Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MASK MEN: Wanasoka maarufu walionekana uwanjani na kifaa tiba cha maski

Mask Men MASK MEN: Wanasoka maarufu walionekana uwanjani na kifaa tiba cha maski

Fri, 21 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Supastaa, Kylian Mbappe amepata suluhu ya kuendelea kuwapo kwenye fainali za Euro 2024 na kuonekana uwanjani licha ya kuvunjika pua, ni kucheza mechi zilizobaki akiwa amevaa maski maalumu.

Staa huyo wa kikosi cha Ufaransa, ambacho usiku wa jana Ijumaa kilikuwa na shughuli pevu ya kuikabili Uholanzi kwenye fainali hizo za Euro 2024, alitazamiwa kuonekana uwanjani akiwa na maski usoni yenye rangi ya bendera ya Ufaransa ili kukinga pua yake iliyovunjika.

Mbappe, ambaye alisajili kujiunga na Real Madrid kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi akitokea Paris Saint-Germain, alivunjika pua kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi na Ufaransa ilikipiga na Austria.

Baada ya kuruka juu kuwania mpira wa kichwa na mchezaji Kevin Danso, Mbappe alijikuta kwenye maumivu makali baada ya kujipigiza pua kwenye bega la beki huyo wa Austria.

Kulikuwa na wasiwasi huenda Mbappe asingeonekana tena uwanjani kwenye fainali hizo baada ya kupelekwa hospitali na kuripotiwa amevunjika pua.

Lakini, sasa mambo yamekuwa tofauti, staa huyo juzi Alhamisi alionekana na maski mazoezini, kitu ambacho kilitarajiwa pia kuonekana uwanjani kwenye mchezo wa Euro 2024 usiku wa jana.

Hata hivyo, kulikuwa na wasiwasi wa Mbappe kukumbana na zuio la Uefa kutokana na kuwapo na kanuni zinazotaka, kitu kingine chochote atakachovaa mchezaji wakati wa mechi, basi kinapaswa kushabiana na rangi ya jezi na kampuni iliyotengeneza ifahamike pia.

Kanuni hiyo inasema hivi: “Kifaa chochote cha kitiba (mfano kofia ya kukinga kichwa, maski, kifaa cha goti au kiwiko) kikivaliwa wakati wa mchezo uwanjani, kinapaswa kuwa na rangi moja na kampuni iliyotengeneza inapaswa kufahamika.

“Kwa kifaa kitakachovaliwa miguuni au mikononi basi kinapaswa kufanana na jezi ya timu.”

Kutokana na hilo, kwa kesi ya Mbappe uamuzi wa kucheza na maski katika mchezo wa jana dhidi ya Uholanzi kama atakuwa amepewa nafasi ya kutumika kwenye mechi hiyo, basi maski yake ilipaswa kupewa ruhusa ya Uefa kwanza.

Mbappe baada ya kuumia, alihoji kwenye mtandao wa kijamii ni maski ya aina gani anayopaswa kuvaa, jambo ambalo liliibua komenti za watu mbalimbali wakiwamo mashabiki na wachezaji pia, kabla ya kuonekana akiwa amevaa kwenye mazoezi ya Les Bleus.

Mchezaji Danso, ambaye ndiye aliyegongana na Mbappe na kumsababisha maumivu makali staa huyo wa Ufaransa, amewaomba radhi mashabiki wa Les Bleus kwa kitendo hicho.

Danso aliandika kwenye mtandao wa kijamii: “Kwa mashabiki wa Ufaransa: Nawaomba radhi kwa kitendo cha Kylian Mbappe wakati tunagomea mpira. Namtakia apone haraka na bila shaka atarejea tena uwanjani.”

Hata hivyo, Mbappe hatakuwa mchezaji wa kwanza kuonekana uwanjani kwenye mechi za soka akiwa amevaa maski baada ya kuwapo kwa mastaa wengine kibao waliowahi kucheza na kifaa hicho kutokana na sababu mbalimbali.

Kuanzia kwa mastaa kama Gvardiol hadi kwa mkali za zama hicho, Gazza ni miongoni tu mwa wanasoka waliowahi kuonekana viwanjani kwenye mechi za soka wakicheza wakiwa wamevaa maski.

Josko Gvardiol

Beki huyo wa Manchester City na Croatia, Josko Gvardiol alionekana akiwa amevaa maski kwenye mechi ya raundi ya 16 bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Japan huko Qatar. Beki huyo aliwahi kuumia pua wakati akiichezea RB Leipzig kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya SC Freiburg mwaka 2022 baada ya kugongana na mchezaji mwenzake Willi Orban, hivyo kwenye mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Japan alivaa baada ya kuwa na hofu na kuhisi maumivu.

Son Heung-min

Fowadi wa Korea Kusini na klabu ya Tottenham Hotspur aliumia uso kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Marseille mwaka 2022. Baada ya hapo, mkali huyo alionekana uwanjani akiwa na maski katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA baina ya Spurs na Portsmouth, alipojaribu kujikinga na hatari ya kuumia zaidi baada ya kupata maumivu hayo ya usoni kwenye mechi ya Marseille.

Victor Osimhen

Straika wa Napoli, Victor Osimhen aliumia jicho kwenye mechi ya Serie A baina ya Napoli na Inter Milan mwaka 2021.

