Hakika Dar es Salaam imempata mtu wake, Ukiupenda mpira utampenda tu Luis Miquissone.
Miquissone ni kati ya wachezaji wachache waliotembeza upako wa soka katika Jiji hili la maajabu. Aliiteka Dar es Salaam.
Hizi kelele unazozisikia mjini hapa ni kwa hisani yake. Kwanini usimfurahie mtu anayekokota mpira huku unyayo ukiwa juu ya mpira? Mtu mwenye uhakika wa kila touch yake ndani ya uwanja, Kwanini usimfurahie?
Kwanini vinyweleo vya mwili wako visisimke kwa hisia kali baada ya kumwona mtu mwenye uwezo wa kukatiza katikati ya kundi la wapinzani kwa kasi ya umeme? Mtu mwenye uhakika wa kutumia miguu miwili pasipo na shaka yoyote! Kwanini usifurahie urejeo wake ?
Miquissone, Anaipa uhakika timu yake mabao ya kila aina, Ana uwezo wa kutumia vizuri mipira iliyokufa, achilia mbali hizo mbwembwe zake zenye majibu ya kila swali gumu kutoka kwa walinzi.
Ukitaka akutengenezee bao kupitia kona, muamini. Ukitaka mabao ya mbali, pia, muamini. Kingine kinachofurahisha zaidi ni uwezo wake wa kuusoma mchezo.
Anajua wakati gani wa kukokota mpira na kuachia. Muda upi wa kukimbia au kutembea, Kila anachofanya ni shangwe kwa mashabiki wake.
Anazielewa mno ‘frequence’ za mpira, kila beki aliyecheza dhidi ya Konde Boy wote walitulizwa na sehemu ya ubongo wa kiungo huyo. Ni ngumu sana kucheza na Konde boy aliye katika kilele cha ubora wake.
Konde boy ni mchezaji wa kipekee, Amekopeshwa imani na mashabiki wa Simba, sina shaka na marejesho yake ya kuwaonyesha uwezo aliobarikiwa.
Konde boy karejea nyumbani, Magazeti hayataacha kuandika habari zake, Anaelewa fika yupo Kariakoo iliyo ndani ya Jiji la Dar es Salaam, mengi yasiowezekana kwingine, hufanyika kirahisi sana hapa.
Agosti 6 atapata nafasi ya kuonekana kwa mara ya kwanza katika uzi wa Simba SC katika kilele cha Simba Day, na zaidi kuna uwezekano wa kucheza mchezo wake wa kwanza ndani ya Simba tangu asajiliwe.
Je ataacha habari gani midomoni mwa mashabiki na wapenda kandanda nchini?