Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MBONA IKO HIVI: Simba ilivyopindua meza Zambia 1979

Simba.jpeg MBONA IKO HIVI: Simba ilivyopindua meza Zambia 1979

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

NINI hasa ilikuwa siri nyuma ya ushindi wa mabao 5-0 ambayo Simba ilipata nchini Zambia mwaka 1979 dhidi ya Mufulira Wanderers baada ya kuwa imefungwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza hapa nchini?

Hilo ni swali ambalo wengi wamekuwa wakijiuliza hasa katika kuelekea pambano la leo la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo imeifunga Simba mabao 4-0 kwenye mechi ya kwanza.

Na kama ilivyokuwa mwaka 1979, mashabiki hawaelewi timu yao ilifungwaje magoli yote manne jijini Johannesburg wakati ikiwa imetawala mechi kwa kiwango kikubwa.

Waliohudhuria pambano la mwaka 1979 - wanasema sio kwamba Simba ilizidiwa sana. Ni makosa ambayo yalifanyika ndani na nje ya uwanja yaliyosababisha kipigo hicho kikubwa.

Stori zenye miaka 40 nyuma yake, ni muhimu kufanywa kwa kuzingatia kwamba mengine hupotea. Mmoja wa watu wa mwanzo kumhoji alikuwa ni jirani yangu Mzee Shaabani mwenye umri wa zaidi ya miaka 75 na shabiki kindakindaki wa Wekundu wa Msimbazi.

Niliacha sehemu kubwa ya masimulizi yake kwa sababu katika mazungumzo yake ya mwanzoni kabisa, aliniambia aliyekuwa ikipa wa Simba kwenye mechi ya Zambia alikuwa Hassan Mlapakolo.

Hadi wakati namhoji mzee huyo, tayari nilishajua golini alikaa Athumani Mambosasa. Kwa hiyo nikajua kwanba kama nataka kujua siri ya ushindi, sitaipata kwa shabiki.

COOKER ALIVYOGEUKA KUKA

Katika mechi zote mbili dhidi ya Mufulira, Abbas Said Mhunzi maarufu kama Abbas Kuka alicheza kama kiungo wa ulinzi. Kwa ambao hawakuwahi kumwona akicheza alikuwa dizaini ya huyu Tadeo Lwanga wa Simba sasa hivi.

Jina la Cooker ni la lugha ya Kiingereza likimaanisha mpishi. Kuka alipewa jina hilo na washabiki wa Simba kutokana na uwezo wake wa kutengeneza mambo ya mpira.

Kuka anakumbuka kwamba katika mechi ya kwanza, kikosi cha Simba kilichoanza kilipangwa ifuatavyo; Athumani Mambosasa, Daudi Salum, Filbert Rubibira, Hussein Tindwa, Kuka, George Kulagwa, Ismail Mwarabu, Abdallah Mwinyimkuu, Thuwein Ally na Ali Hussein.

“Nakumbuka kwamba hatukufanya vizuri kabisa katika mechi ya kwanza. Baada ya kipyenga kupulizwa huku tukiwa tumepigwa nne, hadi mashabiki wetu wenyewe walitununia.

“ Sikumbuki kama tulicheza vibaya sana kwenye ile gemu lakini wenzetu walitumia vizuri karibu nafasi zote walizopata. Kwenye soka, ukipata siku ya namna hiyo ambayo kila anachofanya mwenzako kinakubali, ujue ni siku mdefu hiyo,” anasema Kuka.

Ni muhimu kufahamu kwamba Mufulira pia ndiyo ilikuwa kwenye kilele chake kama mojawapo ya timu bora za Kusini mwa Afrika nyakati zile. Huenda benchi la ufundi la Simba halikuwa hata na mkutano mmoja wa kujadili mazuri na upungufu.

Rubibira ambaye naye alicheza mechi zote mbili, alitaja mambo kadhaa yaliyosababisha Simba iweze kushinda 5-0 na kuwa timu pekee kwenye historia ya Afrika kufanya jambo la namna hiyo.

Jambo la kwanza lilikuwa ni maneno ya kutia faraja kutoka kwa viongozi wa timu na kocha wa wakati huo, Joel Bendera. Pia klabu ilikuwa na Katibu Mkuu aliyeitwa Sanga ambaye naye alikuwa akiwatia moyo.