Na tangu alipoanza kuvaa maski, supastaa huyo wa kimataifa wa Nigeria hajawahi kuacha, akionekana na maski katika mechi zote anazocheza. Na sasa, Osimhen imekuwa kama kawaida yake kucheza akiwa na kifaa hicho cha kukinga asipate maumivu zaidi kutokana na awali kupata maumivu makali kwenye jicho.

Harry Kane

Straika huyo wa kimataifa ya England kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Bayern Munich ambako alijiunga nayo kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana. Kabla ya hapo, Kane alikuwa anakipiga kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur na alivunjika pua kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Crystal Palace mwaka 2016. Kutokana na hilo, Kane alionekana uwanjani akiwa na maski usoni na hivyo kuwamo kwenye orodha ya wanasoka waliowahi kukipiga uwanjani wakiwa na kifaa hicho.

Diego Costa

Straika huyo wa zamani wa Chelsea, mzaliwa wa Brazil, aliyeamua kuchezea Hispania kwenye soka la kimataifa, Diego Costa alionekana akiwa amevaa maski uwanjani wakati The Blues ilipokipiga na Southampton kwenye mechi ya Ligi Kuu England mwaka 2016. Na kwa kipindi hicho Chelsea ilikuwa na mastaa kibao waliokuwa wakivaa maski kuanzia Pedro, Pierre-Emerick Aubameyang, Petr Cech, Cesar Azpilicueta, Gary Cahill hadi Nemanja Matic. Costa alijiumiza pia aligongana na mchezaji mwenzake, Fikayo Tomori mazoezini.

Cesc Fabregas

Kiungo fundi kabisa wa soka, Cesc Fabregas wakati anakipiga Chelsea alikuwa miongoni mwa wachezaji waliowahi kuvaa maski uwanjani, wakati alipocheza mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya QPR na kufunga bao la ushindi kwenye mchezo huo na The Blues ilishinda 1-0 mwaka 2015. Fabregas alilazimika kuvaa maski hiyo baada ya kuvunjika pua kwenye mechi dhidi ya wagumu Stoke City kwenye mikikimikiki hiyo ya soka la England.

Robert Lewandowski

Mwaka 2015, straika wa Poland, Robert Lewandowski aliumia pua pamoja na taya kwenye mechi dhidi ya klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund kwenye Bundesliga wakati huo alikuwa akikipiga kwa miamba ya soka la Ujerumani, Bayern Munich. Kutokana na maumivu hayo, Lewandowski, anayekipiga Barcelona kwa sasa na yupo huko kwenye Euro 2024 akiwa na timu yake ya Poland alilazimika kucheza na maski ili kujikinga na kupata maumivu zaidi.

Fernando Torres

Wakati anaichezea Chelsea, straika wa Kihispaniola, Fernando Torres akionekana uwanjani akicheza huku amevaa maski katika mechi dhidi ya klabu yake ya zamani ya Liverpool. Hilo lilisababishwa baada ya fowadi huyo wa zamani wa Atletico Madrid kuumia pua wakati akiitumikia Chelsea kwenye mechi ya Europa League dhidi ya Steaua Bucharest mwaka 2013. Katika kujikinga na kupata maumivu mengine kwenye pua, Torres alilazimika kucheza akiwa na maski uwanjani.

Daniele De Rossi

Kiungo wa zamani wa AS Roma, ambaye kwa sasa ndiye kocha wa miamba hiyo ya soka ya Italia, Daniele De Rossi, aliumia na kupata mfupa wake wa kidevu kupata ufa mara mbili, wakati wa mchezo dhidi ya Inter Milan mwaka 2009 na hivyo kumlazimisha kucheza mechi zilizofuatia akiwa amevaa maski ili kujikinga na hali ya kupata maumivu zaidi. Kiungo huyo wa shoka uwanjani enzi zake wakati anakipiga, ameingia kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kuonekana uwanjani kwenye mechi za soka wakiwa na kifaa hicho cha kitabibu.

John Terry

Nahodha wa zamani wa Chelsea, John Terry uliumia mfupa wa kidevu na jambo hilo lilisababisha avae maski kwenye mechi alizotumikia timu yake uwanjani. Na mara ya kwanza alionekana akiwa na maski kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Valencia uwanjani Mestalla.

Terry alilazimika kuvaa maski baada ya kuumizwa na staa wa zamani wa Fulham, Clint Dempsey kwenye moja ya mechi zao huko England.

Paul Gascoigne

Kiungo fundi wa mpira wa zama hizo, Paul Gascoigne maarufu kama Gazza alionekana uwanjani akiwa na maski wakati wa mchezo wa kufuzu fainali za Kombe Dunia 1994 dhidi ya Poland. Mechi hiyo ilifanyika mwaka 1993, ambayo Gazza alicheza akiwa na kifaa hicho tiba kwenye uso wake. Gazza alikuwa ameumia mfupa wa taya baada ya kupigwa kiwiko na nahodha wa Uholanzi, Jan Wouters katika mechi nyingine iliyokuwa ya kufuzu pia kwa fainali hizo za Kombe la Dunia 1994.

Chanzo: Mwanaspoti