Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MASHAKA: Bocco ndiye kanipa mchongo Simba

Valentino Mashaka Simbaaaa.jpeg Valentino Mashaka

Sat, 31 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna vitu vimeanza kubadilika katika maisha ya mshambuliaji wa Simba, Valentino Mashaka tofauti na msimu uliopita alipokuwa anaishi akiwa Geita Gold.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mashaka anasema tangu ajiunge na Simba yapo mambo ameamua kuachana nayo ili kuepusha aibu ya kuchafua taswira ya klabu, ambapo alishapewa mwongozo wa namna anavyotakiwa kuishi.

"Nikiwa Geita Gold haikuwa ajabu kula sehemu yoyote ile, ila huku unaweza ukaenda sehemu ukajiachia ukipigwa picha inaweza ikatafsiriwa vibaya. Ajabu zaidi ukicheza Simba na Yanga ni rahisi kujulikana kwa haraka tofauti na timu nyingine," anasema.

BOCCO ALIMPA TAHADHARI MAPEMA

Mashaka anasema baada ya kupata ofa ya Simba alimpigia simu aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco ili kupata ushauri wake na pia kujua klabu hiyo ina utamaduni upi ambao mchezaji akiufuata ni rahisi kucheza kwa kiwango bora.

Ni mazungumzo yaliyochukua saa tatu kumalizika na anakiri yalimjenga na kukubaliana na ofa ambayo alipewa.

"Jambo la kwanza aliniambia nikiamini kipaji changu, niongeze bidii ya mazoezi kwa sababu hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi, nizingatie nidhamu ndani na nje ya uwanja, niipenda kazi ninayoifanya na kupenda kujifunza kila wakati," anasema.

Anaongeza, "nilimpigia Bocco kutokana na heshima aliyojijengea Simba kabla ya kuondoka kwenda JKT Tanzania. Pia ni mshambuliaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi nilihitaji kujifunza vitu vingi kutoka kwake."

Mwongozo aliopewa na Bocco, Mashaka anakiri unamsaidia kuweka umakini kwa kila anachofanya baada ya kujiunga na Simba, kwani anatambua bado ana safari ndefu katika taaluma yake.

"Nafahamu kwamba Simba, Yanga ni klabu kubwa ni rahisi mchezaji kupata umarufu, ila Bocco alishaniambia nisihangaike na hayo. Badala yake kazi ninayokuwa nafanya uwanjani, iwe inazungumza zaidi," anasema.

KUHUSU KUTUPIA MABAO

Anasema katika mazoezi kocha wa timu hiyo, Fadlu Davis anamsisitiza zaidi kutengeneza mbinyo kwa timu pinzani, kuwapa presha mabeki, mikimbio yake iwe ndani ya 18, kutumia nafasi kwa maana nikipata mpira niwe nimeangalia napiga mashuti ya aina gani.

"Kuhusu kufunga nilianza tukiwa katika maandalizi ya msimu yaliyofanyika nchini Misri, ninachokifanya katika Ligi Kuu ni kama mwendelezo."

Anaongeza: "Napenda kujiongeza na mazoezi binafsi, lakini kocha mara nyingi kuna namna ananielekeza kuhakikisha dakika ninazokuwepo uwanjani nakuwa nafanya kitu, huwa anasema nikipewa dakika 10, 20 ama 90 jambo la msingi nazitumiaje."

Mashaka anayeongoza kwa mabao mawili, anasema anatamani msimu huu ikiwezekana awemo katika orodha wafungaji wanaowania kiatu cha dhahabu, jambo linalompa ari ya kupambana zaidi.

"Simba ina wachezaji wazuri, ushindani ni mkubwa, hivyo dakika anazonipa kocha kucheza nizithamini na kuhakikisha nafanya kinachotakiwa kwa umakini," anasema.

ILIKUWA NDOTO YAKE

Ilikuwa ndoto yake siku moja kucheza timu inayochukua mataji ya Ligi Kuu, Kombe la FA, Ngao ya Jamii na kushiriki Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho jambo analoona limetimia na kilichobaki ni kujituma kwa bidii.

"Ni matamanio ya kila mchezaji kuvaa medali za ubingwa wa Ligi Kuu, kucheza michuano ya CAF, nashukuru kupata nafasi Simba, kazi ni kwangu kuipambania timu iliyoniamini kunipa nafasi ya kuwepo kikosini," anasema.

