Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAKALA MAALUM: Kuna hisia viongozi wapo kwenye gharama za mchezo

Salim Save MAKALA MAALUM: Kuna hisia viongozi wapo kwenye gharama za mchezo

Mon, 24 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Pamoja na wadau kupaza sauti sana dhidi ya mgawanyo wa mapato ya mlangoni unavyoumiza sana, si rahisi kusikia kilio hicho kikitoka midomoni mwa viongozi wa klabu na hata kusikia utetezi ukitoka kwa viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) wala Bodi ya Ligi (TPLB).

Kilio kilikuwepo zamani kidogo lakini kikaanza kutoweka taratibu hadi sasa hakisikiki kabisa.

Pamoja na Simba kupata mgawo wa Sh. Milioni 188 kutoka katika mapato ya jumla ya Sh. Milioni 410.6, hakuna kiongozi aliyeonyesha kuumizwa na mgawanyo uliosababisha klabu mwenyeji kupata chini ya nusu ya mapato ya jumla.

Kwa hiyo, kadri siku zinavyokwenda ndivyo suala hilo linavyozidi kuonekana la ajabu. Ni kwamba viongozi wameanza kuelewa kuhusu kanuni hiyo ya mgawanyo au wamekuwa sehemu ya mgawo, hasa kile kipengele nyeti cha gharama za mchezo? Kama nilivyoeleza jana, kanuni haziweki bayana wahusika hasa wa malipo hayo.

“Asilimia saba (7) ya gharama za mchezo itatumika kulipia gharama mbalimbali za huduma zitakazoalikwa na kutolewa kufanikisha mchezo husika. Gharama za mchezo zigawanywe kwa kutumia fomu maalum inayotolewa na TPLB,” inasema kanuni ya 29 ya Kanuni za Ligi Kuu.

“TPLB/TFF itatoa waraka mwanzoni mwa msimu utakaofafanua viwango vya malipo ya maofisa wa mchezo na utaratibu wa malipo.”

Kama nilivyoeleza, kanuni haziendi mbali kufafanua wahusika katika kipengele hiki, ingawa zinamtoa “msimamizi wa kituo, kamishna, mratibu wa mchezo, mtathmini wa waamuzi na waamuzi” zikisema watalipwa na TLPB. Huo waraka unaotolewa TPLB hujumuisha watu gani wanaotakiwa walipwe hizo Sh. Milioni 22.6.

Bila shaka hapa ndipo kuna wapigadebe muhimu kwa viongozi wa klabu, TFF na TPLB wanaonufaika na mgawo huu na ndio maana hakuna kati yao anayepaza sauti kulalamikia gharama za mchezo.

Kwa ujumla eneo hili hujumuisha chawa wengi wanaotumia ustadi wao wa kuzungumza, kusifu viongozi wa klabu, viongozi wa TPLB, viongozi wa TFF na wengine wenye mamlaka katika soka. Wataingizwaje katika gharama za mchezo, ni TFF, TPLB na viongozi wa klabu ndio wanaojua. Kwa hiyo si ajabu kwamba suala hili halilalamikiwi kwa kuwa mzigo wanabeba wote, ingawa klabu ndio zinaumia zaidi kulingana na jinsi zinavyotumia fedha nyingi kujenga vikosi, kutangaza mechi na kujiandaa kwa mchezo.

Wale wenye kampuni za kutoa huduma pia ni wahusika katika eneo hili. Wale wenye kampuni za ulinzi kwa ajili ya kutoa askari maalum wa ulinzi (stewards au wale mabaunsa) ndio pia wanaochukua chao kutoka eneo hili. Madai wanayowasilisha ni shilingi ngapi? Hilo litajulikana hukohuko. Kampuni ni ya nani na je ni ya kiongozi ambaye suala hilo linaweza kusababisha mgongano wa maslahi? Hilo litajulikana mbele kwa mbele. Maswali yako mengi na majibu ni adimu.

Usije ukaona mtu anazungukazunguka pale eneo la VIP, ukadhani anahangaika tu, huyo yumo kwenye mgawo, hata kama hapokei kwa kusaini moja kwa moja kwenye karatasi kubwa ya waliotoa huduma.

