Huu ni mtego. Ukisikia una mechi dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, usiende hutatoka salama. Pale ni machinjioni.
Yanga ambayo kwa sasa inautumia uwanja huo kama wa nyumbani baada ya ule wa Benjamin Mkapa kufungiwa kwa muda kupisha marekebisho, imekuwa na rekodi tamu kwenye Chamazi na imefunga mabao mengi zaidi ya viwanja vyote ilivyocheza msimu huu na kwa jumla imefunga mabao 28.
Nje ya uwanja huo, Yanga imefunga mabao 20 na jumla ina mabao 48 baada ya mechi 19 ilizocheza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kwenye mabao hayo 28 iliyofunga kwenye uwanja huo unaomilikiwa na klabu ya Azam FC, ni rekodi ya kipekee na inaonekana mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara inaujulia uwanja huo hasa kwenye kufunga mabao mbali na umiliki wa mpira na kila timu inayokutana nayo hapo haitoki salama.
Msimu huu (2023/24) Yanga imekuwa ya moto hasa kwenye uwanja huo na imecheza mechi saba za Ligi Kuu, imeshinda zote, imevuna mabao 28 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara tatu tu na kuvuna pointi 21.
Nyota wa timu hiyo waliofunga mabao mengi kwenye uwanja huo ni Stephane Aziz Ki aliyefunga mabao sita, Mudathir Yahya (5), Maxi Nzengeli (4) na 13 yaliyosalia yamefungwa na wengine.
Mwanaspoti linakuchambulia kwa njia ya namba (data) namna Yanga ilivyo mbabe ikicheza kwenye uwanja huo ambao ni machinjioni kwa kila anayetua kucheza hapo.
MSIMU 2023/24
YANGA 5-0 KMC (Azam Complex)
Wafungaji ni Dickson Job (dk17), Aziz Ki (dk 58'), Hafidh Konkoni (dk 69'), Mudhathir Yahya (dk76) na Pacome Zouzoua (dk82).
YANGA 5-0 JKT Tz (Azam Complex)
Wafungaji ni Ki (dk 45+5), Kenedy Musonda (dk54), Yao Kouassi (dk 64) (Max Nzengeli (dk79 na 88).
YANGA 1-0 NAMUNGO FC (Azam Complex,23/10/2023)
Mfungaji Mudathir (dk 88)
YANGA 2-1 MASHUJAA
Wafungaji Nzengeli (dk 45) na Mudathir(dk 85)
YANGA 4-1 MTIBWA (Azam Complex)
Wafungaji Yanga ni Aziz Ki (dk 45, p 65), Musonda (dk 76) na Mahlatse Makudubela 'Skudu' (dk 83).
YANGA 1-0 DODOMA JIJI (Azam Complex)
Mfungaji Mudathir (dk86)
YANGA 5-1 IHEFU (Azam Complex)
Wafungaji Pacome Zouzoua (dk10,) Mudathir (dk30), Aziz Ki (dk 68), Augustine Okrah (dk84) na Nzengeli (dk86).
YANGA 1-0 GEITA (Azam Complex)
Mfungaji ni Aziz Ki (dk 28)
KOMBE LA ASFC
Ukiachana na Ligi Kuu, mechi za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Yanga ilishinda ushindi mnono kwenye Uwanja wa Azam Complex, Raundi ya kwanza na ya pili.
Yanga 5-1 Hausing FC
Yanga 5-0 Polisi Tanzania
Yanga 5-1 Asas Djibout
WASIKIE MUDA/NZENGELI
Mudathir anayeonekana kuujulia uwanja huo, amesema "Uwanja wa Azam Complex ni kama nyumbani, nimecheza mechi za mashindano, nimefanya mazoezi, hivyo nimeuzoea."
Kwa upande wa Nzengeli amesema; "Ninapokuwa uwanjani, nawaza kufanya kazi ipasavyo, ili timu ipate ushindi, nikifunga sawa, nikitoa asisti ni sawa."