Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema kuwa timu hiyo haijafungiwa kusajili madirisha matatu na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kwa kosa la kuchelewa kumlipa madai yake.
Na badala yake, Eymael ambaye ni raia wa Ubelgiji amesema kuwa uamuzi uliotolewa na FIFA ni kuishinikiza Yanga kulipa madai yake ili isikumbane na adhabu hiyo.
Kauli hiyo ya Eymael imekuja muda mfupi baada ya mtandao mmoja wa Afrika Kusini kudai kuwa Yanga imefungiwa kusajili kwa madirisha matatu kwa kosa la kutomlipa kocha huyo.
"Nadhani walioandika taarifa hiyo wameripoti kinyume. FIFA walitoa uamuzi na pande zote tumejulishwa kwamba Yanga wanatakiwa kunilipa stahiki zangu ndani ya siku 45 na iwapo wakishindwa kufanya hivyo, kuna adhabu kubwa zaidi watapewa ikiwemo ya kufungiwa kusajili."
"Kwa hiyo hawajafungiwa kusajili. Wamejulishwa uamuzi wa kutakiwa kunilipa fedha zangu," alisema Eymael.
Eymael aliiongoza Yanga kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara ingawa alitimuliwa baada ya kutoa lugha ya kashfa kwa mashabiki wa Yanga.