Fowadi mpya wa Azam FC, Franklin Navarro aliyesajiliwa kutoka Amerika Kusini, amesema yupo tayari kuanza mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara, licha ya kukiri anakabiliana na changamoto ya lugha, vyakula na mazingira.
Navarro ambaye alikuwa akiichezea Inter Palmira ya kwao Colombia, alisema anaamini kadri ambavyo siku zitakuwa zikisonga mbele mambo yataendelea kumnyookea akiwa na Mcolombia mwenzake Yeison Fuentes (21) aliyetokea Leones FC.
“Kucheza Afrika ni jambo jema kwa ajili ya kupata uzoefu mwingine kwenye maisha yangu ya soka. Kiukweli nasubiri kwa hamu kuanza kucheza mechi za ligi ya Tanzania. Nimekuwa nikipewa ushirikiano wa kutosha kutoka kwenye benchi la ufundi na hata wachezaji wenzangu japo muda mwingine mawasiliano ni changamoto,” alisema na kuendelea:
“Imetubidi kuanza kujifunza Kiswahili na kwa bahati nzuri kwa sasa tunajua namna ya kusalimia. Tukiwa uwanjani ambacho kinaongea huwa ni miguu na ninashukuru kuona wachezaji wenzangu wakijitahidi kutusoma na sisi tumekuwa tukiwasoma na kujua namna ya kucheza nao.”
Navarro na Fuentes wanaongea Kihispaniola hivyo imekuwa changamoto upande wao kufanya mazungumzo ya kina na wachezaji wenzao japo wamekuwa wakipenda kucheza na kufurahi na wenzao kwenye kikosi hicho, huku kukiwa na jambo la ndani zaidi yupo kiongozi ambaye amekuwa akielewana nao.
Wacolombia hao wamekuwa wakijituma katika mazoezi ambayo yanaendelea Azam Complex, Chamazi ambayo Navarro anaonyesha kuwa na uchu na nyavu, hivyo mabeki wa Ligi Kuu wanapaswa kujiandaa naye kwani ni mshambuliaji mwenye kasi na maarifa kama ilivyo wachezaji wengi kutoka Amerika Kusini.
Kwa upande wake, kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo alishaweka wazi mapema hawatawapa presha wachezaji hao hivyo huenda wakaanza kupewa nafasi taratibu kwa kupewa dakika chache za kucheza kwenye kikosi hicho ili kuzoea mikikimikiki ya ligi ambayo imerejea baada ya kusimama kwa wiki chache kufuatia ushiriki wa Taifa Stars kwenye fainali za Afcon huko Ivory Coast.
Februari 9, Azam itakuwa ugenini kucheza mchezo wa kiporo utakaokuwa wa 14 wa msimu huu katika Ligi Kuu dhidi ya Simba, na kama Navarro na Fuentes watapata nafasi ya kucheza watakuwa wachezaji wa kwanza kutoka Colombia kucheza ligi hiyo inayoshika nafasi ya sita Afrika kwa ubora kulingana na Taasisi ya Soka ya Kimataifa ya Historia na Takwimu (IFFHS), ikiwa imeporomoka kwa nafasi moja kutoka nafasi ya tano iliyokuwa inashikilia tangu mwaka juzi.