Unapozungumzia stewards unapata swali jingine kwamba wale polisi ambao huthubutu hata kwenda kutoa ulinzi kwa waamuzi, kazi yao ni nini?

Kwa utamaduni wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), si muhimu kuwa na askari walioshika bunduki ndani ya uzio wa uwanja. Wanatakiwa kuwa sehemu wamewekwa pamoja tayari kutoa huduma wakati wowote wanapohitajika na si kuzurura ndani na silaha za moto.

Ndio, wenzetu barani Ulaya wameshastaarabika kiasi kwamba huwezi kumkuta askari mwenye silaha, wala kundi la wababe (mabaunsa) getini wakati wa kuingia kwa kuwa hakuna anayetaka kuingia bure wala kwa mchongo, hasa sisi viongozi na watumizi wengine wa mpira tunavyopenda VIP. Lakini utamaduni huu tutaujenga kwa miongo mingapi kama kweli binadamu anabadilika? Huko barani Ulaya kulikuwa na mambo hayahaya, lakini yanaisha kadri athari za ujanjaujanja huo zinapojitokeza.

Pengine unaweza kuona ninakwenda nje ya mada, la hasha. Nakupa picha utambue vile unavyoviona vinahusika vipi katika gharama za mchezo. Kwa hiyo umewalipa stewards, lakini pia unatakiwa uweke mzigo japo kidogo kwa askari wa Jeshi la Polisi ili “wale na kunywa” wakati wakitekeleza majukumu yao. Hawa nao watakuletea idadi ya askari kulingana na ukubwa wa mchezo na kwa jinsi walivyotathmini hali ya usalama kwa kutumia intelijensia yao. Hapa hakuna mjadala.

Sasa stewards wa nini na polisi wa nini? Kwa namna moja au nyingine wote wanahitajika, lakini kwa kiwango gani na kwa majukumu gani? Kumbuka hata polisi wamelalamikiwa kuwa wanapunguza mapato kwa kuingiza watu kwa malipo ya nje ya mfumo. Wapo watoa huduma wengine kama zimamoto, ambao siku hizi wamesema ni lazima wawepo kwenye mkusanyiko wowote. Kiwango cha malipo yao kitatokana na wao walivyowasilisha madai yao.

Usisahau wale watu wa huduma ya kwanza, ambao pengine ni muhimu sana kutokana na matatizo yanayoibuka kwenye mikusanyiko mikubwa, ikiwemo hiyo ya Simba na Yanga ambao mashabiki huanza kupoteza fahamu dakika za mwanzo kabisa na hali hiyo huendelea hadi mchezo unakwisha. Kiwango cha malipo yao pia kitategemea jinsi walivyoamka

Siku nyingine unaona waamuzi wamevaa vinasa sauti na spika masikioni, unaweza kukuta hizo pia huingia kwenye gharama za mchezo. Binafsi nilishawahi kupata malalamiko kutoka kwa mtu aliyedai vifaa vyake vilitumika lakini akacheleweshewa malipo. Kwa hiyo, vipengele vya mgawo, kama nilivyovionyesha katika makala ya awali, viko vingi. Vipo ambavyo vinaonekana kama vimedurufishwa lakini ni muhimu na viko ambavyo viwango vyake vya malipo vinaweza kudhibitiwa iwapo hakutakuwa na kuoneana aibu.

Kama nilivyoeleza hapo juu, hali ya kuoneana aibu inatokana na kila mtu kuwa na uchafu ambao huvutia chawa. Hao chawa ni lazima waishi kwenye uchafu huo unaosababisha viongozi wa pande zote tatu kufanya kila jitihada wawalishe kutoka katika mgawo.

Kanuni zinazoongoza mgawanyo wa mapato zilitungwa muda mrefu na zinafanyiwa marekebisho kila baada ya muda fulani. Lakini wakati huu ambao udhamini unaanza kumiminika katika soka, ni muhimu kuziangalia kwa jicho la mwelekeo mpya ili kupunguza hicho kinachoonekana ni kuzinyonya klabu.

Kesho tutaona ni jinsi gani tunavyoweza kuepukana na malalamiko ambayo tunaonekana kuyafungia masikio.

Chanzo: Mwanaspoti