Anapoulizwa ni kipi kimebadilika kwake baada ya kujiunga Simba? Nyota huyo anajibu: "Staili ya maisha ya Simba ni tofauti na timu niliyotoka yapo mambo ambayo siwezi kuyafanya tena kwa ajili ya kulinda 'brand' ya timu, mfano wakati nipo Geita Gold tukimaliza mechi unaweza ukaenda kupiga misele bila shida, ila huku ni tofauti.

"Pia katika mitandao yangu ya kijamii mfano Instagram kabla ya kujiunga Simba nilikuwa na watu elfu sita, lakini kwa sasa nina zaidi ya wafuasi elfu 50, ambao wananishauri nikaze buti."

FADLU HANA MCHEZO

Mshambuliaji huyo anasema siku moja kabla mechi na Fountain Gate iliyopigwa Jumapili ya Agosti 25 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam aliomba ruhusa kwa Fadlu ili akajumuike na familia kusherehekea tukio la dada yake kuvishwa pete, lakini aligomewa.

"Nilitaka anipe angalau saa mbili au moja, lakini alinijibu hayo hayana nafasi na sioni umuhimu wa tukio la ulazima wa wewe kuwepo. Akanisisitiza akili niiweke katika mchezo," anasema mchezaji huyo.

"Dada, shemeji na baba walikuja uwanjani kwa kunisapraizi, ndio maana baada ya kufunga bao, nikaona ni sehemu yangu ya kusherehekea nao, baada ya kukosekana katika tukio hilo".

NI ZAIDI YA MAUMIVU Mashaka anasema kitendo cha timu yake ya zamani (Geita Gold) kufungua mashitaka baada ya kusaini Simba, kilimuumiza na muda wa kesi alikuwa anakosa amani na utulivu.

"Nilipokuwa naangalia mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea katika mitandao na vyombo vya habari kuhusiana na Geita kuishtaki Simba ilikuwa inaniumiza maana nilitamani kuachana nayo kwa amani kama nilivyokuwa nimeitumikia kwa amani," anasema.

"Meneja wangu, wachezaji wenzangu na viongozi wa Simba waliniambia nitulie, kwani ishu ipo kisheria na TFF ni sehemu ya kutoa haki kwa kila mtu, lilipoisha nilifurahia na nikaanza kuweka akili katika kazi."

LILILOMTOA MACHOZI

Hakumbuki vizuri kama ilikuwa 2019 au 2020 akiwa anaichezea Azam B, kwani siku moja kabla ya mechi dhidi ya Yanga B akiwa anapiga stori na washambuliaji wenzake jinsi ya kufunga katika mchezo huo, ghafra alitokea kocha ambaye hakumtaja jina lake na alichomwambia kilimtoa machozi.

"Kocha akaniambia unapochangia hiyo stori ya kufunga Yanga B, Mashaka utacheza mechi ipi ama unapoteza muda tu. Niliumia sana moyo na kujiona sistahili nikaondoka na kujitenga peke yangu nikalia sana.Nikamuomba Mungu anipe uvumilivu ili siku moja nije kuwa mchezaji mkubwa.

"Msimu huohuo kulikuwa na mashindano ya timu za vijana yalifanyika Arusha, ajabu nikawa kinara wa mabao saba kati ya mechi sita nilizokuwa nimecheza," anasema.

Anapoulizwa baada ya kuibuka kinara wa mabao saba katika mashindano ya vijana kocha aliyemkatisha tamaa hakumfuata? Anajibu: "Alinifuata na kuniambia alikuwa ananitania, ila mimi nilielewa vibaya ingawa ni kweli sikucheza dhidi ya Yanga B."

MAJARIBIO YA SWEDEN

Mashaka anasema kuna kipindi alikwenda kufanya majaribio nchini Sweden katika klabu ya Gais ambayo tayari imeshapanda Ligi Kuu, lakini alishindwa kujiunga kutokana na kushindwa makubaliano.

"Japo katika mazoezi ambayo nilifanya na timu hiyo kocha aliyapenda na kutaka niwe sehemu ya kikosi, lakini kulikuwa na makubaliano baina ya wasimamizi wangu na viongozi wa klabu hiyo yalishindwa kufikia, ila bado nina imani ipo siku nitacheza nje ya mipaka ya Tanzania," anasema Mashaka ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao sita Geita.

Chanzo: Mwanaspoti