Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lyanga amwaga wino Geita Gold

Lyanga Pic Data Dany Lyanga kushoto akisaini kandarasi ya kuitumikia Geita Gold

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Klabu ya Geita Gold imethibitisha kuwasajili nyota wanne akiwemo mshambuliaji wa zamani wa JKT Tanzania, Dany Lyanga ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo kwenye Ligi Kuu na kombe la Shirikisho msimu ujao.

Baada ya kupanda daraja kwa Mara ya kwanza msimu huu, timu hiyo iko kwenye maandalizi ya kuhakikisha inasuka kikosi na kuwa tishio pale michuano ya Ligi Kuu itakapoanza Septemba 29, mwaka huu.

Akithibitisha usajili huo Katibu Mkuu wa timu hiyo, Revinus Ntare amewataja nyota wengine waliosajiliwa ni Kelvin Nashon kutoka JKT Tanzania ambaye amelamba mkataba wa mwaka mmoja baada ya klabu yake kushuka daraja msimu huu.

Wengine ni Iddy Mobby kutoka Polisi Tanzania aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya kutemwa na maafande hao wa mkoani Kilimanjaro, pia yumo nyota wa zamani wa Gwambina FC, Yusuph Kagoma ambaye amekula mkataba wa miaka miwili ndani ya wachimba Dhahabu hao.

Ntare amesema mbali na nyota hao, tayari kikosi chao kilishanasa saini za Salim Aiyee kutoka KMC, Olfen Chikola kutoka Fountain Gate huku wakiwaongezea mikataba nyota 10 waliokuwa nao kwenye michuano ya daraja la kwanza.

Walioongezewa mikataba ni mshambuliaji Venance Ludovick, mabeki wa kati Chilo Mkama na Pius Joseph, Baraka Jerome, Lambele Jerome, Geofrey Luzendaze, Jonathan Ulaya, Makenzi Ramadhan, Jeremiah Rubanguka na Sebusebu Samson.

Katika hatua nyingine, timu hiyo imesaini mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya Masita kwa ajili ya vifaa vya michezo vitakavyotumiwa na kikosi chao kwenye michuano mbalimbali ndani ya miaka mitatu.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz