Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAKALA: Kweli Yanga daima mbele nyuma mwiko?

Jangwani Beach.jpeg MAKALA: Kweli Yanga daima mbele nyuma mwiko?

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Septemba 2, 1990 niliamshwa asubuhi na Babu yangu Fidelis Makwega kuelekea Viwanja vya Jangwani kwa ajiri ya misa kubwa iliyosaliwa ambayo Tanzania ilimpokea Baba Mtakatifu Yohane Paul II.

Kwa kuwa nyumbani ni Mbagala basi tuliamka saa 10 ya alfajiri kuelekea huko. Kwa desturi ya usafiri wa wakati huo ukitoka Mbagala Sabasaba basi hilo lilikuwa linapitia hadi Temeke Mwisho.

Kwa kuwa tulikuwa tunaenda Jangwani tulitakiwa kupanda mabasi ya Girls School (Sasa Gerezani) na kushuka hapo. Siku hiyo hali ilikuwa tofauti sana kwani mabasi yalitambua ujio huo yalivunja sheria, kwa hiyo tulipanda basi la moja kwa moja kupitia Kilwa Road na Shimo la Udongo hadi Girls Schools na kushuka hapo na tulitembea kwa mguu mpaka Viwanja vya Jangwani.

Katika ujio huo nyumbani kwetu ushiriki wetu ulikuwa kama ifuatavyo nina binamu yangu mmoja ninayempenda sana anaitwa Piencia Nyema(Mngoni /Mpogoro) yeye alipata wasaa wa kwenda hadi uwanja wa ndege akiwa miongoni mwa watoto waliompokea Baba Mtakatifu. Siku hizi binamu yangu huyu ni mama wa watoto kadhaa akikaribia kujukuu. Pia nilikuwa na shangazi yangu mmoja anayefahamika kama Demetria Makwega yeye alikuwemo katika kwaya maalumu iliyoimba katika misa hiyo ya Septemba 2, 1990.

“Tumpokee kwa shangwe na heri, Tumpokeaa ehe Baba Yohane Paulo, Kiongozi, Mchungaji, Mtumishi wetu mwema wa Kanisa katoliki….”

Hayo yakiwa ni miongoni mwa maneno ya wimbo mmojawapo wa makaribisho hayo.

Ibada ilikuwa kubwa sana tulisali watu wengi huku kukiwa na jukwaa moja kubwa ambalo lilijengwa vizuri kwa mapokezi haya. Nadhani jukwaa hilo lilibakia hapo kwa miaka kadhaa likiwa ni jengo pekee ambalo likiyapamba mandhari ya eneo hilo.Baba Mtakatifu huyo akisalisha huku akitoa baraka ya mwisho kwa lugha ya Kiswahili.

Nakumbuka katika eneo hilo kulikuwa na jengo lingine kubwa la miaka mingi ambalo lilikuwa ni jengo la ghorofa pekee kwa muda mrefu ambalo ulikuwa Viwanja vya Jangwani lilikuwa likionekana kwa juu kama unatazama upande wa Kariakoo.

Jengo hili la Klabu ya Yanga pia liliweza kuonekana vizuri kwa mtu ambaye yupo Magomeni. Mwaka huo wa 1990 nilipomaliza kusali niliwaacha ndugu zangu kurudi Mbagala na mie kuungana na wezangu niliyokutana nao ambao niliwahi kusoma nao tuliamua kupita njia inayoelekea Uwanja wa Kaunda ambao ni uwanja wa timu ya Yanga wenye jengo hili.

Tulitembea umbali kama wa dakika 10 tulikutana na mto ambao ulikuwa mwembamba huku ukipitisha maji machafu ikiwamo takataka za pombe ambazo zilikuwa zinazalishwa na kiwanda cha bia huku uchafu huo ukielekezwa bonde la Muhimbili kuelekea Daraja la Salender.

Tulivuka mto huu ambapo juu yake kulikuwa na vyuma na mbao na tulitembea kidogo tukawa kama tunapanda kilima kidogo tukakaribishwa na ukuta mkubwa ambao ulikuwa umezunguka jengo la klabu ya Yanga. Kwa kuwa tulikuwa vijana wadogo na hatukuwa na kiingilio tuliweza kuruka ukuta huu wa Yanga na kuingia ndani kukiwa na mazoezi ambayo sikukumbuki kama ilikuwa Yanga B au la.

