Mshambuliaji wa Biashara United, Helbert Lukindo amesema kwa sasa anaangalia zaidi kuhakikisha timu yao inatimiza malengo ya kupanda daraja kuliko kufikiria ufungaji bora wa ligi hiyo.
Lukindo amejiunga na Biashara Utd akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Pamba msimu uliopita timu zote zikiwa za Championship.
Mshambuliaji huyo amesema anafurahi kuona akiwa katika kiwango kizuri baada ya kufunga mabao matatu katika mechi tano lakini kwanza anaipa kipaumbele timu yake.
"Mimi ni mshambuliaji kila kitu kinawezekana, ninaweza kuchukua kiatu na ikitokea litakuwa ni jambo zuri katika maisha yangu ya soka.
"Malengo yangu ya kwanza ni kuhakikisha Biashara Utd inapanda kwa sababu ndio jambo ambalo lipo hapa kwa sasa na tunaendelea nalo."
Kinara wa mabao katika Championship ni Maulid Shaban wa Mbeya City akifunga mabao manne.