Mshambuliaji wa Azam FC, Ayoub Lyanga anatarajia kwenda Afrika Kusini keshokutwa Alhamis kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata.
Akiwa Afrika Kusini Lyanga atapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Life Vincent Pallotti ya Cape Town, ambayo mara zote wachezaji wa klabu ya Azam FC wamekuwa wakitibiwa tangu mwaka 2011.
Kiungo huyo Mshambuliaji, alipata majeraha kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya dhidi ya Geita Gold FC, uliochezwa Jumanne (Novemba 02), Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Lyanga aliumia dakika ya 72 baada ya kugongana kichwa na Raymond Masota wa Geita Gold, wakati wakiwania mpira wa juu.
Mara baada ya kupata majeraha hayo, alifanyiwa huduma ya kwanza uwanjani kabla ya kupelekwa Hospitali ya Mbagala, kwa ajili ya huduma ya haraka kuzuia damu kuendelea kutoka puani.
Kisha akapelekwa Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi na kugundulika kuwa amevunjika mifupa mitatu kwenye paji la uso.
Kwanza ni mfupa wa pua, kitaalamu ukiitwa Nasal Bone, Pili mfupa unaoshikilia meno ya juu, yaani Maxillary Bone na tatu ni mfupa wa macho Facial Bone.