Maneno ya mara kwa mara ya kuwatia moyo ya Katibu Mkuu na Bendera aliyefariki dunia miaka michache yaliwapa hamasa kubwa wachezaji.

Ili kuondoa presha ya washabiki na vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kuzoea mazingira ya Zambia mapema, Simba iliondoka Tanzania wiki moja kabla ya mechi. “ Tulipofika Zambia ilikuwa ni mazoezi tu. Tulikuwa tunafanya mara moja kwa siku yalikuwa mazoezi makali. Masaa matatu hadi manne ya kujifua.

“ Nadhani Mufulira hawakujiandaa vema na marudiano. Wao waliona mechi kama waliimalizia Dar. Siku moja kabla ya mechi, ndiyo nilipata picha ya kwanini nasema hivi.

“ Simba ilifikia hoteli moja inaitwa Andrew’s pale Lusaka. Usiku wa kuamkia kwenye mechi, tukaona wachezaji na viongozi wa Mufurira nao wamekuja kulala tunapolala sisi.

“ Walipotuona wakawa kama wanatufanyia utani tu wa kutuambia kwanini tumepoteza muda kwenda Zambia. Wakajua wanatupiga nyingi sana. Hawakujua kwamba sisi wiki nzima tulikuwa tunajifua kwa ajili yao,” anasema Rubibira.

Kwa watu niliowahoji, kuna mkanganyiko kuhusu muda ambao magoli yalifungwa. Kuka na Rubibira wote wanakumbuka kwamba Thuwein na Kulagwa ndiyo walifunga magoli yote matano; Thuwein mawili na Kulagwa ambaye mashabiki wakimwita Best kwa kumlinganisha na George Best wa England alifunga mabao mawili.

Hata mzee wa mtaani kwangu amenipa tu taarifa kwamba mechi ile haikutangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania (RTD) na badala yake mashabiki walikuwa wakidokezwa kidogo tu kuhusu matokeo kutoka Zambia. Taarifa inayokubalika na wote ni hii; Thuwein kupiga hatrick na kuweka rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa ya Mtanzania kufunga goli tatu ugenini.

Na kwamba hadi wakati wa mapumziko, Simba tayari ilikuwa inaongoza kwa mabao matatu. Na Rubibira anasema anakumbuka maneno ya mwisho ya Bendera kabla hawajaingia uwanjani siku ile.

Aliwaambia wachezaji kwamba wao wanatakiwa kupata ushindi mdogo tu ili kulinda heshima yao. Lakini, baada ya kuona wanaongoza mabao 3-0 na Uwanja wa Independence ukiwa umepoa mbele ya aliyekuwa Rais wa Zambia wakati ule, Kenneth Kaunda, Bendera akabadilika kwa kuwaambia sasa wanaweza kufunga magoli mengi zaidi na kuitoa Mufulira.

Kwa hiyo, kama Simba wana cha kujifunza leo kwenye mechi yao dhidi ya Kaizer ni kwmba wachezaji wanatakiwa kuaminishwa kwamba mechi bado haijaisha. Pili wafanyishwe mazoezi yanayoendana na mechi yao ya leo. Wataalamu wote wa mpiira waliona kwenye mechi iliyopita kwamba aina ya magoli walofungwa Simba ilikuwa karibu inafanana.

Pamoja na umuhimu wa mazoezi, ilionekana ni muhimu kwa wachezaji kufanya mazoezi yanayoendana na matatizo yaliyojitokeza mwenye mechi ya awali.

Kina Kajole, Thuwein na Kulagwa walikuja kushangaa kuona umati uliokuja kuwalaki Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kama mashujaa.

Wachezaji waliopewa kila aina ya majina ghafla wakageuka mashujaa. Kuka anakumbuka vitu viwili bado; shuti kali la Thuwein lililoipa bao la tano na la kufuzu na mashabiki kulazimisha gari isiendeshwe. Wao walitaka isukumwe tu hadi makao makuu ya klabu yaliyopo Mtaa wa Msimbazi.

IMEANDIKWA NA EZEKIEL KAMWAGA

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz