Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MEDDIE KAGERE: Sijakata tamaa, nitacheza tu

Kagere+pic MEDDIE KAGERE: Sijakata tamaa, nitacheza tu

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MSIMU wa 2018/19, Simba iliweka rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo ambayo tulitolewa na miamba ya soka la Afrika, TP Mazembe.

Msimu huu tulikuwa na matokeo bora zaidi tukicheza mechi za nyumbani na michezo yote tulishindwa kuwafunga Mazembe mechi ya kwanza ya robo fainali.

Hatukuwa na matokeo mazuri katika michezo ya ugenini hasa hatua ya makundi ambayo tulipoteza yote lakini tulifanikiwa kuweka rekodi kama klabu ambayo ilikwenda kuleta faida kwa nchi.

Miongoni mwa faida kama nchi ambazo zilipatikana tulipata nafasi ya kupeleka timu nne kwenye mashindano hayo ya kimataifa, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho Afrika.

Mafanikio hayo hayakuishia hapo tu bali yalifika mpaka kwangu kwani nilifanikiwa kumaliza nafasi ya pili nyuma ya mfungaji bora wa mashindano ambaye alikuwa na mabao saba.

Nakumbuka msimu huo nilifunga mabao sita huku timu yangu ikiondolewa robo fainali ambayo tulicheza mechi mbili dhidi ya Mazembe ambazo zote sikufunga bao.

Katika mechi ya kwanza ambayo tulicheza kwa Mkapa iliyomalizika kwa suluhu nilikosa nafasi za kufunga ikiwemo ile tikitaka ambayo ilikwenda kugonga mwamba.

Pengine kama ningefanikiwa kufunga bao lolote katika mechi hizo ningekuwa na idadi sawa na mfungaji bora na kwa vile timu yangu ilifika mbali ningeweza kutwaa tuzo hiyo au tungegawana.

Kama ingekuwa hivyo yangekuwa mafanikio makubwa ya klabu pamoja na kwangu kuchukua tuzo kubwa ya Afrika kama kinara wa ufungaji na ningefanya hivyo mara mbili kwani nilichukua tuzo hiyo kwa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara nikimaliza na mabao 23.

Msimu uliofuata tuliondolewa hatua ya awali dhidi ya UD Songo ambapo wenzetu walikuwa tayari katika hali ya kushindana kuliko sisi ambao tulikuwa tunatoka kwenye maandalizi ya msimu.

Msimu huu mambo yamekuwa tofauti kwangu ingawa kwa upande wa timu naona tunaweza kufikia rekodi ambayo klabu iliifikia lakini tunaweza kuvuka au kuweka nyingine mpya.

Bahati mbaya ni kwangu ambaye wakati msimu timu inafikia mafanikio makubwa kama haya nami nilikuwa na idadi ya mabao sita ambayo wakati huu sijafunga hata moja.

Rekodi ambayo inanizunguka katika kichwa changu kwani mpaka sasa Simba imecheza mechi nane na inakaribia kufikia hatua ya mafanikio kama ya misimu miwili nyuma kwangu bado si shwari.

Kimsingi sijakata tamaa kama sitaweza kufikia idadi ya mabao kama hayo kwani nafahamu changamoto ambayo inanikabili mpaka kufikia huko ambapo nilifika awali.

Wakati nafunga mabao sita na kuwa nafasi ya pili nyuma ya mfungaji bora nilikuwa nacheza mara kwa mara kikosi cha kwanza na muda mwingine dakika zote 90 nilikuwa namaliza.

Lakini wakati huu mambo yamekuwa tofauti kwangu kwani nimecheza mechi chache katika mashindano haya na muda mwingine kuna michezo mingine sikutumika kabisa.

Inakuwa ngumu kwangu kucheza kwa muda mchache tena ambao timu inakuwa na malengo ya kulinda matokeo ambayo wameyapata au kuna presha fulani inabidi nitumike kwa aina hiyo.

Kutokucheza kwangi si kama nipo vibaya au nimeshuka kiwango, jambo hilo si la kweli kwani naamini kulingana na mfumo pamoja na mahitaji ambayo kocha anayataka ameamua kumtumia mwingine.

Nakumbuka hata wakati ambao nacheza kulikuwa kuna wengine wanakaa nje kwa ajili yangu hawakuwa wabaya bali mahitaji ya kocha yalikuwa kwa aina ya uchezaji wangu.

Sina shida yoyote na wala sijakata tamaa naamini nitacheza na nitaweza kufunga kama ilivyokuwa katika ligi nimecheza mechi chache lakini naongoza msimamo wa wafungaji.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz