Beki wa kushoto wa Young Africans, Joyce Lomalisa anaendelea vizuri licha ya jeraha alilolipata kwenye mechi ya Namungo FC na kushindwa kuendelea na mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex juma lililopita.
Beki huyo kutoka DR Congo alikanyagwa na Hashim Manyanya katika mechi ambayo Young Africans ilishinda bao 1-0 na hivyo kuibua hofu kama anaweza kukosekana kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi (Septemba 30).
Daktari wa Young Africans, Moses Etutu amesema kuwa beki huyo alikuwa na maumivu kwenye paja na baada ya kumfanyia vipimo waligundua damu imevilia kwa ndani na baada ya matibabu sasa anaendelea vizuri, wakipambana kuhakikisha anakuwepo kwenye mechi ijayo.
Young Africans inatarajia kuvaana na Al Merreikh ya Sudan katika mchezo wa mkondo wa pili wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini wiki mbili zilizopita.