Nyota wa Azam FC, Ayoub Lyanga anatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold.
Kiungo huyo mshambuliaji aliumia katika mechi hiyo baada ya kugongana kichwa na mchezaji wa Geita, Raymond Masota wakati wakiwania mpira wa juu.
Daktari wa timu hiyo, Mwanandi Mwankemwa alisema Lyanga alifanyiwa vipimo vya X-Ray katika Hospitali ya Ekenywa iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam na kugundulika kuvunjika mfupa wa pua na jino kabla ya kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Mara baada ya kupata majeraha hayo alifanyiwa huduma ya kwanza uwanjani kabla ya kupelekwa Hospitali ya Mbagala, kwa ajili ya huduma ya haraka kuzuia damu kuendelea kutoka puani, kisha akapelekwa Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi na kugundulika kuwa amevunjika mifupa mitatu kwenye paji la uso,” alisema.
Lyanga atapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Life Vincent Pallotti iliyopo Cape Town, Afrika Kusini.