Mara baada ya kuripoti kambini na kushuhudia nyota wenzake wapya waliosajiliwa, kiungo wa Simba Luis Miqquissone ameibuka na kutamka kuwa msimu ujao kwa kuanza atahakikisha wanarejesha makombe yote ya ndani.
Makombe hayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Azam Sports ambayo yamechukuliwa na Yanga ndani ya misimu miwili mfululizo ambayo pia wamepanga kuyabakisha tena msimu ujao.
Kiungo huyo ambaye ni raia wa Msumbiji amejiunga na Simba katika dirisha hili kubwa la usajili akitokea Al Ahly ya nchini Misri.
Akizungumza nasi, Luis alisema kuwa kwanza anajisikia furaha kurejea tena kwa mara ya pili Simba ambayo tangu ameondoka msimu 2019-20 timu hiyo, haikubeba taji lolote.
Luis alisema kuwa, anaamini malengo yake yatafanikiwa katika msimu ujao ya kurejesha makombe hayo yote yaliyochukuliwa na watani wao wa Jadi, Yanga kutokana na usajili bora ambao wameufanya.
Aliongeza kuwa pia wana kibarua kingine cha Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ambacho ni kuhakikisha anaifikisha timu katika nafasi nzuri ikiwemo hatua ya nusu fainali baada ya kufika mara kwa mara hatua ya robo fainali.
“Kwa siku hizi mbili ambazo nimekaa na wachezaji wenzangu kambini Uturuki, nimeshuhudia viwango bora vya wachezaji ambao wamesajiliwa katika msimu ujao ninaamini utakuwa msimu wa mafanikio.
“Hivyo basi mimi na wachezaji wenzangu wengine wapya na tuliowakuta lengo letu ni kuhakikisha msimu ujao tunamaliza tukiwa na Makombe yote muhimu, na kufanya vyema Kimataifa.
“Ninaamini hilo linawezekana kwetu, kwani tutapambana kuhakikisha tunatengeneza muunganiko mzuri ambao utakuwa na tija ndani ya timu, kikubwa mashabiki watuunge mkono kwa kutusapoti uwanjani,” alisema Luis.
Katika hatua nyingine kiungo mshambuliaji, Msenegali Pape Ousmane Sakho aliyeuzwa Klabu ya Quevilly Rouen Metropole (QRM) ya nchini Ufaransa amebariki jezi yake namba 10 kukabidhiwa Luis.