Wakati tetesi za usajili zikimhusisha beki wa Yanga, Joyce Lomalisa kujiunga na Simba mwenyewe kaibuka na kuweka wazi kuwa yupo tayari kucheza timu yoyote Tanzania Bara lakini kwa masharti.
Lomalisa ambaye ni raia wa DR Congo aliyesalia kwenye kikosi cha Yanga, anamaliza mkataba wake na mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia kwa misimu miwili akitwaa mataji ya ndani na kucheza hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lomalisa ambaye mashabiki wanamkubali kutokana na umahiri na umbo lake la kiuchezaji na uwezo wa kumwaga majalo, alikiri kuwa bado ni mchezaji wa Yanga kwa mujibu wa mkataba ambao ameweka wazi kuwa unamalizika mwisho wa msimu huu.
"Mimi bado ni mchezaji wa Yanga watu ndio wanaandika wanachojisikia mwisho wa msimu kila kitu kitajulikana kwasababu ndio mkataba unamalizika hivyo kama ntabaki au ntaondoka kila mmoja atafahamu," alisema na kuongeza;
"Napenda kubaki Yanga lakini hawajanifuata kwaajili ya mazungumzo ya mkataba mpya nimebakiza mwezi mmoja tu hakuna mazungumzo yoyote hivyo kama kuna timu zinahitaji huduma yangu zinatakiwa kuwasiliana na meneja wangu yupo Angola," alisema.
Lomalisa alisema yupo tayari kwenda timu yoyote ambayo itampa kipaumbele cha kucheza kama ilivyo kwa Yanga sasa ambayo amekiri kuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza.
"Mchezaji unaenda kwenye timu ambayo una uhakika wa kupata maisha mazuri na kutumikia mkataba wako kwa usahihi kuanzia kucheza na kuipa timu matokeo hivyo ili nitoke hapa natakiwa kuzingatia hivyo vitu," alisema.
Akizungumzia hali ya afya yake baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountaine Gate Yanga wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0, alisema anaendelea vizuri na ameanza mazoezi ya gym.
"Naendelea vizuri,ninaanza mazoezi hivyo naamini mechi inayofuata naweza kupata nafasi ya kurudi kucheza," alisema na kuongeza;
"Nikiwa fiti nina uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza hiki ndio nakitaka ikitokea nikapata nafasi ya kuondoka Yanga timu ambayo bado natamani kuendelea kuitumikia lakini sioni nafasi kutokana na viongozi kutokufanya mazungumzo na mimi hadi muda huu," alisema.
Mwanaspoti limeambiwa kwamba Yanga wanafanya uamuzi mgumu kwa nyota wake wawili wa nafasi ya ulinzi ya beki ya kushoto, Lomalisa Mutambala na Nickson Kibabage.
Watambakisha kikosini staa huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ambaye anacheza kwa mkopo kutokea Singida Fountain Gate akichukua nafasi ya Mcongo huyo anayetimka mwisho wa msimu akihusishwa na Simba.
Kibabage alikuwa Yanga kwa mkopo ambao unaisha mwisho wa msimu huu lakini viongozi wa Yanga hawajakubali kumpoteza beki huyo damu changa ambaye anafunga na kutoa asisti za mabao.
Ipo hivi; Uongozi wa Yanga umekubaliana kuachana na Lomalisa na kumalizana na Singida Fountaine Gate kwa kumnunua Kibabage na kumpa mkataba mpya wa miaka mitatu kwa dau la Sh250Mil na mshahara mnono.
Kibabage alikuwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na Singida Fountaine Gate hivyo Yanga wamefanya biashara na walima zabibu hao kwa kujimilikisha beki huyo ambaye Simba walishapeleka ofa ya kumtaka kwa dau la Sh100Mil.
Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Singida Fountaine Gate, Hussein Masanza ambaye amekiri Yanga kufika mezani kwaajili ya mazungumzo juu ya kumnasa beki huyo.
"Yanga wameonyesha kuvutiwa na beki huyo kwani wamerudi mezani kutaka kummiliki wao sio kuendelea kucheza kwa mkopo kama ilivyo sasa," amesema na kuongeza;
"Ni kweli wamekuja na mazungumzo kati ya pande zote mbili yanakwenda vizuri mambo yakienda kama tulivyopanga basi taarifa itatolewa kwaajili ya kuujulisha umma juu ya mchezaji huyo."
Kibabage ambaye hadi sasa ndani ya kikosi cha Yanga ametoa pasi tatu zilizozaa mabao alijiunga na timu hiyo Julai mwaka jana na baada ya mkataba wake wa miezi sita kuisha walimuongeza miezi mingine sita.