Tulipoingia hapo tulikutana na kiwanja ambapo mazoezi haya yalikuwa yakifanyika huku getini ilitakiwa kila anayepita kulipa fedha ya kiingilio.

Upande ambapo wa juu ya kiwanja hiki palikuwa na eneo ambalo lilikuwa kama kilima hivi hapo kulikuwa na sehemu ya kufanyika michezo mingine kama vile ngumi huku eneo hilo huwa linatumika kukaa watazamaji.

Hiyo ndiyo ilikuwa mandari ya uwanja huu wa Kaunda miaka hiyo ambayo leo hii ni miaka kama 31. Mandari hiyo niliyoiona miaka hiyo siyo mandhari ya eneo hilo leo hii kwani ule ukuta ambao siye kama watoto tuliweza kuruka leo haupo na huo uwanja leo uliotumika kwa mazoezi haupo kwani umejazwa udongo.

Ukiangalia ule usawa wa ukuta ambao tuliweza kuuruka ndiyo usawa wa paa za nyumba zile zilizosombwa na mafuriko.

Nilidokezwa kuwa Wana wa Jangwani sasa wakiujaza udongo huo usawa wa uwanja, kwa usawa wa ukuta na paa za nyumba zilizosombwa na mafuriko. Nia ya Yanga kuweka kifusi hiki ni kuhakikisha mara baada ya kukijaza vizuri ingesaidia kuweza kujenga vizuri.

Swali ni je hayo maji ya mvua yanayosababisha mafuriko katika eneo hilo hayawezi kuubadilisha udongo huo na kuwa tope? Na eneo hilo kujaa tena maji?. Kwa hakika kuna uwezekano mkubwa wa udongo huo utakuwa tope na kusombwa na mafuriko.

Niliwahi kumuuliza rafiki yangu mmoja ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Tanzania Jemedari Said aliniambia kuwa:

“Timu hii inapaswa kuhakikisha inamshukuru sana mheshimiwa Paul Makonda aliwahi kuwapa eneo la kujengwa uwanja huko Kigamboni la hekari 7 ambalo lilikuwa na thamani ya shilingi milioni 700 kwa wakati huo”

Nadhani mawazo ya Mheshimiwa Makonda yalikuwa ni sahihi na faida kubwa kwa Yanga. Mdau huyu wasoka anasema kuwa eneo waliopatiwa Yanga ni kubwa na lina manufaa makubwa kiuwekezaji.

Pili eneo la Kigamboni namna lilivyo ni eneo lililo jirani na bahari na mara zote maeneo haya huwa tambalale sana kwa hiyo suala la mafuriko linaweza kuwa ni hadithi ya kusahau na mito michache inapita na kumwaga maji yake usawa wa bahari huko Kigamboni .

Tatu, mchezo wa soka wa sasa unahitaji sana kukuza vipaji na kuwajenga vijana wadogo, kwa hiyo Yanga wanapokuwa na eneo kubwa wanaweza kujenga hata Hosteli ya vijana hao wa Yanga B na wao kuishi hapo huku wakifundishwa mchezo huyo.

Nne, Ndugu Jemedari alisema kuwa hivi sasa kilabu nyingi za soka zinategemea ufadhili wa mtu mmoja kwa hakika kama uwekezaji mkubwa utafanyika iwe kwa mkopo au mkataba wowote ule unaweza kuepusha timu hizo kuwa chini ya mtu mmoja.

Tano, Mdau huyu anasema hata eneo hilo la bure na bure ina gharama sana, Yanga wana wajibu wa kufanya uchunguzi wa ardhi hiyo ilivyo huku wasije kujenga kwa haraka na baadaye majengo kuweka ufa.

Kwa wana Yanga wanawajibu wa kuhakikisha wanatumia eneo hilo mapema vinginevyo anaweza kuja Baba Mtakatifu mwingine kutembelea Tanzania huku Yanga wakiwa bado wanapambana na mafuriko ya Jangwani. Niliambiwa kuwa hivi sasa Simba tayari wanatumia kiwanja chao cha Bunju kwa mazoezi huku kikiwa na hosteli nzuri, wana Yanga wanapaswa kuiga hilo na kulifanyia kazi kwa haraka sana. Kweli Yanga iwe daima mbele na nyuma iwe mwiko.

[email protected]

0717649257

Chanzo: www.tanzaniaweb.live