Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MAELEKEZO: Wachezaji Ligi Kuu wapewa mchongo

99700 Pic+wachezaji MAELEKEZO: Wachezaji Ligi Kuu wapewa mchongo

Fri, 20 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kusimama mashindano ya soka nchini kwa mwezi mmoja inaweza kuwa fursa nzuri kwa wachezaji wa timu mbalimbali kupumzisha mwili na kujiweka fiti kabla ya kuendelea siku za usoni.

Mashindano hayo yamesimamishwa na Serikali na utekelezaji wake ukafanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa ni miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na tishio la kuenea kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

Baada ya kucheza idadi kubwa ya mechi kwa miezi mitatu mfululizo bila kupata mapumziko, hii inaweza kuwa nafasi adimu kwao kujiweka sawa tofauti na mashindano mengine yasingesimamishwa.

Kuanzia Januari kumekuwa na mechi mfululizo za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, Kombe la Azam Sports Federation pia wapo wachezaji ambao sehemu kubwa ya mzunguko wa kwanza wa ligi walitumikia timu za taifa katika mashindano mbalimbali.

Wachezaji wa timu za Ligi Kuu walikuwa na muda mchache kupumzika na hata kuimarika baada ya kupata majeraha, kutokana na ratiba ngumu ya kucheza idadi kubwa ya mechi ndani ya muda mfupi kuanzia Januari hadi sasa.

Pia ratiba hiyo ilihusisha safari za mara kwa mara kwa kutumia usafiri wa barabara kutoka mkoa mmoja hadi mwingine

Pia Soma

Advertisement
Kwa wastani kuanzia Januari Mosi hadi sasa, idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu zimecheza michezo 18 katika siku 79, hivyo tofauti ya muda kutoka mechi moja hadi nyingine ni siku nne.

Ndani ya siku hizo nne, baadhi ya timu husafiri kutoka kituo kimoja kwenda kingine, kupumzisha miili baada ya mechi iliyopita na kufanya mazoezi ya kujiandaa na mechi inayofuata.

Lakini kwa timu nyingine, ndani ya kipindi hicho zimekuwa zikikabiliwa na wachezaji wenye majeraha ama ambao wametoka kupona wakihitaji muda wa kujiimarisha.

Kusimama kwa ligi na mashindano mengine kumechukuliwa kama afueni kwa timu na haikushangaza kuona zikitangaza kuwapa mapumziko wachezaji wao.

Ili kulinda viwango vyao nyota hao wa timu mbalimbali wameshauriwa kukitumia kipindi hiki kufanya mazoezi binafsi na kujiweka sawa jambo ambalo linaweza kuwapa unafuu makocha pindi wakirejea kambini.

Mbali na hilo, umakini katika matumizi ya vyakula na taratibu nyingine za kiafya zinapaswa kuzingatiwa na wanasoka walio mapumzikoni ili kutojiweka katika uwezekano wa kupata majeraha au kuongezeka uzito jambo linaloweza kuathiri programu na mipango ya makocha wao.

Ni kama ambavyo mastaa wa timu zinazoshiriki ligi Ulaya wamekuwa wakitumia kipindi hiki kujiimarisha kwa kufanya mazoezi binafsi katika makazi yao ili kuhakikisha wanalinda ufiti wa mwili.

Mfano wa nyota ambao wamekuwa wakitumia kipindi hiki kujiweka fiti ni beki wa Real Madrid, Sergio Ramos ambaye hivi karibuni aliachia video inayomuonyesha akifanya mazoezi binafsi nyumbani kwake.

Kocha wa Namungo Hitimana Thiery alisema anaamini wachezaji wake watakitumia vyema kipindi hiki watapata manufaa watakaporejea katika mashindano yakianza.

“Baada ya siku 10 watarejea kambini kwa kipindi chote cha mapumziko naamini wataituliza miili na kujiweka sawa na kubwa zaidi wazingatie kanuni za afya,” alisema Thiery.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema kuwa wameandaa programu kwa wachezaji wao katika kipindi hiki ambacho watakuwa mapumzikoni na kila mmoja atapaswa kuifuata.

‘Kocha wa viungo, Riedoh Berdien amewapa ratiba wachezaji wote wakiwa majumbani kwao. Ratiba ya chakula, kuishi, muda wa kufanya mazoezi na mambo mengine ya msingi,” alisema Eymael.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije aliwataka wachezaji wote bila kujali wanacheza klabu ndogo au kubwa kufuata nidhamu watakapokuwa katika siku za mapumziko.

Chanzo: mwananchi.co.tz