Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAGUFULI ALIVYOZIBEBA SIMBA, YANGA

7cd59ffd7e2ff841b927668a6e8e168b.jpeg MAGUFULI ALIVYOZIBEBA SIMBA, YANGA

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KLABU kongwe za Simba na Yanga ni miongoni mwa zitakazomkumbuka Rais John kutokana na yale waliyoyapata katika uongozi wake ambayo ni ngumu kufutika kirahisi.

Tangu enzi za mkoloni soka la Tanzania, limekuwa likibebwa na timu za Simba na Yanga. Ndizo zimekuwa kioo kwa timu za madaraja ya chini kutokana na mafanikio yake ya ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Magufuli aliliona hilo ndio maana aliamini kuzisapoti timu hizo ilikuwa ni kuleta chachu ya mchezo wa soka nchini ambapo katika kipindi cha uhai wake umeifanya Ligi Kuu Tanzania Bara iongezeke ushindani na kuwa mfano katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Hivi sasa huwezi kuutaja mpira wa Afrika Mashariki pasi na kuigusa Simba na Yanga, ambazo kwa sasa zimekuwa zikivutia wachezaji kutoka mataifa makubwa kisoka kama Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ghana, Burkinafaso, Angola, Msumbiji, Zambia na Ivory Coast, hii inaonesha jinsi gani alikuwa na lengo la kuupeleka mbali mchezo wa soka nchini.

Miamba hii ya soka nchini itamkumbuka Magufuli kwa haya. Simba ndio timu ambayo itakuwa na kumbukumbu nzuri na Magufuli kwani katika kipindi chake imeingia hatua ya makundi mara mbili katika kipindi cha misimu mitatu ilianza mwaka 2018/19 ambapo iliingia makundi na kuishia hatua ya robo fainali na kuondolewa na TP Mazembe.

Msimu uliofuata 2019/20 haikuwa na mwendo mzuri ikaondolewa hatua ya awali na UD Songo ya Msumbiji , kabla ya kurudi kwa kasi msimu wa mwaka 2020/21 ambapo hadi Magufuli anafariki, Simba inaongoza kundi A, lenye timu za Al Ahly, AS Vita na Al Merrikh.

Kwa muda mrefu Simba na Yanga zilikuwa zikiendeshwa na matajiri ambao walipoamua kukaa pembeni mambo hayakuwa yakienda lakini katika uongozi wa Magufuli timu hizo zimeingia katika mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa mfumo wa hisa ambapo wanachama watakuwa wakimiliki asilimia 51 na mwekezaji akimiliki asilimia 49, hivyo kuwapa mamlaka wanachama.

Mchakato huo unaendelea vizuri lakini wakati mambo yakienda vyema Magufuli, ameondoka na kushindwa kushuhudia kile alichokipambania.

Kwa muda mrefu Simba na Yanga licha ya ukubwa wao zilikuwa hazinufaiki na mauzo ya jezi kutokana na kutapakaa kwa jezi feki lakini katika awamu ya Magufuli jambo hilo limepungua kama si kukoma kabisa.

Tumeshuhudia viongozi wa Simba na Yanga wakiwa sambamba na Jeshi la Polisi kutafuta wauzaji wa jezi feki kama alivyofanya aliyekuwa katibu mkuu wa Yanga Charles Mkwasa Oktoba 8, 2017 lakini pia Desemba 11, 2020 Yanga chini ya Ofisa uhamasishaji wake Antonio Nugaz waliendesha msako wa jezi feki Kariakoo na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Mgufuli pia atakumbukwa kuongeza hamasa kwenye michezo wa soka kwa kuingia viwanjani kuhamasisha mashabiki kujitoa kwaajili ya timu zao rejea tukio lake la kwenda kushuhudia sherehe za ubingwa wa Simba, lakini pia alipata wasaa wa kushuhudia pambano la watani wa jadi ambalo Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa kujitoa na kuzisaidia klabu hizi kongwe kupata udhamini ambapo kupitia ushawishi wake aliwavutia Gharib Mohamed wa GSM na Rostam Aziz wa Taifa Gas kuwekeza Yanga, lakini pia kupitia Wizara ya maliasili aliwapa udhamini Simba, kutokana na jinsi wanavyofanya vyema nje ya mipaka ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz