KOCHA wa Kagera Sugar, Francis Baraza amesema kiwango alichokionyesha kiungo mkabaji wa Simba, Mganda Thadeo Lwanga kimeipa uzito nafasi hiyo, kuondoa presha kwa Didier Gomes (Simba) ya kutegemea mchezaji mmoja.
Kabla ya Simba kumsajili Lwanga, mzawa Jonas Mkude ndiye alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, lakini kwa sasa kumekuwa na ushindani baina ya viungo hao, jambo linalompa uhuru Kocha Gomes kumtumia anayemtaka.
Baraza alisema; “Mantiki ya Simba kuwa na kikosi kizuri ni kwa sababu kila nafasi ina wachezaji wenye kiwango cha juu ambacho anayeanza na kutokea benchi wote wanaweza wakabadili matokeo, ikiwemo nafasi ya kiungo mkabaji anayocheza Mkude na Lwanga wote wapo vizuri.”
“Kiwango alichokionyesha Lwanga katika mechi alizocheza kinampa changamoto mzawa kuzidisha mazoezi na kuwa kwenye pigi ya kung’ang’aniana namba asiwepo anayejimilikisha, hilo ni faida kwa kocha kuwa na kikosi anachokiamini kumpa matokeo,” alisema.
Alisema anamfahamu Lwanga kabla ya kutua Simba ni mchezaji mpambanaji asiyependa kufanya kazi mbovu, hivyo anaamini Mkude atakuwa na mtazamo mpya wa nani ambavyo anatakiwa kukifikisha mbali kipaji chake.
Mbali na hilo, Kocha Baraza alikizungumzia kikosi chake anakiamini kitafanya kazi ya kuhakikisha wanabaki ligi kuu.
“Tangu nianze kuinoa Kagera Sugar, timu imecheza mechi tano nne za ligi moja ya Kombe la Shirikisho la Azam, katika hizo nimefungwa tatu, sare mbili na changamoto ya matokeo hayo bado nilikuwa nawasoma wachezaji,” alisema.