilikuwa mjumbe wa bodi kama wajumbe wengine. Simba inaendeshwa na bodi. Hata katiba ya Simba mwenyekiti anachagua wajumbe wawili na kusimamia mkutano,” anasema.

Mkwabi anasema baada ya kuachia uenyekiti Simba, maisha yake yalikuwa Tanga muda mwingi kutokana na kuwa kiongozi wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Soka Tanga Mjini, lakini pia anafanya biashara zake zilizopo Tanga na Dar.

“Mwanzoni nilikuwa Tanga sana, lakini kwa sasa nipo jijini Dar es Salaam, kwa sababu nina biashara Tanga na Dar es Salaam ingawa muda mwingi nipo sana Tanga. Nashukuru Mungu naendelea vyema na majukumu yangu nikipata nafasi nikiwa Dar es Salaam huwa nakuja viwanjani kuangalia timu yangu ya Simba na wanachama wenzangu.”

Kuhusu maendeleo ya soka Tanga anaeleza kuna timu zaidi ya 50 akiona ndio wilaya inayoongoza kwa kuwa na timu nyingi Tanzania.

“Kipa namba tatu wa Simba, Salimu Juma, Mahadhi, Gadiel Michael wametoka kwenye ligi ya Wilaya ya Tanga. Kuna vijana wengi, licha ya kuonekana levo ipo chini kutokana kutokuwepo na sapoti yoyote, viongozi tunatakiwa kuingia mfukoni. Kuna wakati nilitoa jezi za timu 50 ili kuziunga mkono timu za mkoa huu,” anasema.

ACHOMOA BEKI YANGA

Mbali na hilo, Mkwabi anazungumzia tukio la usajili wa Gadiel kutoka Yanga kwenda Simba kwamba, vita ilianzia Misri kumshawishi hadi kufanikiwa saini yake.

“Gadiel asingesaini Simba bila juhudi zangu, nakumbuka tukiwa Misri niliona juhudi za Yanga kutaka kumalizana naye, lakini nikagundua walikuwa wanazungumza kwa makosa ya kiutendaji, nikajipanga na wenzangu nikafanikiwa kumshawishi kulekule tukamalizana kimyakimya,” anasema.

“Mwisho ikawa imebaki kumalizana tu kwa hatua ya mwisho aliporudi jijini Dar es Salaam, nilisimamia kuhakikisha hatui Tanzania akiwa mikononi mwa watu wa Yanga na hatua hiyo ikafanikiwa na sasa yupo kwetu akitusaidia.”

“Lakini tukio ambalo kwangu ni faraja kuwa mwanzilishi wa Simba Tv kitu ambacho kinaipa klabu pesa. Ni ubunifu, una faida kwa Simba. Tukio lingine ni ile mechi ya Simba na Yanga sare ya mabao 3-3, ilikuwa mechi bora, ilianza kwa huzuni ikamalizika kwa furaha, nyingine mechi ni dhidi ya Nkana tuliyoingia hatua ya makundi,” anasema.

Mkwabi anasema soka linatakiwa kuanza na misingi ya chini. Pia kuwepo makocha wenye taaluma sahihi kwenye vituo na uwekezaji huo unafanyika kuwajengea wachezaji tabia ya kujitambua.

“Nadhani tunakuwa tunakurupuka bila kuwa na misingi mizuri ya kuandaa wachezaji, ndio maana wanakuja juu na kushuka ghafla.

USHAURI MO DEWJI

Anasema ikitokea akapata nafasi ya kumshauri Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ atamwambiaje?

“Sitakuwa na maneno mengi kwa MO Dewji zaidi ya kumwambia Wanasimba wanampenda, hilo ashukuru. Lakini hapohapo anatakiwa kufanya jambo moja tu - kuitendea haki Simba, watu wakikuamini uwalipe wema ili kesho wakukumbuke kwa mazuri.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz