Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lule, kocha anayezipotezea Simba na Yanga

Lule Pic Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule

Sun, 6 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Msimu uliopita Mbeya City haikuwa na matokeo mazuri hadi kusubiri dakika za mwisho kujihakikishia kubaki Ligi Kuu chini ya Kocha Mathias Lule.

Lule, raia wa Uganda alitua kikosini ikiwa ni mechi mbili za mwisho kumaliza raundi ya kwanza akijaza nafasi ya Amri Said ‘Stam’ aliyeng’atuka kutokana na mwenendo usioridhisha.

Katika jumla ya mechi 20 alizosimamia kipindi hicho alishinda saba, sare tisa na kupoteza nne na kuisaidia timu kumaliza nafasi ya 10 kwa pointi 42.

Hata hivyo, kocha huyo baada ya kumalizika kwa msimu huo na kuiwezesha timu hiyo kubaki kwenye ligi mabosi waliamua kumuongezea mkataba wa kuendelea kusalia Mbeya.

Kazi nzuri aliyoonyesha hasa dakika za mwisho waliposhinda mechi nne mfululizo ikiwamo kipigo kikali cha mabao 4-0 dhidi ya Biashara United kiliwapa matumaini viongozi na kuamua kumbakisha.

Lule msimu huu amekuwa na mwenendo mzuri kutokana na kuisimamia michezo 14 ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho ambapo ameshinda mitano, sare saba na kupoteza miwili.

Hadi sasa timu hiyo ipo nafasi ya tatu kwa pointi 22, huku ikiwa ndio timu pekee iliyoweka rekodi ya kumsimamisha bingwa mtetezi Simba kwa kumfunga mara ya kwanza msimu huu kwa bao 1-0.

Mbeya City pia chini ya Lule imekuwa na rekodi tamu na ya kipekee kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kucheza mechi saba za Ligi Kuu bila kupoteza hata moja.

Kutokana na rekodi tamu na za kibabe alizoweka kocha huyo, amefunguka mipango na matarajio yake huku akisikitishwa kuwa timu ya kwanza Ligi Kuu kuondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho.

Siri ya mafanikio

Lule anasema kufanikiwa hadi sasa kunatokana na mjumuiko wa kitimu ndani na nje ya uwanja ambapo kila mmoja kwa nafasi yake anatimiza wajibu.

Anasema alichofaulu ni kuwaandaa wachezaji kikosini kuliko kumtegemea mtu mmoja, jambo ambalo limekuwa na faida kubwa.

Lule anasema kuwa kikosini kwake hakuna staa, bali timu yenyewe ndio inabaki kubeba taswira na nembo kwa ujumla, suala ambalo limewasaidia kwa kiasi kikubwa.

“Kila mtu anatimiza majukumu yake na kutekeleza wajibu, sisi hapa hakuna mchezaji staa, wote wanacheza mpira mmoja na hatumtegemei mtu mmoja isipokuwa ni kucheza kitimu,” anasema Lule.

Anafafanua kuwa kabla na baada ya mchezo hufanya tathmini na kuazimia kwa pamoja kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na hilo limewabeba katika mechi zao.

Mipango na mikakati

Kocha huyo asiye na maneno mengi anasema mipango yao ni kushinda kila mechi huku akifichua kuwa ubingwa siyo ishu.

Anasema Mbeya City hawawanii ubingwa, bali wanachopigania ni pointi tatu kila mechi na kwamba mambo ya Simba na Yanga ni kawaida kama zilivyo timu nyingine.

“Ubingwa? Sisi hatutaki labda tunachopambania ni pointi tatu kila mechi, hayo ya Simba na Yanga hawatupi presha ni sawa na timu pinzani nyingine ambazo tunapambana nazo,” anasema.

Anaeleza kuwa mikakati iliyopo ni kuwaandaa vyema kiufundi wachezaji ikiwa ni saikolojia ili wanapokuwa uwanjani wasiwe na presha au uoga kwa timu yoyote.

Anaongeza kuwa wanachotaka ni kuona hawashuki kwenye nafasi zao tatu za juu kwani msimu uliopita hawakuwa na matokeo mazuri jambo lililompa presha.

“Mengine ni mambo ya kiutawala, lakini sisi uwanjani tunahakikisha mpira umepigwa tumepata ushindi na mkakati ni kuona hatushuki nafasi tetu za juu.”

Hata hivyo, anaongeza kuwa licha ya matokeo waliyonayo, lakini kuna ugumu na ushindani mkali kwenye ligi na kwamba yeyote anayeteleza anaachwa.

“Ndio maana tumekuwa makini na kila mchezo, hatuna mechi ndogo sisi kwa sababu tunaona ugumu ulivyo, mtu anapoteleza mchezo mmoja anaachwa,” anasema kocha huyo.

Alia na FA

Mbeya City ndio ilikuwa timu ya kwanza Ligi Kuu kuondoshwa kwenye hatua ya 32 ilipokubali kuchomolewa na Ndanda ya Championship kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.

Kutokana na hilo, Lule anasema aliumizwa na matokeo hayo, kwani mbali na kutolewa ilikuwa mechi ya kwanza kutibuliwa nyumbani.

Anaeleza kuwa haikuwa mipango yao lakini wanakubaliana na matokeo, huku akieleza kuwa waliumizwa na hali hiyo ambayo hata mashabiki iliwagusa sana.

“Tulilenga kufanya vizuri katika michuano hiyo, lakini ilisikitisha sana kuona tunaondoshwa mapema sana na timu ya chini, lakini kufungwa nyumbani,” anasema.

Anasema kwa sasa wamesahau matokeo hayo na akili na nguvu zote ni kwenye mechi za Ligi Kuu ambazo hazina mtoano ili kuhakikisha wanafikia malengo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz